Aliembaka mjukuu wake Pemba tarehe za mahakama zamchanganya

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTUHUMIWA Ridhiwan Khamis Juma wa Wawi Chake chake, anaedaiwa kumbaka mjukuu wake, ameshindwa kutokeza mahakamani akitokea rumande, ikidaiwa kua, ni siuntafahamu ya tarehe aliotakiwa kuwasili mahakamani, kusikiliza shauri lake.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Chakechake, Hashim Kassim, aliuuliza upande wa mashitaka uliokuwa ukiongoza na sajenti Juma Habibu kutoka jeshi la Polisi, juu ya taarifa za mtuhumiwa kutoonekana mahakamani.

Ndipo Mwendesha mashitaka huyo, alidai kua, taatrifa kutoka rumande zinaeleza kua, mtuhimiwa alichanganya tarehe husika aliotakiwa kufika mahakamani, na ile ya kusikiliza ombi lake la dhamana.

Mwendesha mashitaka huyo kwenye mahakama ya mwanzo, alidai kua, huwenda mtuhumiwa alijua tarehe yake ya kufika mahakamani ni Januari 14 na sio Januri 13 ambayo kesi yake iliokua inaendelea.

“Muheshimiwa hakimu mimi sio mwendesha mashitaka husika wa shauri hili, maana shauri liko mahakama ya Mkoa Chakechake, lakini nilipofuatilia tulielezwa kua, mtuhumiwa alichanganya tarehe baina ya leo na kesho,’’alidai.

Hata hivyo mwendesha mashitaka huyo, alidai kuwa shauri lipo kwa ajili ya kutajwa, lakini kutokana na mwendesha mashitaka husika kutofika mahakamani, aliomba lighairishwe na kulipangia tarehe nyingine,’’alidai.

Mara baada ya kumaliza maelezo hayo, hakimu wa mahakama hiyo ya mwanzo Hashim Kassim, alisema kua pamoja na mtuhumiwa kutokuwepo mahakamani, lakini shauri hilo hawezi kulitia mkono kwa vile ni la mahakama ya Mkoa.

Hakimu huyo alisema kua, shauri hilo ni mahakama ya mkoa, hivyo ni vyema mtuhumiwa huyo, kufika tena mahakamani hapo, Januari 27 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na shauri lake.

Kabla ya kulipangia tarehe hiyo, hakimu huyo alimuuliza wakili wa upande wa utetezi Zahran Mohamed Yussuf, ikiwa anapingamizi na maelezo ya upande wa mashitaka.

Wakili huyo, alijibu kwa kumueleza hakimu kua, hana pingamizi na maelezo ya upande wa mashitaka, na kuiomba mahakama hiyo kulighairisha na kulipangia tarehe nyingine.

“Kama ndio hivyo,  mahakama inaligharisha shauri hili hadi Januari 27, mwaka 2020 na siku hiyo mtuhumiwa afike kwenye mahakama yake husika, na hakimu atakuwepo siku hiyo,’’alisema.

Awali mtuhumiwa huyo akiwa ndani ya mahakama ya mkoa ‘A’ Chakechake chini ya hakimu Abdull-razak Abdull-kadir Ali na Mwendesha mashitaka kutoka afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka, Mohamed Ali Juma, alidai kua mtuhumiwa huyo akijua kua ni kosa, alimbaka mjukuu wake.

Tukio hilo lilitokea katika tarehe isiofahamika mwezi Machi mwaka 2019, majira ya saa 7:00 mchana Wawi wilaya ya Chakechake Pemba.

Wakili huyo wa serikali alidai mahakamani hapo kua, siku hiyo alimuingilia mjukuu wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kufanya hivyo ni kosa, kinyume na kifungu cha 143 (1), (4) cha sheria ya Adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria halali ya Zanzibar, iliopitishwa na baraza la wawakilishi.

Kifungu hicho cha (4) kinaeleza kuwa, “iwapo itadaiwa kwenye taarifa au shtaka na ikithibitika kwamba, mtu mwanamke ana umri chini ya miaka 18, mkosaji mwanamme atapewa adhabu ya kifungo cha maisha

Ambapo kifungu cha (6) cha sheria hiyo hiyo, kinaeleza kua ‘iwapo mtu mwanamme anajaribu kutenda kosa lolote kati ya yaliotajwa, atakuwa ni mkosa, na atapewa adhabu ya kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka 10’

Taarifa za kihalifu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonesha kua, kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2017, kulikuwa na jumla ya watu 159 waliofanyiwa matendo ya kuingiliwa na maharimu wao, ambapo wanaume ni 141 walioripotiwa na wanawake walikuwa 18.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa ya kipolisi iliongoza ni Temeke 86, Singida 47, Dododma 7, Simiyu 5, Shinyanga 4,  Kagera 3, Tabora na Mara wawili wawili, wakati mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, na Mtwara kulikuwa na watu mmoja mmoja huku mikoa mitano ya Zanzibar hakukua na matukio ya aina hiyo kwa mwaka huo wa 2017.

MWISHO