KMKM Pemba chakamata vipolo 15 vya makonyo yaliotaka kusafirishwa magendo

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

KIKOSI Maalum cha Kuzia Magendo ‘KMKM’ kamandi ya Pemba, kimekamata vipolo 10 vya makonyo makavu ya karafuu, vyenye ujazo wastan wa kilo 1, 500 yaliodhaniwa kuwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa nje ya Pemba kwa njia ya magendo.

Akitoa taarifa mbele ya uongozi wa Mkoa wa kaskazini Pemba, Mkuu wa operesheni KMKM kamandi ya Pemba ‘LCDR’ Bakari Salum Othman, alisema makonyo hayo, waliyakamata eneo la Msuka wilaya ya Micheweni.

Alisema waliyakamata eneo la bandari bubu inayoitwa Mpapindi majira ya saa 7:00 usiku, karibu na msitu wa hifadhi wa Ngezi, yakiwa kwenye vichaka.

Alieleza kuwa, wapiganaji wake, waliopo kambi ya Msuka walifika katika eneo hilo, kwa kutumia usafiri wa kawaida na kisha kuamua kujificha iwapo engetokezea mwenyewe.

“Baada ya kuyakuta wakati huo wa saa 7:07 usiku sisi tulijificha masafa kidogo, ili kumsubiri mmiliki, ingawa hadi majira ya saa 10:00 alfajiri hakutokea muhusika na kuamua kuondoka nayo na kuyakabidhi serikali ya mkoa,’’alieleza.

Hivyo alifafanua kua, kwa vovyote vile kwa eneo walioyakuta kwa vile sio mbali na bandari bubu, uwezekano wa kutaka kusafirishwa kimagendo ni mkubwa zaidi.

Ameendelea kuwasisitiza wananchi wasiotakia mema nchini kwa kujiajiri kwenye magendo, kuwa walinzi wa magendo hawalali na wamekuwa wakifanya doria katika kila pembe ya kisiwa cha Pemba.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Omar Khamis Othaman, alisema bado wanakosa usingizi kutokana na uwepo wa bandari bubu zaidi ya 100 ndani ya mkoa, ambazo hutumiwa na wajanja kuipotezea mapato serikali.

Alisema kwa wilaya ya Wete pekee zipo zaidi ya 70 idadi inayolingani na wilaya ya Micheweni, ambapo wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha hazitumiki vibaya ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi katika maeneo hayo.

“Mimi niwapongeze sana wenzetu wa KMKM kwa kuwa waadilifu kwa kukamata bidhaa ya magendo na kuamua kuyafikisha serikalini na hasa mali ghafi inayotokana na zao la taifa la karafuu,’’alieleza.

Alieleza kuwa, sasa bidhaa ya makonyo imekuwa na thamani kuanzia ndani na nje ya nchi, ndio maana wasioitakia mema nchi, wamekuwa wakiyatorosha nchini.

Alikitaka kikosi hicho cha KMKM kuendelea kuwa makini kwenye maeneo yao na maeneo mengine, ambayo wasafirishaji magendo wamekuwa yakitumia hasa kipindi hichi cha sherehe.

“Inawezekana wapo wanaotumia kipindi hichi cha sherehe za hapa na pale na wao kujaribu kupita na bidhaa za magendo, sasa lazima muendelee na umakini wenu kwenye kazi,’’alifafanua.

Akizungumzia kuhusu uvunaji wa zao la karafuu ndani ya mkoa wake, alisema maeneo kama ya Konde na vijiji jirani na wilaya ya Chakechake ndimo ambamo zao hilo limezaa kwa wingi.

Baadhi ya wananchi wa Wete, waliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kupandisha bei za lao makonyo kutoka shilingi 1,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi 2,000.

Ali Khamis Muumini na Haji Kali Nahoda walisema, inawezekana tamaa ya wafanyabiashara kwamba, kwa vile baadhi ya maeneo ya Mombasa nchini Kenya, bei iko juu ndio wamekuwa wakishawishika na hilo.

“Bei iongezwe kama ilivyofanywa kwenye karafuu, pengine hiyo tabia ya kuyavuusha kimagendo inaweza kuondoka, maana inawezekana hao wanaofanya hivyo, wanafuata bei kubwa,’’alisema Ali Khamis.

Vipolo hivyo 10 vya makonyo ya karafuu yaliokamatwa na KMKM vina ujazo wa kilo 1,500 ambapo vina thamani wastani wa shilingi milioni 2.2 kwa bei ya kilo moja shilingi 1,500.

Mwisho