Kijana wa Mtambile Pemba atupwa rumande kwa tuhma za ubakaji

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

KIJANA Salum Hafidh Mohamed miaka 18 wa Mtambile wilaya ya Mkoani Pemba, ametupwa rumande hadi wiki mbili zijanzo, na Mahakama ya Mkoa ‘B’ Chake Chake, akikabiliwa na tuhuma za ubakaji wa mtoto wa miaka 15.

Akiwa mahakamani hapo chini ya Hakimu Luciano Makoye Nyengo, mtuhumiwa huyo baada ya kusomewa tuhuma zake na Mwendesha Mashtaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Seif Mohamed Khamis, alitamkiwa na Hakim huyo huyo kosa lake la ubakaji halina dhamana.

Awali Mwendesha Mashtaka huyo alidaia kuwa, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na makosa matatu kwa mtoto huyo, ambapo aliyafanya kwa nyakati tofauti.

Kosa la kwanza kwa mtuhumiwa huyo ni la ubakaji, ambalo alilifanya Juni 22, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku eneo la Kwa masharifu Mtambile, ambapo alimbaka mtoto huyo mwenye miaka 15.

Aidha mtuhumiwa huyo huyo, anadaiwa kumbaka mto huyo huyo tarehe hiyo majira ya saa 8:30 usiku na kisha kumbaka tena majira ya saa 11:00 alfajiri, eneo hilo hilo la Kwa masharifu Mtambile wilaya ya Mkoani.

Ambapo kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Mara baada ya maelezo hayo, mtuhumiwa huyo alinyoosha mkono wake juu, kuashiria kutaka kusema jambo, na Hakimu Luciano Makoye Nyengo alimruhusu.

“Mheshimiwa Hakimu naiomba mahakama yako tukufu kunipatia dhamana juu ya kosa hili, ambalo natuhumiwa nalo,’’alidai mtuhumiwa huyo.

Hakimu huyo alimtaka mtuhumiwa huyo kwenda rumande hadi Machi 30 mwaka huu, na kumueleza kuwa mahakama yake haina uwezo wa kutoa dhamana, huku akiutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mahidi siku hiyo.

Mwisho