CCM Kiwani Mkoani watakiwa kushirikiana

IMEANDIKWA NA HABIBA ZARALI-PEMBA

WANANCHI wa jimbo la Kiwani wilaya ya Mkoani Pemba, wametakiwa kushikamana na kushirikiana kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM), kwani ndio chama pekee kinachotekeleza ilani yake na kuwaletea maendeleo wananchi.

Mwakilishi wa jimbo la Kiwani, Mussa Fumu Mussa, aliyasema hayo Kendwa Kiwani, wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo katika mkutano wa kuzungumzia maendeleo yaliyofanywa jimboni humo kupitia mfuko wa Mwakilishi na serikali kuu kwa kutumia  ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Alifahamisha kwa kuwa CCM ndio kilichopinduwa kwa lengo la kuwakombowa wananchi na unyonge hivyo hakina budi kutekeleza Ilani yake kwa asilimia mia moja.

Alisema hadi sasa katika jimbo la Kiwani, Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeshafikia asilimia 95  jambo ambalo ni faraja kwa wananchi hao kutokana na kuwa na maendeleo Jimboni mwao.

“Jambo la muhimu ni kuzidisha umoja wetu tulionao, ili maendeleo yazidi kupatikana katika jimbo letu kwani kila mmoja anayahitaji katika kuendeleza maisha yake ya kila siku,”alisema.

Alieleza kuwa katika shehia nane ambazo zimo Jimboni humo zinafaidika na maji safi na salama, elimu, miundombinu ya barabara na umeme na kuahidi kuwa katika sehemu chache za ndani ambazo hazijafika huduma hizo watazipata kabla ya 2020 kwani lengo ni wananchi wote kuweza kufaidika nazo.

Alifahamsha kuwa katika Jimbo hilo limebahatika kuwa na kisiwa kidogo cha Shamiani Mwambe, ambacho nacho tayari kimeshafaidika na umeme, ambao ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika visiwa vyote vidogo kufikishwa huduma hiyo.

Katika hatuwa nyengine mwakilishi huyo aliwataka wananchi hasa vijana kutoshawishiana kujiingiza katika masuala ya udhalilishaji na madawa ya kulevya, kwani yanapelekea kuathiri nguu kazi ya taifa.

“Vijana tunapaswa kulinda vitendo ya udhalilishaji na madawa ya kuleya kwani yanapelekea kutowa akili na baadae nchi itakuwa haina mtu wa kuiendeleza,”alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mkoani, Issa Juma Ali, alisema katika masuala ya maendeleo ni vyema wananchi wakaachana na itikadi za vyama ambazo hazina muskakbali mzuri kwao.

Alisema maendeleo yanayofanywa jimboni yana mchango mkubwa kupitia Mwakilishi hivyo ni wajibu wa wananchi kuhudhuria katika mikutano hiyo kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa .

“Wakati mwengine munapoeleza changamoto zenu wenyewe inakuwa ni vizuri kwani nyinyi ni wengi munaona mengi huko munakoishi lakini Mwakilishi ni mmoja bila shaka atakayoona ni machache halafu changamoto zinazowakumba mnaziona njoni muziseme,”alisema.

Nae Katibu wa Chama wilaya, Muhamed Ali Abdalla, alisema hatua iliyofikia katika kutekeleza ilani jimboni humo inaridhisha na kuwataka vijana kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa wenye sifa pale utakapofika muda wake.

“Tuhakikishe wote wenye sifa wanajiandikisha, ili kuweza kutimiza wajibu wao,”alisema.

Mapema wakimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Shein kwa mazuri nayoyatenda diwani wa wadi ya Kengeja, Mshenga Haji Khamis na Diwani wadi ya Kendwa, Ishaka Hemed Juma, walisema  mazuri yanayofanywa kupitia serikali yako wazi kila mmoja anayaona.

Hivyo waliomba wananchi wote kuithamini na kuitunza miradi waliyonayo jimboni humo ikiwemo ya majisafi na salama,skuli, vituo ya afya, vyoo na hata barabara na umeme ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kufaidisha vizazi vijavyo. (chanzo: Zanzibar leo)