Leo ni siku ya unawaji mikono duniani, kitaifa Zanzibar kuadhimishwa Pemba

 

LEO tarehe 15, Oktoba, ni siku ya kimataifa ya unawaji mikono duniani kote, ambapo kitaifa kwa Zanzibar sherehe hizo zinaadhimishwa kisiwani Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman wakati akizungumza na waandishi wa habari ukumbi wa ZBC Chake Chake, alisema dunia inaadhimisha siku hiyo maalum kutokana na kuwashajihisha wananchi kuwa na utamaduni wa kunawa mikono.

Alisema yapo maradhi kadhaa kama vile matumbo ya kuharisha, vikope, nimonia na mengine yamekuwa yakisababishwa na kula chakula bila ya mtu husika kutonawa.

Naibu waziri huyo, alisema utamaduni wa kunawa mikono ndio maagizo ya wataalamu wa Afya, hivyo lazima kila mmoja atekeleze hilo bila ya shuruti.

Maadhimisho ya siku na kunawa mikono kitaifa kwa Zanzibar ambayo yanafanyika kisiwani Pemba ukumbi wa Samail Gombani Chake Chake, ambapo mgeni rasmi akitarajiwa Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed.

Kabla ya Waziri huyo anayetarajiwa kuwa mgeni kuwahutubia wananchi, atapokea maandamano ya wahudumu wa afya na wananchi wengine yanayotarajiwa kuanza eneo la Mkoroshoni ZBC hadi ukumbini hapo.

Ujumbe wa mwaka huu kitaifa ‘osha mikono okoa maisha ‘ ambapo wa kikanda kwa Zanzibar ‘usafi wa mikono kwa wote’.