Diwani Ngwachani akemea miradi ya maendeleo kuhusishwa kisiasa

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA           

DIWANI wa wadi ya Ngachani Jimbo la Chambani wilaya ya Mkoani Pemba Salum Makame Juma, amewataka wananchi kushirikiana vyema wanapofikiwa na miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao, na wasiipe nafasi itikadi ya kisiasa kuwagawa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi eneo la Mapape shehia ya Chambani, alisema wananchi hawana budi kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kushirikiana kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema, inawezekana serikali kuu, au mwakilishi katika jimbo ameshatekeleza wajibu wale wa kuanzisha miradi ya maendeleo, hivyo ushiriki wa kila mmoja ni jambo la lazima.

Diwani huyo alieleza kuwa, kwa mfano zinapokuwepo fedha kwa ajili ya ujenzi kama wa skuli au ukarabati wa barabara ni vyema wananchi wakaona umuhimu wa kushirikiana kwa pamoja.

“Mfano hapa kijiji cha Mapape, tunaujenzi wa skuli ya maandalizi kwa ajili ya watoto wetu, lakini ushiriki wa wananchi uko hafifu na pengine hata hili wapo wanaoliona kama jambo la kisiasa zaidi, kumbe ni la maendeleo,” alieleza.

Aidha Diwani huyo aliwataka wananchi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu viongozi wao, ili wanapotekeleza majukumu yao wapate ari na nguvu ya kutekeleza kwa nguvu.

Katika hatua nyingine, Diwani huyo wa wadi ya Ngwachani, amesifu juhudi za Mwakilishi huyo za kuwaletea maendeo wananchi wake, katika sekta za elimu, ukarabati wa barabara, usambaazaji wa maji safi na salama.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Chumbageni wadi wa Ngwachani Khamis Mohamed Nahoda, alisema kama sio mwakilishi huyo, skuli ya maandalizi ya kijiji cha Ndongoni isingemalizika ujenzi wake.

Alisema, awali ujenzi wa skuli hiyo ulikamwa kutokana na ukosefu wa fedha, ingawa baadae Mwakilishi huyo, aliamua kuchangia fedha ambazo zilisaidia na sasa kuanza kutumika.

“Wananchi wa kijiji cha Ndongoni shehia ya Chumbageni, walishirikiana vyema, baada ya mwakilishi wa Jimbo la Chambani kutoa fedha, na sasa skuli imeshaanza kutumika,’’alieleza.

Nae Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Chambani Shaibu Ali Juma, alisema kwa upande wao chama kimepata hadhi kubwa baada ya uwepo wa matawi zaidi ya saba mapya ya kisasa.

Alisema baada ya kutangaazwa kushika nafasi hiyo, Mwakilishi huyo, aliamua kuyajenga matawi ya CCM kama vile ya Kwazani, Chumbageni, Ngwachani, Dodo na Chambani na sasa yana muonekano mzuri.

“Mwakilishi wetu kwa kule wanaccm kushirikiana vyema, sasa matawi yetu yanang’ara maana alikuwa akitoa fedha taslimu na kisha wenyewe kutia nguvu kazi,’’alieleza.

Nae mwanachi Hassan Khamis Haji wa Chwale Chambani alisema, sasa watoto wao wanaondoka na kufuata elimu ya maandalizi masafa ya mbali, baada ya kumalizika kwa skuli yao.

Kwa upande wake Asha Muhsin Rashid wa Mapape alisema, kumalizika kwa ujenzi wa skuli yao, wanatarajia kuanzia mwakani skuli hiyo kutumika.

Aidha Haji Juma Haji wa kijiji cha Kwazani Wambaa, alisema hawatomsahau mwakilishi huyo, kutokana na kuifanyia matengenezo ya dharura barabara yao.

“Ilikuwa ukifika kijiji cha Wambaa, kuja kijijini kwetu Kwazani hasa siku za mvua ilikuwa ni dhiki, maana mashimo na misingi haikuruhusu kupita, lakini sasa iko vyema,’’alieleza.

Kwa upande wake Mwakilishi huyo wa Jimbo la Chambani Bahati Khamis Kombo, alisema ushirikiano aliyopewa kuanzia kwa jamii, masheha, madiwani ulimsaidia kutekeleza wajibu wake kwa upana.

Alisema, awali baada ya kutangaazwa kuliongoza Jimbo, alipata tabu moyoni na akijihakikishia kuwa hatoweza kuliongoza jimbo, ingawa baada ya kupokea ushauri wa wenzake amekamilisha kuwatumikia wananchi kwa usahihi.

Mwakilishi huyo wa Jimbo la Chambani tayari ameshajenga skuli za maandalizi Wambaa, Ndongoni, Dodo, Mapape, Kekewani, Chumbageni na Chwale pamoja na ujenzi wa matawi saba ya kisasa ya CCM.

MWISHO