Ajitia mafichoni akidaiwa kubaka mapacha Pemba

 

IMEANDIKWANA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, linaendelea kumsaka kijana Issa Khalid Rashid, anaetuhumiwa kuwabaka watoto wawili mapacha eneo la Wingwi Wilaya ya Michweni Pemba.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mohamed Shehan Mohamed, alisema  bila ya halali, mtuhumiwa huyo aliwabaka ndugu hao mapacha wenye umri wa miaka 17 kwa kila mmoja.

Alieleza kuwa, tukio hilo lilitokea baina Novemba 10 majira ya saa 3:00 asubuhi na Novemba 14 mwaka huu saa 5:00 asubuhi kijiji cha Wingwi Wilaya ya Micheweni mkoani humo.

Kamanda Shehan, alisema kuwa baada ya kutenda kosa hilo mtuhumiwa alikimbia, ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta  na atakapopatikana, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Mtuhimiwa huyu amefanya unyama mkubwa wa kuwabaka ndugu wawili mapacha, kwani wanaweza kuathirika kisaikolojia na kimwili, hivyo tunaendelea kumtafuta, ili afikishwe mahakamani”, alisema Kamanda.

Kamanda huyo, aliitaka jamii kuacha muhali zinapotokezea kesi hizo, ili kuweza kufanikiwa kutokomeza vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto.

“Uhalifu huu sana hufanywa na ndugu wa karibu na majirani, jambo ambalo, linasababisha jamii kuwa na muahali, hivyo tusioneane aibu, vinapotokea vitendo hivyo turipoti kwenye vyombo vya sheria”, alisema.

Aidha alieleza kuwa, ushirikiano unahitajika zaidi katika kuhakikisha jamii, inakuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi wakati wanapoitwa kwenye vyombo vya sheria, ili kuweza kumtia hatiani mtuhumiwa, iwapo atabainika na kosa.

“Bila ya ushahidi huwezi tu kumtia hatiani mtuhumiwa, kuna baadhi ya wanajamii, wanakuwa wagumu kutoa ushahidi, baadae wanakaa na kusema hakuna hukumu inayotolewa, hivyo tushirikiane”, alieleza Kamanda.

Kamanda huyo pia aliitaka jamii kuwa makini kwa watoto wao sambamba na kuwafuatilia nyenendo zao, jambo ambalo litasaidia kudhibiti vitendo hivyo.

“Watoto tusiwaachie sana kuzurura, tuwe nao karibu muda wote, ili kuwaepusha kufanyiwa vitendo hivyo”, alieleza.

Kubaka ni kosa kisheria kinyume na kifungu cha 108 cha Sheria ya adhabu, Sheria namba 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzibar, ambapo kifungu cha 109 kimetaja adhabu ambayo katika mazingira yeyote ni kifungo kisichopungua miaka 30 chuo cha mafunzo na faini au vyenginevyo ni kifungo cha maisha.

                                              MWISHO.