Kampuni QBC yaipa tano ZSSF utoaji fedha kwa wakati

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

KAMPUNI ya Quality Building contractors ‘QBC’ imesema haijawaghi kufanya kazi na taasisi yoyote hapa nchini na kisha kuingiziwa rasilimali fedha kwa wakati unaotakiwa, kama unavyofanya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ‘ZSSF’.

QBC kwa sasa inajenga ofisi mpya ya ghorofa tatu iliyopo Tibirinzi Chake Chake, kwa ajili ya watendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ‘ZSSF’ kisiwani humo, na tayari shilingi bilioni 1 zimeshatumika kati ya shilingi bilioni 7.9 zilizotengwa kwa kazi hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mhandisi ujenzi kutoka kampuni hiyo, Mohamed Hamad Shehe wakati kamati ya fedha, kilimo na biashara iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake dk: Mwinyihaji Makame Mwandini, ilipotembelea ujenzi huo na ule wa hoteli iliopo Mkoani Pemba.

Mhandisi huyo alisema, ZSSF imekuwa ndio taasisi ya kwanza kwao, kuifanyia kazi ya ujenzi na kutoa fedha kwa wakati, jambo linalowapa nguvu na ari ya kufanya kazi haraka.

Alisema walikuwa na wasi wasi wa upatikanaji wa rasilimali fedha wakati wakiendesha kazi hiyo ya ujenzi, lakini wamegundua kuwa ZSSF ni taasisi ya mwanzo kuwahi kufanya kazi nayo na kuingiziwa fedha wakati mwafaka.

“Hapa ndugu Mwenyekiti hakuna changamoto hata moja, maana jambo kubwa na la kwanza ni fedha, lakini ZSSF umekuwa ikitupa fedha kwa wakati uliopangwa, na hili ndio linatupa nguvu na ari ya kumaliza kwa wakati,’’alisema.

Alisema ujenzi wa mradi huo ulioanza mwezi Juni mwaka jana, pamoja na kuanza kwake, kuwa kulikuwa ni kipindi cha mvua, lakini unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka huu.

Mapema Mwenyekiti wa kamati ya Fedha, Kilimo na Biashara dk Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema kazi inayofanywa na ‘ZSSF’ ya uwekezaji ni chachu ya kupanua uchumi wa Zanzibar.

Alisema ZSSF kwa kushirikiana na wajumbe wao wa Bodi ya wadhamini, wamekuwa wakifanya kazi kubwa na ya maendeleo kwa kule kufanya uwekezaji endelevu kwa uchumi wa taifa.

“Mimi kwa niaba ya wajumbe wa kamati hii, niseme kuwa ZSSF endeleeni na juhudi zenu za uwekezaji, maana ni njia moja wapo ya kuutunisha mfuko mkuu wa serikali,’’alisema.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo alisema, ni vyema kwa wajenzi wa ofisi hiyo ya ghorofa tatu, kufanya kazi kwa ari na ubora, ili fedha za serikali zisipotee ovyo.

Kwa upande wake Meneja uwekezaji wa ZSSF Zanzibar Abdull-azizi Ibrahim Iddi, alisema utendaji wa kazi kwa watendaji wa Mfuko huo kisiwani Pemba, umekuwa ukipanuka ingawa eneo lao la kazi ni finyu.

Alisema ndio maana ZSSF, imeamua kuendesha ujenzi huo, ili jengo hilo linalotumika sasa kwa ofisi, liachwe kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli ambao kwa sasa unaendelea.

“Ongezeko la matumizi ya ofisi na ongezeko la wafanyakazi wetu na ufinyu iliojitokeza, ndio sasa tumamua kujenga ofisi mpya na inayotumika sasa iwe ni kwa ajili ya kuendeleza biashara ya hoteli,’’alieleza.

Nae mjumbe wa Kamati hiyo ambae ni Mwakilishi wa Jimbo la Mtambile Mohamed Mgaza Jecha, aliipongeza ZSSF kwa hatua yake ya kuibadili Pemba kimajengo na uwekezaji.

Wakati huo huo Kamati hiyo ya Fedha, Biashara na Kilimo ilitembelea sehemu ya ujenzi na matengenezo makubwa yanayoendelea kweye jengo la hoteli ya Mkoani Pemba kwa sasa iliochini ya ZSSF.

Ambapo wakiwa kwenye eneo hilo, Meneja uwekezaji wa ZSSF Abdull-aziz Ibrahim Iddi, alisema baada ya hoteli hiyo kukaa kwa muda wa miaka 12 bila ya kutumika, serikali iliikabidhi ZSSF kwa ajili ya kuiendesha.

Alisema kuwa, baada ya kukabidhiwa jengo hilo Oktoba 19, mwaka 2018, walianza harakati za kumtafuta mshauri, na ujenzi ulianza kwa kufuata taratibu zote za manunuzi.

Alieleza kuwa, hatimae kampuni ya ‘ARQES AFRICA’ ya Jijini Dar-es Salaam iliibuka msindi na kuanza kazi ya kulikagua jengo hilo na kutoa mapendekezo na michoro mipya kulingana na jengo na mahitaji.

Aidha Meneja huyo Uwekezajia alifafanua kuwa, baada ya taratibu za kimanunuzi kumalizika kampuni ya ‘BENCHMARK’ ya Tanzania bara, nayo iliibuka mshindi wa kulikarabati jengo hilo na kuongeza ghorofa mbili zaidi.

“Ukarabati wa jengo hilo ambalo lilikuwa la ghorofa moja, umehusisha kuongezwa kwa ghorofa mbili na sasa kuwa na idadi ya vyumba 18 ya kulala wageni, badala ya vile vinane vya awali,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Meneja huyo uwekezaji, alieongeza kuwa, baada ya kumalizika kwake mwishoni mwa mwezi huu wa Machi mwaka 2020, kunatarajiwa kuzaliwa ajira za kudumu zaidi ya 50 kwa wananchi mbali mbali.\

Nae Mkadiriaji majengo kutoka kampuni ya ‘BENCHMARK’ Khamis Rashid Khalfan, alisema ujenzi huo ambao kwa sasa umeshafikia asilimia 85, utakuwa wa kisasa na kuung’arisha mji wa Mkoani.

Alisema kazi hiyo wanaendelea kuifanya kwa ufanisi mkubwa hasa kwa vile hakuna changamoto ya upatikanaji wa fedha, jambo linalowatia nguvu katika kazi hiyo.

Alisema wamekuwa makini wanapopata kazi kama hizo, wakiamini kuwa ujenzi bora, imara na unaomalizika kwa wakati ndio hadhi na ubora wa kampuni yao.

Ujenzi na ukarabati mkubwa wa jengo ambao ulianza Julai 4 mwaka jana, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2020.

Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ZSSF umekuwa ukutumia fedha za wanachama wa mfuko kwa ajili ya uwekezaji, katika miradi yenye tija, ili baadae waweze kuzirejesha na wanachama wakabidhiwe wanapo stafaafu.

ZSSF ambao umeanzishwa kwa sheria no 2 ya mwaka 1998 na kufanyiwa marekebisho kadhaa na kuanzishwa upya kwa sheria no 2 ya mwaka 2005 baada ya mapitio makubwa.

Mwisho