Daktari mtoa mimba Pemba mikononi mwa Polisi

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

DAKTARI mstaafu anaeishi mjini Chakechake Nassor Khalid Mohamed miaka 56 na wateja wake wawili, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba, wakituhumiwa kwa kula njama ya kutoa mimba, kwa mwanamke wenye umri wa miaka 21.

Awali, Jeshi hilo la Polisi kabla ya kuwashikiliwa watuhumiwa hao, walipokea taarifa kutoka kituo kidogo cha Polisi Mtambile wilaya ya Mkoani, kwamba kuna nyumba moja eneo la Mgagadu ndio anayoitumia daktari huyo, kuendeshea shughuli hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Hassan Nassir Ali, alisema nyumba ambayo ni ya urithi ya marehemu baba yake daktari huyo, ipo eneo la Mgagadu ambapo ndipo anapoendeshea shughuli zake hizo za utoaji wa mimba kila wakati.

Alisema, baada ya jeshi la Polisi kupata taarifa hizo, walinyemelea na kisha kuivamia nyumba hiyo na kuwakamata watu watatu, akiwemo mwanamke mwenye miaka 21 alietambulika kwa jina la Sabiha Othman Iddi na Makame Haji Vuai miaka 35 wote wakaazi wa kijiji cha Gongomawe wilaya ya Chakechake.

Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa uchunguuzi wao wa haraka wamebaini kuwa, kijana Makame ambae nae alikamatwa ndani ya nyumba hiyo, ndie anaesadikiwa kumpa ujauzito mwanamke huyo na kisha kuamua kumfikisha kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya kuitoa mimba hiyo.

“Baada ya kuivamia nyumba hiyo, pamoja na kumkamata daktari huyo mstaafu, lakini pia tulimkamata mwanamme mmoja na mwanamke, ambae ndie aliekuwa katika harakati za kuata kutolewa mimba hiyo,’’alifafanua.

Aidha Kamanda huyo, alisema baadae walifanya upekuzi ndani ya nyumba hiyo, na kuvikamata vifaa mbali mbali ikiwa ni pamoja na bomba za sindano, mkasi maalum ‘mdomo wa bata’, glavs na dawa maaluma zinazoaminika za kuzuia maumivu.

“Tulishangaa kuona ile ni nyumba ya kawaida, lakini mna vifaa kama vile hospitali ya rufaa, ndio maana tumepata wasisi kwamba, yale tulioambiwa kama inatumika kutolea mimba kila dalili zipo kwa aina vifaa tulivyovikuta,’’alifafanua.

Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo, kwa sasa watuhumiwa wote hao wako mikononi mwa Polisi, wakiendelea kuhojiwa, na mara upelelezi utakapokamilika, watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Wakati huo huo, Jeshi hilo la Polisi linaendelea kumtafuta kijana Salum Marzouk wa kijiji cha Ngomani wilaya ya Mkoani, akituhumiwa kumlawiti mtoto wa miaka 13 na kumsababishia maumivu.

Aliwataka wananchi wa kijiji hicho kushirikiana vyema na Jeshi la Polisi pale watakapomuona popote mtuhumiwa huyo, kutoa taarifa ili akamatwe na kisha kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Bado Jeshi hilo la Polisi, linaendelea kumtafuta Hamdu Othman Mcha wa kijiji cha Kwazani shehia ya Wambaa wilaya ya Mkoani, alieikimbia familia yake, baada ya kudaiwa kumbaka mjukuu wake.

Mwisho