Daktari Chake Chake: ”Mwenyeulemvu wa akili aliingiliwa kweli”

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

DAKTARI wa hospitali ya Chake Chake kitengo cha mkono kwa mkono Ali Mzee Mrisho, amedai mahakamani kuwa, mwanamke mwenye ulemavu wa akili aliemchunguuza, alimbaini kuingiliwa na kuondoka kabisa uzima.

Daktari huyo ambae ni shahidi nambari nne, kwenye shauri la tuhuma zinazomkabili kijana Abdalla Khatib Abdalla za kumuingilia mwanamke mwenye ulemavu wa akilil alidai kuwa, aligundua hayo baada ya vipimo vyake.

Alidai kuwa, alibaini kuwepo kwa uwazi wenye kupita vidole viwili vya mtu mzima, wakati mwanamke huyo alipofikishwa kituoni kwake, kwa tuhuma za kuingiliwa kimwili.

Daktari huyo huku akioongozwa na wakili wa serikali Juma Ali Juma, aliiambia mahakama ya Mkoa ‘B’ Chake Chake chini ya Hakim Luciano Makoye Nyengo kuwa, alimpokea mwanamke huyo akiwa na fomu ya matibabu PF3 kutoka kituo cha Polisi.

“Ni kweli, wakati nikiwa kwenye kituo changu cha kazi cha Mkono kwa mkono hospitali ya Chake Chake, nilimpokea mwanamke huyo, akihitaji huduma na nilimfanyia kama taratibu zilivyo,’’alidai.

Mara baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake, Hakim Luciano alimtaka mtuhumiwa huyo, kumuuliza mwaswali shahidi daktari ikiwa anayo.

“Mtuhumiwa umemsikia daktari maelezo yake alioyatoa kupitia uchunguuzi wake, na mahakama imeshapokea fomu ya PF3 kama kielelezo cha alichokisema, sasa kama unamaswali muulize,’’Hakimu alimpa nafasi mtuhumiwa.

Ndipo mthumiwa huyo, alipotaka kujua kutoka kwa daktari huyo, kuna njia ngapi ambazo mwanamke anaweza kuondoa uzima ‘bikra’ kutokana na utaalamu wake wa muda mrefu kazini.

Aidha mtuhumiwa huyo, ambae alikaukiwa na maswali kwa daktari huyo, alimtaka ataje njia hizo na kuzitaja kuwa ni pamoja na uume, vidole, jiti na jambo jengine lenye ncha kali.

Mara baada ya maswali hayo ya mtuhumiwa, Hakimu aliuuliza upande wa mashitaka, ikiwa wana jambo lolote, ndipo Wakili huyo wa serikali Juma Ali Juma, alipodai kuwa, wameshafunga ushahidi dhidi yao.

Hivyo Hakaimu Lucino, alimueleza mtuhumiwa huyo, sasa anayo kesi ya kujibu na kumtaka akajipange kwa ajili ya utetezi na wakutane hapo Machi 30, mwaka huu na yeye kurudishwa rumande.

“Mahkama imekuona una kesi ya kujibu mtuhumiwa, sasa kajipange pange ukija tena mahakamani hapa, iwe ni kwa ajili ua utetezi pekee, ‘alisema Hakim huyo.

Awali mtuhumiwa huyo alidaiwa kuwa, Juni 24 mwaka jana majira ya 1:15 asuhuhi, eneo la Pujini wilaya ya Chake Chake, isivyo halali alimuingilia kimwili mwanamke mwenye ulemavu wa akili miaka 18.

Ilidaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo Abdalla Khatib Abdalla, alifanya tendo hilo huku akijua kuwa, muathirika ni mwenye ulemavu wa akili, ambapo ni kosa kinyume na kifungu cha 116 (1) sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018.

Mwisho