DC Wete alaani vikali ukataji wa mikarafuu

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

SERIKALI ya Wilaya ya Wete imelaani kitendo kilichofanywa na watu wasiojuikana kwa kukata mikarafuu mibichi yenye karafuu, katika shamba la mkulima Ahmada Ali lililopo Shumba Vyamboni huko Taifu Wilaya ya Wete.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Wete, Mkuu wa wilaya hiyo Kaptein Khatib Khamis Mwadini alisema kuwa, hicho ni kitendo cha uhujumu uchumi wa nchi.

Alieleza kuwa, wamegundua kuwa waliofanya hivyo ni kwa ajili ya kupata kuni kwa kuuza, jambo ambalo sio utaratibu na unarudisha nyuma maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla.

“Hivi sasa kumezuka mtindo wa baadhi ya wananchi ambao hawapendi maendeleo ya nchi hii kukata miti ya mikarafuu ilhali ikiwa na karafuu, hii sio tabia nzuri na inarudisha nyuma maendeleo yetu”, alieleza Mkuu huyo.

Kaptein Khatib alieleza, hadi sasa bado hakuna mtu aliyeshtumiwa kuhusika na hujuma hiyo ila uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na Polisi watafuatilia na atakaepatikana na hatia hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Lakini kwa sasa tutakuwa na zoezi maalum la kukamata na kuchukua kuni mbichi za mkarafuu ambazo zinakatwa bila ya kibali kinachotolewa na Idara ya misitu”, alisema Kaptein Khatib.

“Nitoe wito kwa wananchi wote wa Kisiwa cha Pemba kuwa zao la karafuu ni zao la kiuchumi, hivyo tunatakiwa tulitunze na tulithamini na mtu yeyote ambae anakwenda kinyume na taratibu za Serikali hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”, alisema mkuu huyo.

Mapema Mkuu huyo aliwataka wananchi wote ambao wanajishughulisha na ununuzi wa karafuu kwa kikombe kuacha mara moja kazi hiyo kwani Serikali itawachukulia hatua kali kwa yule atakaepatikana akifanya jambo hilo.

“Kwa sasa tutapambana nao wale ambao wanajifanya wao wana mamlaka ya kununua karafuu mbichi na hata kavu kwa wananchi wengine, kwani hawa ndio wanaofanya watu waibe karafuu za watu”, alisema Kaptein Khatib.

Hata hivyo alisema kuwa, kwa sasa Wilaya yake imeshamkamata kijana mmoja katika shehia ya Piki akinunua karafuu mbichi na kesi yake iko Mahakamani na kuwataka wananchi kushirikiana pamoja na Serikali ya Wilaya ili kupinga vitendo hivyo.

“Kwa sasa tumeshamfikisha kijana mmoja wa shehia ya Piki ambae yeye aliuziwa karafuu mbichi kutoka kwa mwanafunzi wa darasa la tatu na hivi sasa kesi yake inaendelea Mahakamani”, alifahamisha DC.

Mkuu huyo pia aliwaomba wafanyakazi wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla, ili kuhakikisha karafuu zote zinazochumwa ndani ya Wilaya hiyo au nje ya Wilaya hiyo zinauzwa katika vituo ambavyo vinatambulika Serikali na sio vyenginevyo.

Mkulima wa karafuu Ali Mussa Shehe mkaazi wa Kizimbani Wete alisema kuwa, suala la ukataji wa mikarafuu linawarudisha nyuma kimaendeleo hivyo ipo haja kwa Serikali kuweka ulinzi katika katika mashamba ya mikarafuu, ili kudhibiti wizi na uhalifu unaotendeka kwenye mashamba hayo.

“Kwa kweli wanaokata mikarafuu kwa ajili ya kuni au mbao wanatuumiza, kwa sababu zao la karafuu ndio tegemeo letu linalotupatia fedha za kujikimu na maisha.

Nae Issa Mohamed Ali mkaazi wa Piki Wete alisema ni vyema kwa kila anaekata mikarafuu na wanaonunua karafuu kwa wananchi mitaani wakachukuliwa hatua za kisheria kwa haraka, kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya wakulima wa zao hilo na Taifa kwa ujumla.

“Kwanza watoto hawaendi skuli wala chuoni wanaposikia kwamba mtaani kuna mtu ananunua karafuu, wanakwenda kwenye mashamba kuokota karafuu kwa lengo la kujipatia fedha, hivyo wanatuharibia watoto wetu”, alieleza.

Zao la karafuu ni zao ambalo linawanyanyua wananchi wa Zanzibar kiuchumi hasa kisiwani Pemba, ingawa kuna baadhi ya wahalifu hulihujumu zao hilo kwa kuikata mikarafuu na kuiba zao hilo, bila kujali nguvu za mkulima.

MWISHO.