Bodi ya Mikopo elimu ya Juu Z’bar yaja na mbinu mpya

Imeandikwa na Haji Nassor – Pemba

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar ‘BMEJZ’ imesema, imeshabuni njia nyingine ya kuwafuatilia wadaiwa wa bodi hiyo, hasa ambao wameshaajiriwa na wamekaa kimnya bila ya kuiarifu bodi hiyo, ikiwa ni pamoja na kumshughulikia mdaiwa mmoja moja.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa bodi hiyo kisiwani Pemba Ahmada Omar Juma, alipokuwa akijibu hoja za maafisa utumishi na wahasibu wa serikali, kwenye mkutano wa kubuni mbinu ya urejeshaji wa mikopo ya bodi hiyo, uliofanyika baraza la mji wa Chakechake.

Alisema, kuelekea mwaka 2020, bodi hiyo sasa imeamua kufuatilia wadaiwa kwa mtindo mwengine, ikiwa ni pamoja na kwenda kwenye wizara moja moja na kumshughulikia mdaiwa mmoja moja, ambapo ziara hiyo, itambatana na adhabu ya shilingi 50,000.

Alisema kuwa, wapo wadaiwa wa bodi hiyo, baada ya kumaliza masomo na sasa wameshaajiriwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini hawajafika kwenye ofisi za bodi ya mikopo ya elimu juu, ambako ndiko walikokopeshwa fedha na kusoma elimu ya juu.

“Tunaomba kuwaarifu tu kwamba, wale wote wanaoipiga chenga Bodi ya mikopo, kwa kukaa kimnya bila ya kutoa taarifa ya kuanza kukatwa mishahara yao, sasa wajiandae tutawafuata mmoja mmoja, na tukiwagunuda wataandamwa adhabu ‘penalt’ ya shilingi 50,000 kila muda, hadi amalize deni,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, Mratibu huyo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kisiwani Pemba Ahmada Omar Juma, aliwataka wale wote wanaokopo kuelewa kuwa, fedha hizo sio ruzuku bali ni mkopo, unaohitajika kulipwa kwa wakati.

“Ukikopa ujue kuwa, kuna mdaiwa amesharejesha ndio maana na mwanafunzi mwengine akapata kukopo, sasa aliekopa akishindwa kurejesha anaukondesha mfuko wa Bodi,’’alieleza.

Mapema Afisa Mdhamini, wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salum, aliwataka maafisa hao kuvunja ukimnya na kuweka kando udugu na ujamaa kwa watumishi wanaodaiwa na Bodi hiyo.

Alisema, kama wanafikiria kufikia kwenye uzalendo uliotukuka, kwanza ni kuweka mbele maslahi ya taifa, ikiwa ni pamoja na kuwaibua na kuwapelekea taarifa zao kwa bodi, ili waanze makato.

Alisema serikali, imeweka mazingira bora na rafiki kwa wanafunzi wa Zanzibar, ili wasome bure kuanzia elimu ya maandalizi hadi sekondari, na kwa elimu ya juu imeweka mikopo yenye masharti nafuu zaidi.

Alisema mkopo unaotolewa na Bodi hiyo ndio pekee duniani kote, ambao unamasharti laini na hauna riba kwa mkopoji, kwa lengo la kuweka mazingira bora, ili wazanzibar wote wapate fursa ya kujisomea elimu ya juu.

“Nendeni popote mfuatilie aina ya mikopo inayotolewa, na kisha mfananishe na mkopo unaotolewa na wizara ya Elimu, basi mtaona huu wa kwetu, ni wa kiungwana zaidi,’’alifafanua.

Hata hivyo amewataka waajiri na wadhamini kuwahimiza wadaiwa, ili kufanya marejesho baada ya kumaliza kusoma, ili na wengine wapate fursa hiyo.

Baadhi ya washiri wa mkutano huo, wameitaka Bodi hiyo kuongeza kasi ya kufuatilia wadaiwa mbali mbali, hasa kwa vile sheria inawaruhusu hadi kuwafungulia mashitaka.

Mohamed Zubeir Ame, alisema lazima Bodi hiyo iweke pembeni urafiki na wafanye kazi kwa mujibu wa sheria inayowaongoza, ili wadaiwa wasidhani kuwa fedha hizo ni ruzuku.

Nae Tatu Abdalla Msellem, alisema wakati umefika kwa Bodi hiyo kuwatangaaza wale wadaiwa wa Bodi hiyo, sambamba na kuweka picha zao kwenye maeneo mbali mbali, inaweza kusaidia kufanya marejesho.

Kwa upande wake Mohamed Kombo Juma, alisema wakati umefika sasa kwa Bodi hiyo, kuzihama ofisi zao na kuhamia kwenye taasisi na mashirika mbali mbali, ili kuwatafuta wadaiwa wa bodi hiyo na kuanza makato.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar ‘BMEJZ’ imeanzishwa chini ya sheria no 3 ya mwaka 2011, miongoni mwa majukumu yake ni kutoa mikopo kwa wanafunzi, waliopata udahili katika vyuo vya elimu ya juu vya ndani ya nje ya nchi.

Jukumu jengine ni kukusanya na kusimamia marejesho ya mikopo yote ya elimu, iliotolewa kwa wanafunzi kuanzia mwaka 2006 kwa lengo la kuufanya utaratibu wa utoaji wa mikopo kuwa endelevu.

Tokea kuanzishwa kwa Bodi hiyo mwaka 2011 hadi mwezi Novemba mwaka 2019, bodi hiyo imeshapokea jumla ya shilingi bilioni 58.8, ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 55.2 zimeshatumika kutoa mikopo kwa wanafunzi na shilingi bilioni 3.6 zimetumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi na kazi nyingine.

                         Mwisho