Magufuli amuombea kura Dk. Mwinyi kwa njia ya simu Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Dk. John Pombe Magufuli, amewaomba wananchi kisiwani Pemba, kumpa kura Mgombea urais wa Zanzibra kupitia chama hicho, Dk. Hussein Ali Mwinyi ili ashirikiane nae kwa kuzitatua changamoto zao, ikiwemo ajira kwa vijana.

Alisema kuwa, watahakikisha wananasimamia na kuyatekeleza yale yote yaliyomo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2020/2025 kwa kutatua changamoto zote zinazowakabili wanachi wa kisiwani Pemba.

Akizungumza na wananchi hao kwa njia ya simu ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaaliwa Kassim Majaaliwa aliyekuwepo kwenye mkutano, uliofanyika shehia ya Mchanga mdogo Jimbo la Kojani wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wa kumnadi mgombea urais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.

“Kwa kushirikiana na Dk. Hussein Ali Mwinyi tutahakikisha tunazitatua changamoto mbali mbali za wananchi kwa ajili ya kuleta maendeleo zaidi, hivyo mchaguweni Dk. Mwinyi”, alisema.

Alisema Dk. Mwinyi anatosha mno kuwa rais wa Zanzibar hivyo hakuna jana kwa wananchi wa Pemba, kupoteza kura zao.

Alisema, CCM imemteua Dk. Mwinyi baada ya kumuona anafaa kuwa kiongozi kutokana na uchapakazi wake, uaminifu na kuwajali watu wa makundi wote.

“Ndugu zangu wa Pemba mimi nitakuja huko baada ya uchaguzi mkuu, lakini kwanza namleta kwenu Dk. Mwinyi na mumchague anafaa sana sana,’’alisema.

Katika hatua nyingine Mgombea huyo wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akizungumza kwa simu wakati akiwa Ikulu, alisema Zanzibar inahitaji pia kiongozi anaeupenda na kuenzi Muungano.

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli aliwaomba wananchi hao na wanaccm kumchagua yeye ili awe rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ashirikiane na Dk. Mwinyi katika kuwatumikia wananchi wote.

Akimuombea kura Dk, Magufuli,  mjumbe wa Kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM Taifa, Majaliwa Kassim Majaliwa alisema, kiongozi huyo ni mchapakazi, mwaminifu, mwadilifu na msimamizi mzuri.

Alisema hivyo ipo haja kwa wananchi kumchagua tena, ili kuendeleza yale ambayo yamebakisha katika miaka yake mitano ya mwanzo.

Majaliwa alisema, taifa lina hitaji kiongozi mchapakazi ambae atawaletea wananchi maendeleo wote bila ya ubaguzi kama Dk, Magufuli.

Nae Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema, dhamira ya kugombea urais ni kuwatumikia wazanzibari hususani wanyonge pasi na ubaguzi wa aina yoyote.

“Katika kampeni zangu ambazo nimepita kwa wananchi nimekutana na wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo, wakulima wa mwani, wavuvi, mamalishe nia yangu ni kuwasaidia, ili kuona wanajikuza kiuchumi,” alisema.

Aidha Dk. Mwinyi amesisitiza suala la amani na kusema kwamba shughuli ambazo zinafanywa na wananchi haziwezi kutekelezeka bila ya amani na utulivu huku akiwataka wananchi kuingia katika uchaguzi kwa usalama ifikapo Oktoba 28.

Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Sadala (Mabodi) alisema, sera ya chama hicho ni kushinda hivyo lazima kila mwanaccm hilo alijue ili kuhakikisha kura yake haipotezi.

“Tunaviomba vyama vyengine vyote na hata wale ambao hawana vyama lakini wanapiga kura, watupe ridha aili kuendeleza maendeleo kama ilivyo ada,’’alieleza.

Mapema Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema, Chama hicho siku zote kimekua kikifanya kampeni zake za kistarabu, ili amani iliyopo ndani ya nchi iendelee kudumu.

Alieleza kuwa, mara hii Kisiwani Pemba ushindi utakua ni wa mfano, na kuhakikishia wananchi kuwa, ulinzi utakuwepo wa kutosha siku ya Uchaguzi.

“Mwende mukapige kura mapema ifikapo Oktoba 28 kwani 27 ni siku ya vikosi maalumu ambavyo vitakuja kuwalinda siku yenu ya kupiga kura,” alisema.

 

 

MWISHO