Bodaboda kuruhusiwa Zanzibar

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, imesema baada ya kufanya marekebisho ya sheria na kanuni itazisajili bodaboda.

Waziri wa wizara hiyo, Dk.Sira Ubwa Mwamboya, alieleza hayo jana wakati akiwasilisha taarifa ya serikali kuhusu hoja binafsi ya mjumbe wa baraza la Wawakilishi, Mohamed Dimwa kuhusu usafiri huo.

Alisema miongoni mwa vyombo hivyo ni pamoja na usafiri wa pikipiki ambapo serikali itazipatia namba za usajili kuwa za biashara pamoja na kuzipatia leseni za kusafirisha abiria nchini.

Alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria namba 7 ya 2003 na kanuni zake, serikali imeandaa utaratibu utakaowezesha kurasimisha usafiri wa bodaboda kuwa ni miongoni mwa aina za biashara za usafirishaji abiria.

“Kifungu cha pili cha sheria kitafanyiwa marekebisho kwa kuongeza maana ya ‘tax motorcycle’ kwa sababu usafiri huo utakuwa ni sawa na usafiri mwengine”.

Alisema katika kifungu cha 48(2) cha sheria pia kitafanyiwa marekebisho kwa kuongeza ‘tax motorcycle’ katika vyombo vinavyoruhusiwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria.

Wajumbe wa baraza hilo waliwataka wahusika wa biashara ya bodaboda kufuata taratibu na sheria zitakazowekwa na serikali.