Kesi ya mwanamke Pujini aliemtafuna mwenzake mdomo yaahirishwa

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

UPANDE wa mashtaka katika mahkama ya Mwanzo wilaya ya Chake Chake, umelazika kulihairisha tena, shitaka linalomkabili mtuhumiwa Mkasi Makame Juma wa Pujini, anaedaiwa kumtafuna mwanamke mwenzake mdomo na shavu, kutokana na kutopokea mashahidi.

Mwendesha mashtaka mahakamani hapo kutoka Jeshi la Polisi sajenti Juma Habibu, alidai kuwa, shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikiliza mashahidi, ingawa hawajawapokea.

Alidai kuwa, lakini pia shauri hilo ni vyema likapangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza mashahidi hao, kutokana na mwendesha mashtaka husika, kutokuwepo mahakamani.

“Mheshimiwa hakim, shauri lililopo mbele yetu, ni kwa ajili ya kusikilizwa, lakini kwanza hatujapokea mashahidi na vyenginevyo, mwendesha mashtaka husika anadharura,’’alidai.

 

Mara baada ya maelezo ya mwendesha mashtaka huyo, hakim wa mahakama hiyo ya mwanzo Hashim Kassim, alimuuliza mtuhumiwa ikiwa ana hoja yoyote.

“Kwanza mtuhumiwa umeyasikia maelezo kutoka upande wa mashitaka, kwamba hawajapokea mashahidi na muhusika wa shauri hili ambae ni mwandesha mashtaka hakufika mahakamani, unasemaje,’’alimuuliza.

Mtuhumiwa huyo Mkasi Makame Juma miaka 22 wa Pujini, alimjibu hakimu huyo kuwa, hana pingamizi na maelezo hayo yaliotolewa mahakamani hapo.

Hivyo, hakimu huyo alimtaka mtuhumiwa huyo kurudi nyumbani na kuwasili mahakamani hapo tena Febuari 3, mwaka huu kuendelea na shauri lake.

Awali ilidawa kuwa, mtuhumiwa huyo alimshambulia Fatma Ali Hamad kwa kumtafuna mdomo na sehemu ya shavu lake la upande wa kulia.

Ambapo hali hiyo, ilidaiwa kuwa, ilimsababishia maumivu mkali muathirika, ambapo hilo ni kosa kinyume na kifungu cha 230 cha sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar iliopitishwa na baraza la wawakilishi.

Tukio hilo la shambulio la kuumiza mwili, lilidaiwa kutokea majira ya saa 3:00 asubuhi eneo la Pujini wilaya ya Chake Chake Mkoa wa kusini Pemba, Januari 9 mwaka jana.

Wakati huo huo mahakama hiyo, imehairisha hatua ya utetezi kwa mtuhumiwa Mohamed Rashid Abdalla anaedaiwa kuiba kuku wawili wenye thamani ya shilingi 30,000 kutokana na kutokuwepo kwa mwendesha mashtaka husika.

Aidha kesi hiyo ambayo ni ya tuhuma ya wizi wa mali ya Rashid Ali imehairishwa na mahkama hiyo, kutokana na hakimu husika kutokuwepo mahakama hapo kikazi.

Awali ilidaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo aliiba kuku hao ambao mmoja ni dume na jike wenye rangi mchanganyiko, tukio lililotokea April 4, mwaka jana majira ya saa 7:15 mchana kijiji cha Ditia Wawi.

Ambapo ilidaiwa kuwa, kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 258 na 268 (1), (2) na (3) sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Ambapo kesi hiyo, sasa itarudi tena mahakama husika Januari 30, mwaka huu na mtuhumiwa amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutumiza masharti ya dhamana.

Mwisho