Alala rumande Pemba kwa tuhuma za kudakwa na kete 1,037 za dawa za kulevya

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

KIJANA Nassor Khamis Nassor miaka 22 mkaazi wa shehia ya Mgogoni wilaya ya Chake Chake na Michenzani Unguja, ameswekwa rumande, akikabiliwa na tuhma za kupatikana na kete 1,037 za dawa zinazoaminika kuwa ni za kulevya.

Ilidaiwa kwenye mahkama ya Mwanzo Chake Chake na Sajenti Juma Habibu wa mahkama hiyo kuwa, mtuhumiwa huyo alipatiana na kete hizo aina ya heroin, zenye uzito wa gramu 21.67, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Katika kesi hiyo ambayo ni ya mahkama ya Mkoa, ilisomwa kwenye mahakama hiyo kwa dharura ya kiofisi, baada ya Mwendesha mashtaka na hakimu husika, kutokuwepo mahakamani hapo.

Kabla ya Mwendesha Mashtaka huyo kutoka Jeshi la Polisi Sjent Juma Habibu, hajaanza kumsomea mtuhumiwa huyo tuhuma zake, Hakimu wa mahkama ya Mwanzo, Hashim Kassim alimueleza kuwa, hatotakiwa kujibu lolote.

Hakim alisema mtuhumiwa hatopewa nafasi ya kusema jambo lolote ndani ya mahakama hiyo, kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumsikiliza kisheria.

“Mtuhumiwa unataka kusomewa tuhuma zako za kupatikana na kete 1,037 zinazoaminika kuwa dawa za kulevya aina ya ‘heroin’ lakini hapa utasomewa tu na Mwendesha mashtaka, lakini hutotakiwa kusema jambo, maana mahakama yangu haina uwezo kisheria,’’alisema hakimu huyo.

Baada ya maelekezo hayo ya Hakimu huyo kwa mtuhumiwa huyo, alimpa nafasi Mwendesha Mashtaka na kumsomea mtuhumiwa shauri hilo, la kupatikana na dawa za kulevya.

Maara baada ya kumaliza kumsomea mtuhumiwa huyo shauri hilo,  huku akiwa tulii mahakamani hapo, hakimu alimpangia Febuari 24, mwaka huu kwenda kwenye mahkama husika.

Ilidaiwa kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 2 mwaka huu, majira ya saa 11:00 jioni, eneo la Chanjaani Chake Chake, ambapo mtuhumiwa huyo alipatikana nakete 1,037 zinazoaminika kuwa ni za dawa za kulevya, zenye ujazo wa gramu 21.67.

Kufanya hivyo ni kosa, kinyume na kifungu 15 (1) a cha sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama ilivyorekebishwa na sheria namba 12 ya mwaka 2011, samba mba na sheria namba 1 ya mwaka 2019 sheria ya Zanzibar.

 Mwisho