Mabwana harusi sasa kulipa kodi badala ya mahari

 

Ni takribani miezi minne sasa hakuna ndoa iliyofungwa katika kijiji kimoja la jimbo la Kano, nchini Nigeria tangu chifu wa eneo hilo kuanzisha malipo ya kodi ya harusi.

Ado Sa’id, ambaye ni chifu wa kijiji cha Kera kaskazini magharbi mwa Nigeria, amewataka mabwana harusi kulipa kodi ya kiasi cha dola 377.

Hii ikiwa ni mbadala wa utamaduni ambao uliopo wa kulipa samani, vyombo vya jikoni na vitu vingine vya thamani kwa ajili ya kutoa kwa familia ya bibi harusi watakapofunga ndoa.

Kiongozi huyu amesema kuwa kulipa kodi ni rahisi zaidi kuliko kulipa mahari na itawafanya watu wengi kufunga ndoa kirahisi.

Wanamuziki wa jimbo la Kera
Image captionWanamuziki wa jimbo la Kera

Alisema utekelezaji utaanza baada ya kushauriana na wanakijij, jambo amalo lilipingwa vikali.

Wanakijiji wanahisi kuwa utaratibu uliokuepo zamani ulikuwa mzuri na walikuwa wanaweza kununua zawadi wanavyotaka.

Mwanakijiji mmoja , Isah Kera, anasema kuwa sheria mpya inawalazimisha wapenzi kwenda kufunga ndoa sehemu nyingine ili kukwepa kodi hiyo.

Mwanakijiji mwingine, Sani Kera anasema kuwa ana watoto watano ambao wako tayari kuoa ,lakini mipango yao imebidi ihairishwe.

Unaweza pia Kusoma kuhusu harusi:

Wakati Nigeria wanalalamikia kodi kwenye harusi, vijana wa mataifa ya Afrika mashariki wamekuwa wanalalamikia gharama ya mahari inayotolewa katika jamii mbalimbali.

Presentational grey line

Je ni kweli gharama ya juu ya mahari inawazuia vijana kufunga ndoa Afrika Mashariki?

Tanzania:

Tanzania, ni nchi nyingine inayotajwa kushuhudia viwango vikubwa vya mahari katika baadhi ya jamii.

Huenda ndio moja ya sababu inayowafanya baadhi ya vijana kutooa kwa njia rasmi.

Vigezo ni vingi vinavyobaini kiwango cha mahari atkachotozwa kijana, mfano katika baadhi ya jamii – weupe wa msichana humaanisha mahari zaidi, lakini pia kiwango cha elimu cha msichana anyechumbiwa.

Kwa kukadiria kijana huitishwa ng’ombe au pesa zenye thamani ya kati ya shilingi milioni 5 hadi milioni 20 za Tanzania.

Uganda:

Utamaduni huu ni wa kawaida nchini Uganda, zaidi kwa jamii zilizopo katika maeneo ya mashinani, lakini pia hutolewa katika maeneo ya mijini.

Mahari nchini humu hufuata msingi ambao umekuwepo – kutoa kitu ili upewe mke.

Lakini sasa kuna mtindo kwa baadhi ya familia kuandikishana mikataba na bwana harusi kama ithibati ya kulipa mahari anayoitishwa.

Inaaminika kuwa iwapo mke amemtoroka mumewe baada ya kuteta na akarudi kwao, familia yake haina budi ila kurudisha mahari yote aliyolipiwa.

Mnamo 2010 mahakama nchini humo iliamua kuwa utoaji mahari ni halali, lakini majaji walipiga marufuku mtindo huo wa kurudishwa mahari wakati ndoa inapovunjika.

Kenya:

Katiba nchini Kenya haishurutishi ulipaji wa mahari, lakini ni jambo linalofahamika kuwa mahari hulipwa katika jamii tofuati nchini.

Baadhi ya jamii kwa mfano kwa wafugaji husisitiza mahari ya mifugo, huku kwa jamii nyingine mali, pesa taslimu na hata madini hupokewa kama mahari.

Huwepo hisia kwamba kuna malipo aliyotolewa mke kwenda kwa mume.Presentational grey line

Mahari ni nini?

Utamaduni wa kutoa mahari upo katika nchi nyingi ulimwenguni zikiwemo barani Asia, mashariki ya kati sehemu kadhaa za Afrika na pia katika baadhi ya visiwa vya pasifiki.

Kiwango kinachotolewa hutofautiana kuanzia zawadi ndogo tu za kuendeleza utamaduni huo hadi maelfu ya dola za Marekani kwa mfano kama inavyoshuhudiwa katika ndoa za baadhi ya jamii.

Tangu jadi, utoaji mahari umekuwa ni utamaduni unaoheshimiwa na kuenziwa pakubwa hata miongoni mwa jamii za watu waliosoma na kuishi maisha ya kisasa.

Kwa kawaida mahari huwa ni kama mkataba wa makubaliano kabla ya ndoa ambapo mali kama ng’ombe, ngamia, mbuzi au hata pesa taslimu hulipwa na bwana harusi kwa familia ya bibi harusi ili apewe mke.

Iwapo mume hatotimiza mahari iliyokubaliwa kwa muda uliotolewa, kuna jamii ambao humrudisha mke nyumbani mpaka mume akamilishe kulipa mahari. (BBC)