Kamanda Awadh : kesi ipo vizuri muda wowote itapelekwa kwa DPP

Imeandikwa na Salmin Juma , Zanzibar

Jeshi la Polisi nchini limeshauriwa kuharakikisha upelelezi wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia ili haraka  zipatiwe hukumu inayostahili.

Imesemwa kufanya hivyo kutasaidia kuondosha wasiwasi kwa wadai wa kesi hizo kuwa hakuna ujanja wa mashauri yao kuingiliwa na watu wengine wanaokusudia kuharibu kesi hizo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mama wa mtoto anaedaiwa kuingiliwa kinyume na maumbile mkaazi wa Mwanakwerekwe kisiwani Ungaja  alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya maendeleo ya kesi yake ya tukio la udhalilishaji wa kijinsi dhidi ya mwanawe mwenye umri wa miaka 12 mwanafunzi wa skuli ya Kijitoupele lililoripotiwa kituo cha Polisi kijitoupele tokea 13 mwezi wa 3, 2020.

Mama huyo alisema, kesi nyengine zinatumia muda mrefu na mazingira yake hayafahamiki kiasi ambacho yanatia wasiwasi kuwa kuna namna ya kutaka kuvuruga kesi hizo.

“mfano mimi, askari walikasirika sana eti kwanini nimetia wanasheria katika kesi yangu, nikawajibu, mimi nilikua sijui nimo katika kutafuta msaada tu” alisema mama huyo.

Akiendelea kueleza alisema, tokea kutokea tukio la kudaiwa kuingiliwa kinyume na maumbile mtoto wake, anachokijua yeye kua kesi imeshafikishwa mazizini lakini hadi sasa hakuna chochote anachokijua kuhusu kesi hiyo.

“nilipokwenda kituoni kijitoupele kuuliza, ni kama wamenisusa walinipa karatasi tu ya kesi yangu, wakanambia fuatilia mwenyewe, mana askari aliyepewa kama kaiwacha, kisa nimekwenda kuripoti kwa sheha na kuingiza mwanasheria, hivyo sijui niulize wapi wala nifanye nini”alisema mama huyo.

Kwa upande wake msaidizi wa sheria na mwanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji Fatma Khamis Ali kutoka Chama wa waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA upande wa Zanzibar ambae ndie aliyeiibiwa kesi hii alisema, hata yeye anajua tu kua kesi imefika mazizini na wala haoni kuwa ni jambo baya kuingiza watu wa kumsaidia katika jambo hilo.

Alisema, kutokana na uzito wa kesi hizo ni vizuri sana askari polisi kutoa mashirikiano ya kutosha kwa wananchi kwani miongoni mwao wapo waonashindwa kutoa mashirikiano kiasi ambacho wadai wa matukio hurudi nyuma kufuatilia.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua kesi hiyo imefikia wapi na nini kinachoendelea, kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Maghrib Unguja Awadh Juma Haji alisema, kesi hiyo ipo vizuri, imefika mazizini kweli na imeshaondoka  na kumfikia yeye kwa ngazi ya kuelekwa kwa mkurugenzi wa mashtaka.

“kesi imeshaletwa kwangu na imeshakamilika kila kitu tunasubiri muda tu kuipeleka kwa DPP”

Katika kesi hii mtuhumiwa Makame Vuai Pandu mkaazi wa Mwanakwerekwe anaekisiwa kua na umri wa miaka 22 anatuhumiwa kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kike mwenye miaka 12 anaesoma skuli ya Kijitoupele.

Inadaiwa, mtuhumiwa alimchukua kwa nguvu mtoto huyo katika gari na kwenda nae huko Fuoni mambo sasa katika kichaka na kumuingilia kinyume na maumbile.