Kijana wa miaka 29 mikononi mwa Polisi Pemba kwa tuhuma za ubakaji

Imeandikwa na Salmin Juma – Pemba

Hatimae kijana Ali Khamis Ali ( 29) mkaazi wa Vitongoji Chake Chake anashikiliwa na Jeshi la polisi kusini Pemba kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka 14 na kumsababishia ujauzito.

Tukio hilo linadaiwa kutokea mwezi wa Septemba mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku huko Vitongoji Chake Chake Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madungu  Kamanda wa polisi mkoa wa kusini Pemba Hassan Nassir Ali alisema  mtoto huyo alifanyiwa kitendo cha ubakaji mwezi Septemba mwaka huu, ingawa hakujulikana mpaka alipogundulika kuwa ana ujauzito.

“Mtoto huyo alibakwa kipindi cha nyuma lakini mwezi huu ndo amegundulika kuwa ni mjamzito, hivyo Jeshi letu linashughulikia tuhuma hizi, zilizotolewa dhidi ya kijana Ali Khamis Ali” alisema Kamanda huyo.

Alieleza kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa huo linaendelea na upelelezi wa tuhuma hizo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Aliwataka wanajamii kuwa na ushirikiano katika kupambana na kesi za udhalilishaji kwa watoto, kwa kwenda mahakamani kutowa ushahidi pindi wanapotakiwa, ili kuondosha kabisa vitendo hivyo.

“Matukio ya udhalilishaji kwa watoto yanaendelea siku hadi siku, hivyo tushirikiane pamoja kuhakikisha tunadhibiti vitendo hivyo na wahalifu waogope”, alisema.