Aliempiga mwenzake jiwe ataka mashahidi mahakamani

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTUHUMIWA anaedaiwa kumpiga jiwe mwenzake na kumvunja mguu, ameiomba mahakama ya Mwanzo Chake Chake, kuharakisha kuwapandisha mashahidi mahakamani, kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa fangasi na tumbo la kuharisha.

Mtuhumiwa huyo Takdiri Mohamed Khamis miaka 28 wa Pondeani Mtambile wilaya ya Mkoani, alidai hayo ndani ya mahakama hiyo kuwa, ambapo shauri lake lilikuwa likitaka kuahirishwa, kutokana na mahakama husika hakim kutokuwepo mahakamani.

Alidai kuwa, ni vyema upande wa mashtaka ukawapandisha mashahidi wa kesi yake, maana hali yake imekua ikizorota siku hadi huko rumande.

Alidai hayo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Hashim Kassim kuwa, amekuwa akiumwa na tumbo la kuharisha, fangasi na kuumwa na macho, hivyo amedai ni wakati sasa mashahidi kufikishwa mahkamani hapo.

“Mheshimwa hii ni mara pili, mimi nafika mahakamani kujakusikiliza mashahidi, lakini nikifika hawakupatikana, sasa naiomba mahakama yako tukufu iwalete, maana hali yangu sio ‘fresh’ naharisha na kisha nna fangasi,’’alidai.

Awali, mara baada ya mtuhumiwa kupanda kizimbani hapo akitokea rumande, mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo Sajenti Juma Habibu wa jeshi la Polisi alidai kuwa, shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikiliza mashahidi.

Alidai kuwa, pamoja na kwamba mwendesha mashitaka husika hakufika mahakamani, lakini hata hivyo kwa upande wake hajapokea mashahidi.

“Mheshimiwa shauri lililopo mbele yako la shambulio la kuumiza mwili, lipo kwa ajili ya kusikiliza mashahidi, lakini hatujawapokea na tunaiomba mahkama yako, iliaharishe na kulipangia tarehe nyingine,’’alidai.

Mara baada ya maelezo hayo, hakim huyo wa mahakama ya mwanzo Chake Chake Hashim Kassim, alimuuliza mtuhumiwa akiwa ameyasikia maelezo ya mwendesha mashtaka.

“Je mtuhumiwa umeyaskia maelezo ya upande wa mashtaka, kwamba hawajapokea mashidi,’’alimuuliza matuhumiwa na kujibu ndio na kuiomba mahakama hiyo kuwapandisha mashahidi.

Hivyo hakimu huyo, alimuamuru mtuhumiwa huyo kurudi rumande tena hadi Januari 27, mwaka huu ambapo siku hiyo kesi yake, itakuwa kwa hakimu husika na mashahidi watakuwepo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo alimshambulia Mkubwa Makame Faki, kwa kumpiga jiwe na kumvunja mguu wake wa kulia, tukio lililotokea Disemba 14, mwaka 2019 majira ya saa 1:00 usiku.

Kufanya shambulio la hatari ni kosa kinyume na kifungu cha 208 cha sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.

Ambapo kifungu hicho cha 208 kinaweka wazi kuwa, iwapo mahakama itamtia hatiani mtuhumiwa wa kosa hilo, adhabu yake ni kutumikia kifungo kwa kipindi kisichozidi miaka saba ’7’.

Wakati huo huo mahakama hiyo, imelighairisha shitaka la kuumizwa mwili linalomkabili Ali Hussein Ali miaka 29 wa Minazini Chake Chake, kutokana na kutokuwepo kwa mashahidi.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Disemba 12, mwaka jana, majira ya saa 8: 00 mchana eneo la Chachani Chake Chake, ambapo bila ya halali alimpiga ngumi za usoni na mbavuni na mkanda mkononi kijana Abdaillah Zamir Othman.

Aidha mtuhumiwa anadaiwa kumsababishia maumivu makali sehemu za mwili wake, jambo ambalo ni kosa kisheria kinyume na kifungu cha 230 sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.

Hivyo hakimu huyo wa mahakama ya mwanzo, aliliahirisha shauri hilo hadi Febuari 3, mwaka 2020 na kuutaka upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Mwisho