20 wafariki wakikimbilia mafuta ya upako kwa kiongozi wa kanisa

 

Watu 20 wafariki dunia mjini Moshi walipokuwa wakikusanyika katika viwanja vya Majengo kuhudhuria Ibada iliyoongozwa na Mtume Boniface Mwamposa.

Watu hao wamefariki dunia baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta ya upako.

Katika tukio hili watu 16 wamejeruhiwa.

Kiongozi wa kanisa la Inuka Uangaze, anayejitambulisha kama nabii na mtume Boniface Mwamposa , hii leo amelazimika kusitisha ibada kwa ajili ya kuitikia wito wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Tanzania kulikotokea vifo vya waamini wake.

HospitaliHaki miliki ya pichaGODFREY THOMAS , AYO TV
Image captionBaadhi ya waumini wakiwa hospitali

Mwamposa ambaye huendesha ibada zake katika eneo la Tanganyika Packers, leo Jumapili Februari 2, Nabii huyo amelazimika kufupisha ibada ya kwanza na kuanza safari ya kuelekea Moshi alikoitwa na polisi.

Ibada huwa inaisha majira ya saa saba lakini leo imeisha saa nne na nusu asubuhi.

Gazeti la Mwananchi limeandika kuwa jana katika kongamano lake la kukanyaga mafuta ya upako mkoani Kilimanjaro, watu 20 walipoteza maisha wakisukumana kukanyaga mafuta hayo.

Wakati hayo yakiendelea, waumini wa nabii huyo wamemkingia kifua na kueleza suala la watu kukanyagana kwenye mikutano mikubwa ni kawaida.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wakitoka katika Ibada huko Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Magufuli ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.

Idadi ya vifo vya watu huenda ikaongezekaHaki miliki ya pichaGODFREY THOMAS , AYO TV
Image captionIdadi ya vifo vya watu huenda ikaongezeka

Aidha amemtaka mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro bi. Anna Mghwira kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.

Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote kuchukua tahadhali katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vinasimamia ipasavyo tahadhali za kiusalama. (bbc)