‘Aliyepatikana na kete 175 za bangi atakiwa kujitetea Mahakamani Pemba’

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa ‘B’ Chake Chake chini ya Hakimu Luciano Makoye Nyengo, imesema mtuhumiwa Bakar Nassor Said wa Vitongoji wilaya ya Chake Chake, aliepatikana na kete 175, zinazosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin, zenye ujazo wa gramu 7.8, anayo kesi ya kujibu.

Mahakama hiyo, iliyatamka hayo mara baada ya mtuhumiwa huyo, kukubali ushauri wa upande wa mashitaka, kwamba wayasome maelezo ya shahidi wa mpelelezi kama yalivyoandikwa, baada kuwepo mafunzoni kwa muda mrefu.

Upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha mashtaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Seif Mohamed Khamis, uliiambia mahakama kuwa, shahidi mpepezi hajapatikana kwa vile yuko mafunzoni.

Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa, shahidi huyo ni wa mwisho kwao, kama atarudi kuja kutoa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo, anaesadikiwa kupatikana na dawa za kulevya aina ya heroin.

“Mheshimiwa shauri hili lipo kwa ajili ya kusikilizwa, ingawa hadi sasa bado upande wetu hatujampokea shahidi wetu wa mwisho, ambae ni askari mpelelezi maana yuko mafunzoni,’’alidai.

Hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, alimuuliza mtuhumiwa huyo, iwapo ameyaskia maelezo ya upande wa mashtaka na ikiwa anakubaliana nayo.

Mtuhumiwa huyo, awali alikataa ushahidi wa askari huyo mpelelezi kusomwa kama ulivyoandiwa, pasi na yeye mwenyewe kuwepo, akidai kuwa ataendelea kustahamili.

“Mheshimiwa hakimu wacha mimi niendelee kuvuta subra huko rumande, mapaka atakaporudi huyo shahidi, au harudi tena, na mimi nahisi huyu ni muhimu sana kwangu,’’alihojia mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo Hakimu huyo, alimuwelewesha tena mtuhumiwa huyo, kuwa ushahidi wa mpelelezi huyo upo mikononi mwa upande wa mashtaka kwa njia ya maandishi, unaweza kusomwa na kuuskiliza, au utarudi tena rumande.

Baada ya maelekezo hayo, mtuhumiwa alikubali kuwa ushahidi huo ulioletwa kwa njia ya karatasi, usomwe na mwendesha mashtaka kama ulivyoandikwa na hana hofu yeyote.

Ndipo mwendesha mashitaka huyo, aliposimama na kuanza kuusoma ushahidi huo wa askari mpelelezi wa kituo cha Polisi Chake Chake, mwenye namba F 8121 dc Henry, huku akipata nguvu kupitia kifungu cha 34 (1) (2) cha sheria ya Ushahidi namba 9 ya mwaka 2016.

Ambapo kupitia maelezo ya ushahidi huyo, alidai kuwa Mei 18, mwaka jana majira ya saa 9:03 jioni, akiwa kazini kwake kituo cha Polisi Chake Chake, alikwenda Polisi wa kitengo cha kupamba na dawa za kulevya, mwenye namba F 4920 dc koplo Issa na kumkabidhia mtuhumiwa huyo.

Alidai kuwa, mtuhumiwa huyo wakati anakabidhiwa alikuwa na kielelezo chake, ambacho ni kete 175 za unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin.

Mwendesha mashtaka huyo Seif Mohamed Khamis kupitia ushahidi wa askari mpelelezi, ambae hakuwepo mahakamani hapo kwa dharura za kiofisi, alidai kuwa baada ya hapo alimfungulia mtuhumiwa taarifa za kihalifu.

“Baadaya kumpokea mtuhumiwa huyu ambae yuko mahakamani hapa, nilimfungulia taarifa zake na kisha kumtahadharisha juu ya kosa lake hilo,’’alidai.

Aidha maelezo hayo ya ushahidi yamedai kuwa, baada ya kuandika taarifa hizo, alikifungua kielelez hicho na kisha kuzihesabu kete hizo na kubaini kuwa ni 175, ambapo shughuli zote hizo zilishuhudiwa na mtuhumiwa na askari mwengine.

Baada ya mwendesha mashtaka huyo kumaliza kuusoma ushahidi huo wa askari mpelelezi, hakimu Luciano Makoye Nyengo wa mahakamani hapo, alimueleza mtuhumiwa huyo anayo kesi ya kujibu.

“Kwa ushahidi huu na mwengine uliotolewa, mtuhumiwa unaonekana unayo kesi ya kujibu na sasa utarudi tena rumande hadi Machi 30, mwaka huu kwa ajili ya utetezi wako,’’alisema.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo Bakar Nassor Said miaka 22, Mei 18 mwaka jana majira ya saa 8:05 mchana eneo la Vitongoji Fidel Castro wilaya ya Chake Chake, bila ya halali alipatikana na kete 175 za dawa za kulevya.

Kete hizo zinazosadikiwa kuwa ni za aina ya heroin zina uzito wa kilogram 7.8, jambo ambalo ni kosa, kisheria kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria ya Udhibiti wa dawa za kulevya, sheria namba 9 ya mwaka 2009.

Aidha hilo ni kosa pia kama ilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 11 (a) cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.

Mwisho