Kamati za uvuvi Chake Chake zajengewa uwezo kujiongezea kipato

 

 IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MSAIDIZI Mkurugenzi wa Kilimo, Maliasili na Mazingira wa Baraza la mji wa Chake Chake Pemba, Salum Zubeir Masiku, amesema ukulima wa chumvi, mwani na ufugaji wa samaki, usipofanywa kwa uangalifu, unaweza kuzaa janga la uharibifu wa mazingira ya habari.

Aliyaeleza hayo, alipokua akijibu hoja za wenyeviti wa kamati za uvuvi za shehia ya wilaya ya Chake Chake, kwenye mafunzo ya siku moja, ya kuimarisha uwezo wa usimamizi wa sheria na utekelezaji wa sera na kanuni  za uvuvi, yaliofanyika ofisi ya baraza la Mji Chake Chake.

Alisema kazi hizo ni sehemu ya kujiingizia kipato halali kwa mwananchi, ingawa kusipokuwa na uangalifu wa utekezaji wa sheria husika, kunaweza kukuathiri maisha ya viumbe vyengine.

Alieleza kuwa, wapo baadhi ya wakulima wa chumvi, mwani na ufugaji wa samaki, wamekuwa wakiendesha kazi hizo kwa ukataji wa mikoko na uchimbaji wa fukwe za bahari, pasi na kuzingatia sheria.

Aliongeza kuwa, anaelewa kazi hizo ni miongoni mwa kazi halali ambapo lipo kundi la wananchi limejiajiri katika eneo hilo, lakini suala la uangalifu ili kuyalinda mazingira ni jambo la msingi.

“Wapo wananchi kabla ya kuendesha kilimo cha mwani hukata miti, na wengine wanaolimwa mchumvi huchimba fukwe kama wanavyofanya wafugaji samaki, sasa lazima uangalifu wa hali ya juu uwepo,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, amewahakikishia wenyeviti hao kuwa, wataandaliwa vitambulisho maalumu, ili wavitumie wanapokuwa kazini, ili kuondoa usumbufu wanaoupata wanapotekeleza majukumu yao.

Alieleza kuwa, pamoja na kwamba wanatambulika rasmi kwenye shehia zao, lakini suala la vitambulisho wataliangalia vyema, ili wawe huru zaidi kwenye kazi zao.

Hata hivyo, amewataka wenyeviti hao kuhakikisha wanazungumza na wanajamii, ili kuona wanaendelea na utekelezaji wa sera za uhifadhi wa mazingira ya bahari kwa maslahi ya watu wote.

Mapema Afisa uvuvi wa baraza la Mji wa Chake Chake Mohamed Massoud Omar, alisema bahari ndio rasilimali kuu ya maisha ya mwanadamu wa kila siku, hivyo suala la kuilinda halina mbadala.

Alieleza kuwa, kila mmoja anawajibu huo,  kwa nguvu zake zote na akishindwa kwa pale anaposhuudia uharibifu na uchafuzi anapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo husika.

“Sheria na kanuni zetu hazituzuii kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama kama KMKM, Polisi, Mahakama na hata viongozi wetu wa shehia, chamsingi bahari ibakie salama.

Katika hatua nyingine Afisa huyo, amewataka wenyeviti hao kuendelea kutoa elimu ya kuilinda mikoko kwani athri yake haiishii katika eneo moja pekee.

Kuhusu kuwepo kwa wavuvi wenye uwelewa mdogo wa sheria na taratibu za uvuvi, pamoja na kutokuwepo kwa timu ya pamoja kuimarisha shuguli za uvuvi, alisema ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Idara yao.

Nao wenyeviti hao wa kamati za uvuvi za shehia ya wilaya ya Chakechake, walisema wanamatumaini makubwa na uamuzi wa serikali ya kufanya ugatuzi, ambao utawakomboa na taaluma ya uvuvi.

Mwenyekiti wa kamati ya wavuvi shehia ya Pujini Ali Sadriki Abdalla, alisema wakati umefika sasa kwa maafisi husika kufika shehiani, ili kukutana na wadau wa uvuvi kuhusu taaluma ya uvuaji halali.

Nae Mwneyekiti wa kamati ya uvuvi ya shehia ya Shungi Kassim Juma Kassim, alisema kazi wanayopapamba na wananchi ni ukataji wa mikoko na upigaji mkaa usiofuata taratibu.

“Hivi sasa mimi na kamati yangu, tunaendelea kupambana na wakataji wa mikoko na wale wanaopiga mkaa, maana sasa hata wageni kutoka Tanzania bara, nao wanafanyaka kazi hizi tena kwa kasi,’’alifafanua.

Mafunzo hayo ya siku moja, kwa wenyeviti wa kamati za uvuvi za shehia zilizomo wilaya ya Chakechake, ni muendelezo wa mafunzo yanayoendeshwa na Idara ya Kilimo, Maliasili na Mazingira ya Baraza la mji wa Chakechake, ili kuwajengea uwezo wenyeviti hao.

Mwisho