Je Dangote kuinunua klabu Arsenal mwaka 2021?

 

Hakika ni habari ambazo mashabiki wengi wa klabu ya Arsenal wanapenda kuzisikia.

Tajiri namba moja Afrika, Mnigeria Aliko Dangote anahusishwa tena na taarifa za kutaka kuinunua klabu anayoishabikia ya Arsenal.

Tofauti ni kuwa safari hii, duru zinasema kuwa jambo hilo linaweza kutokea mwaka 2021.

Dangote amenukuliwa na shirika la habari la Bloomberg akisema kuwa: ‘Ni timu ambayo ndiyo nataka kuinunua, lakini ninachosema ni kuwa (kampuni) yangu ina miradi ya dola bilioni 20 ambayo kwanza inabidi niikamilishe… labda kufikia 2021 tutaweza (kuinunua Arsenal).”

Toka Septemba 2018 bilionea Stan Kroenke ndiye mmiliki pekee wa klabu hiyo.

Mmiliki wa Arsenal Stan KroenkeHaki miliki ya pichaMEG OLIPHANT/GETTY IMAGES
Image captionMmiliki wa Arsenal Stan Kroenke anakosolewa na mashabiki wa klabu hiyo kwa kutowekeza vilivyo.

Hata hivyo, mashbiki na baadhi ya wachambuzi wa kandanda wamekuwa wakimtuhumu tajiri huyo ambaye anamiliki vilabu vya michezo mingine kama kikapu nchini Marekani kuwa haweki kipaumbele katika uwekezaji ndani ya Arsenal.

Mashabiki wamekuwa na hamu ya kuona wachezaji wenye majina makubwa wakisajiliwa, jambo ambalo bado halifanyiki.

Japo kuna ambao wanaoamini Dangote anaweza kubadili mambo, lakini hapo kabla aliwahi kuahidi kuinunua klabu hiyo lakini biashara haikufanyika.

Mwaka 2017 alitamba kuwa anatarajia wamiliki wa klabu hiyo wangeondoka mara tu baada ya yeye kuwasilisha ofa yake.

Julai 2018 akaliambia shirika la habari la Reuters kuwa: “Tutainunua Arsenal kuanzia mwaka 2020… hata kama kuna mtu mwingine atainunua, tutaendelea kuifuatilia tu.”

Je, Dangote anatofautiana vipi kifedha na matajiri wengine wa EPL

Roman Abramovich
Image captionRoman Abramovich ametumia pochi lake kubadili hadhi ya Chelsea toka alipoinunua mwaka 2003.

Kwa mashabiki wa Arsenal inawezekana ikawa si habari njema sana kwao kujua kwamba Dangote na Kroenke wanalingana kifedha.

Kwa mujibu wa jarida la mambo ya fedha na utajiri la Forbes, Dangote ana utajiri wa dola bilioni 10, huku Kroenke akiwa na dola bilioni 9.7.

Hivyo Dangote amemzidi mwenzake kwa dola milioni 300 tu.

Kinara wa kifedha katika ligi ya EPL ni mmiliki wa Chelsea bilionea wa Kirusi Roman Abramovich.

Toka tajiri huyo ainunue klabu hiyo mwaka 2003 mafanikio makubwa ikiwemo kunyanyua mataji ya EPL na hata taji la Klabu Bingwa Ulaya.

Mmiliki wa Wolves Guo Guangchang ana utajiri wa dola bilioni 7.2. (BBC)