Amani, utulivu watawala mitihani kidato cha nne Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, imesema mitihani ya kidato cha nne, inaendelea vyema kisiwani humo na hadi sasa hakujaripotiwa tukio lolote la ukiukwaji wa kanuni, sheria na taratibu nyingine za mitihani.

Afisa Mdhamini wizara hiyo, Mohamed Nassor Salim, alisema tayari ameshatembelea skuli kadhaa kisiwani Pemba na hajaripotiwa na wala hajakumbana na kesi yoyote ya maajabu kwenye vyumba vya mitihani.

Alisema, bado hali ya utulivu na usalama ingali inatawala kwenye skuli zote za serikali na binafsi, huku wanafunzi hao wa kidato cha nne wakiendelea na mitihani yao kwa utulivu.

Alisema, hilo linawezekana limesababishwa na vikao pamoja na mikutano ya mara kwa mara, iliyokuwa ikifanywa na wizara, skuli na baadhi ya taasisi juu ya kudumisha nidhamu katika kipindi chote cha mitihani.

“Kwa kweli hadi sasa tunashukuru, mitihani ya (darasa la kumi na mbili) kidato cha nne kisiwani Pemba inaendelea vyema na tunashkuru hakujaripotiwa tukio ambalo sio la kawaida”, alisema.

Hata hivyo Afisa Mdhamini huyo, alisema bado sheria zipo pale pale kwa msimamizi, mwanafunzi au mzazi na atakeshawishi au kusaidia kufanya udanganyifu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi.

Alieleza kuwa, sheria ziko wazi, kwa mtu au kundi la watu ama taasisi itakayogundulika kufanya udanganyifu au kusababisha kuchafua amani ndani au nje karibu ya chumba cha mitihani, sheria itatumika.

Katika hatua nyingine Afisa Mdhamini huyo, amewataka wanafunzi waendelee kujiamini na kuwa watulivu katika kipindi chote cha mitihani ya taifa, ili imalizike kwa salama na amani kama ilivyoanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Shehan Mohamed Shehan, alisema ni kweli hadi sasa mkoa uko shuwari hasa kwenye eneo la mitihani, na kusema kuwa hadi Novemba 7 hakujaripotiwa tukio lolote la udanganyifu.

“Hadi sasa mitihani inaendelea vyema na hakuna msimamizi, mwanafunzi, mzazi au mtu mwingine aliedaiwa kuivuruga au kufanya udanganyifu wowote”, alieleza.

Baadhi ya wanafunzi waliokataa kutaja majina yao, walisema mitihani imeanza vyema, ingawa usimamizi umekuwa nzito mno, jambo ambalo linawatia hofu.

Walisema, wasimamizi wamekuwa wakiranda randa kila wakati jambo ambalo huwakosesha umahiri na utulivu wa akili wa kujibu mitihani hiyo ambayo kwao walisema ni ya mwisho.

“Ni vyema wasimamizi wakawa na utulivu wa hali ya juu na kama hakuna shida, waache kuzunguruka zunguruka ovyo ndani ya vyumba vya mitihani, kwani wanatutia wasiwasi,’’walisema.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi hao wamewataka wanafunzi wenzao ambao wanahisi kuna masuali magumu na wanashindwa kuyajibu wawe watulivu na muda wa kutoka ukifika watoke taratibu.

Afisa Elimu sekondari Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad alisema, sio busara sana kwa wasimamizi kuzunguruka ovyo madarasani, ikiwa hakuna haja hiyo.

Alisema, yeye anavyoamini kama wasimamizi hawana shaka na mwanafunzi, hawawezi kutembea tembea ovyo darasani, inawezekana hata wakifanya hivyo, wamembaini mwanfunzi ana mashaka.

“Mimi niwaombe wanafunzi kwanza wawe watulivu wao kwenye vyumba vya mitihani, ili na wasimamizi nao watakuwa watulivu, maana wale wako kazini na moja ya kazi zao ni kufichua udanganyifu”, alieleza.

Nae Afisa Elimu sekondari mkoa wa Kusini Pemba Mwalimu Haji Kombo, alisema hata mkoani humo, utulivu umetawala kwenye skuli zote, zinazoendelea na mitihani ya taifa.

Alisema cha msingi ni kwa wanafunzi kuendelea kuheshimu misingi, sheria na kununi za mitihani ili imalizike salama kama ilivyoanza.

Mitihani ya taifa ya kidato cha nne Tanzania ambayo ilianza Novemba 4, kwa masomo mawili ya lugha ya kiengereza na soma la uraia ‘civics’ wakati Novemba 5 wanafunzi walifanya somo la Bilologia na historia, ambapo mitihani hiyo inatarajiwa kumalizika Novemba 18 nchini kote.

                          Mwisho