Alieshindwa kudhibiti vidole vyake Wawi Pemba yamkuta mapya

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa ‘B’ Chakechake, imemtupa chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka saba, kijana Talib Mohamed Khamis wa Wawi, baada ya kubainika kufanya kosa la shambulio la aibu kwa mtoto wa kike wa miaka 10 kwa kumpitishia vidole sehemu zake nyeti.

Hakimu wa mahakama hiyo, Lociano Makoye, aliridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita mahakamani hapo akiwemo mtoto mwenyewe, mama yake, dada, Polisi na daktari aliemfanyia uchunguuzi mtoto huyo.

Kesi hiyo kwa mara ya kwanza, ilifikishwa mahakamani hapo Disemba 11, mwaka jana, ambapo kijana huyo alikutikana na kosa kosa hilo, alililofanya eneo la Ditiwa Wawi Chakechake Pemba.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Seif Mohamed Khamis, kuwa siku hiyo ya tukio, kijana Talib majira ya 7:00 mchana, alimshambulia mtoto wa kike miaka 10, kwa kumchezea sehemu zake za siri jambo ambalo ni kosa.

Mwendesha Mashitaka huyo, aliielezea mahakama hiyo kuwa, kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 114 (1) cha sheria no 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

“Wewe Talib ulimtendea visivyo mtoto wa kike wa miaka 10, siku hiyo ya tukio, jambo ambalo unajua kuwa ni kosa, ‘’alieleza Mwendesha mashiataka huyo mahakamani hapo.

Baada ya maelezo hayo pamoja na ya mashahidi, Hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye, aliridhika na ushahidi huo usio na shaka na kumtaka mshitakiwa, atumikie kifungo cha miaka saba chuo cha mafunzo kuanzia August 1, mwaka huu.

Kabla ya hukumu huyo, mshitakiwa huyo aliomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu, kwa vile bado ni mdogo na anahitaji kufanya kazi za kujiletea maendeleo.

Wakati haya yanatokea, ripoti ya kihalifu ya Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2017, inaripoti kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka huo, jumla ya matukio 13,457 ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yaliripotiwa.

Idadi hiyo ni ndogo, ikilinganishwa na matukio 10,551 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2016, ambapo kwa mikoa ya kipolisi iliyoongoza ilikuwa ni Temeke ilioripoti matukio 2,426, Dodoma 1,283, Tanga 1,064.

Mikoa mengine ilioripotia matukio hayo kwa idadi kubwa ni Kinondoni 984 na Arusha 972, huku mikoa iliokuwa na idadi ndongo ni Viwanja vya Ndege mawili, Lindi 19, Kaskazini Unguja 29, Kaskazini Pemba 30 na Kusini Pemba 36.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ubakaji yaliokuwa 2,984, shambulio 2,752,  mimba mwanafunzi 1,323, shambulio la kudhuru mwili 1,293, Lugha ya matusi 1,218 na kujeruhi yalikuwa matukio 1,065.

 

                                 Mwisho