Dk. Mwinyi awaahidi matamu wafanyabiashara Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira yake ni kuyafanya maisha ya kila mzanzibar kuwa mazuri ili aweze kujitegemea wenyewe kiuchumi.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wafanya biashara, mbali mbali wa kisiwani Pemba katika ukumbi wa mikutano kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi Chake chake, mkoa wa kusini Pemba.

Alisema, wananchi wa Zanzibar lazima wategemee neema tupu kutoka kwake, kwa vile dhamira yake ni kuwatumikia wananchi kwa dhati.

Alisema, mipango na mikakati yake ambayo yamo kwenye Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025, ni kuwepo kwa viwanda, na kuinua uchumi, ili umasaidie mwananchi wenye kipato kidogo.

“Zanzibara inawezekana sana kila mmoja kujitegemea na kuendesha maisha yake, maana bado hakuna viwanda vya kutosha hadi sasa, ambapo hilo nikiingia madarakani nitawaonesha njia,’’alisema.

Hivyo, amewaomba wananchi wa Zanzibar kumpa ridhaa kwa kumpigia kura hapo Oktoba 28, mwaka huu, ili aitekeleza vyema Ilani ya CCM.

Kuhusu wafanyabiashara na changamoto zao, Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliwaahidi kuwa endapo atapata ridhaa ya kuwa raisi, atashirikina na wafanya biasha wote Zanzibar, kwa kuhakikisha kuwa wanaimarisha shuguli za biashara kwa maendeleo ya nchi.

Alieleza, suala la kuwepo utitiri wa kodi analifahamu vyema, na katika kulitatu amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa, atakaa na mamlaka husika na kuweka mpangilio mzuri wa ulipaji kodi kwao.

Alisema, wataunda chombo kimoja ambacho kitakusanya kodi zote, ambazo zinatakiwa kulipa na kutakuwa na kodi rafiki kwa wafanya biashara, sio kila chombo kukusanya kodi kwa mfanyabiashara mmoja.

“Naelewa kuwa, moja jambo zito ambalo kwa sasa wafanyabiashara hapa Zanzibar ni pamoja na kuwepo kwa utitiri wa kodi, lakini nawaahidi nitalishughulikia,’’aliwaahidi.

Aidha mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa, kama akipata ridhaa, atahakikisha anaimarisha miundombinu ya barabara, ili iwe ya kisasa zaidi.

Alisema, bara bara ambazo ataanza nazo kwa kisiwani Pemba, ni ile ya Chake Chake – Wete yenye urefu wa kilomita 21, Finya- Kicha yenye urefu wa kilomita 8.8 na zile ndani ya mji wa Wete zenye urefu wa kilomita 9.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi CCM Dk. Juma Abdalla Juma Sadala,   amewashukuru sana wafanya biasha hao kisiwani Pemba kwa kufika na kuwa tayari kumsiliza mgombea uraisi huyo.

Nao wafanyabiashara hao kwa pamoja wamekubali kuchaguwa viongozi wa chama cha mapinduzi kwa kuamini kuwa watatatuliwa matatizo yao, ambayo yanawakabili katika  shughuli zao.

                             Mwisho