Hili lawezekana kuwajenga woga watoto na kudhalilishwa?

 

 Kabla ya kuisoma habari hii, jua unachopaswa kujua

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

JAMII nchini imeshauriwa kuanzisha utaratibu maalum wa kuwafanyia uchunguuzi kila baada ya muda watoto wao wa kike, ili kuwagundua ikiwa wameshafanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kisha kukaa kimnya.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mrajisi wa mahakama kuu Zanzibar kisiwani Pemba ambae ni hakimu wa mahakama ya mkoa Chake Chake, Abdull-razak Abdull-kadir Ali wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Chake Chake.

Alisema, rai moja na nzuri ili kuwagundua watoto wao kama wameshaanza kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji kama vile ubakaji, ni kuamua kuwafanyia uchunguuzi kila wakati.

Alisema kwa vile watoto wamekuwa na tabia ya kukaa kimnya mara wanapofanyiwa vitendo hivyo, aidha kwa kutishiwa na wafanyaji au kuwaogopa wazazi wao, hivyo ni vyema sasa kuwepo mpango wa kuwachuunguza.

Naibu Mrajisi huyo wa mahakama kuu, alieleza kuwa wapo watoto licha ya sheria kuwatambua kuwa bado ni watoto wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa njia ya siri, jambo ambalo wanashindwa kujishtaki kwa wazazi.

Alieleza kuwa, wengine kabla ya kufafanyiwa vitendo hivyo hutishiwa maisha na wafanyaji, hivyo njia pekee kwa wazazi kuwagundua na tabia hiyo, ni vipimo vya mara kwa mara.

“Mimi kwenye jamii, naona njia ya watoto hasa wa kike ili kuwaepushi na udhalilishaji ni kuwafanyia uchunguuzi ambao hauna wakati maalum,”alishauri.

Aliongeza kuwa hilo likifanyika, linaweza kuwapa hofu watoto wenyewe, kwani wanaweza kukumbwa na wasiwasi wa kugundulika kuwa wameshafanyiwa udhalilishaji ama laa.

Katika hatua nyingine hakim huyo wa mahakama ya Mkoa Chake Chake, alisema hata baadhi ya sheria kama vile ile ya Mtoto namba 6 ya mwaka 2011, kwa kule kumtambua mtoto kuwa ni aliyechini ya miaka 18, nalo ni tatizo.

Alisema, inawezekana yupo mtu ana miaka 17 na miezi 11 na nusu na muda saa 5:59 usiku ambapo kama akifanya tendo la ndoa kwa hiari, sheria bado inamlinda kama ni mtoto.

“Eti utaskia mwanamke ana miaka 17 na nusu, amebakwa lakini ukimuangalia hana mikwaruzo ya kubakwa wala hajaathirika popote, illa sheria inamuelewa kuwa bado mtoto, ingawa matendo ni mtu mzima,’’alifafanua.

Akizungumza hivi karibuni kwenye mkuatano wa wadau wa kupinga udhalilishaji, daktari Aboud Khamis Maabad kutoka wizara ya Afya Pemba, alieleza kuwa wakati umefika wadau wa sheria, kukindoa kifungu kinachomtambua mtoto ni mtu yeyote  aliyechini ya umri wa miaka 18.

Alisema kifungu hicho ndio cha kwanza, kinachowapa jeuri watoto kwamba wanaweza kushawishi kudhalilisha ikiwemo kubakwa na kulawitiwa, bila yao kuonekana na kosa, kutokana na kulindwa na kifungu hicho.

“Mtu anamiaka 17 na nusu, anakubali kuingiliwa na kisha anabeba mimba, ikija juu ndio anaonekana na kisha kuulizwa, bila ya sheria nayo kumshughulikia kwa kupokea mimba, hapo lazima paangaliwe,’’alifafanua.

Mtoto Haji Silima Omar wa Chake Chake alisema, sheria ya mtoto haichangii bali ukosefu wa baadhi ya mahakimu kushindwa kutoa adhabu kali kwa wabakaji, ndio kunakochangia kuongezeka kwa matendo.

Nae mtoto Warda Haji Khamis wa Machomane, alisema njia ya kuwafanyia uchunguuzi watoto ni rai nzuri, ambapo wengi wanaweza kukumbwa na woga.

Kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, alisema njia ya kuwachunguuza kila muda watoto, ubaya wake ni kuchangia kupata athari ya kisaikolojia.

Alisema kila muda mtoto kumpeleka hospitali kumfanyiwa upekuzi, anaweza kujiona kama amenyimwa haki hake, bali njia rahisi ya kuondoa udhalilishaji kwao, ni kuwaeleza uwazi juu ya athari za kufanya tendo la ndoa mapema.

“Njia ya kuwapeleka hospitali kila wakati, tunaweza kuzaa ugonjwa mwengine kwa watoto wetu wa kukosa furaha ya kuishi, bali sasa waelezwe ukweli juu ya tabia fulani,’’alishauri.

Aidha Mratibu huyo wa TAMWA kisiwani Pemba, alisema kama wazazi watawaeleza watoto waliokwisha kuwa wakubwa kimwili, juu ya athari za kukukubaliwa kuingiliwa au kuchezewa chezewa, wanaweza kupata woga na kubaki salama.

Afisa Mdhamini wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na watoto Pemba Hakim Vuai Shein, alisema njia ya kuyaondoa matendo hayo, ni jamii kuungana kwenda mahakamani kutoa ushahidi.

Mwisho