Mahakama Chake Chake: ‘PWISO’ wasilisha watetezi wako Aprili 2′

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa ‘B’ Chake Chake, imempa muda hadi April 2 mwaka huu, mtuhumiwa wa kuvunja nyumba Mohamed Ali Abdalla ‘PWISO’ wa Mtambile wilaya ya Mkoani kuwasilisha mashahidi wake wa utetezi, baada ya mahakama hiyo kuona ana kesi ya kujibu.

Kauli hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, mara baada ya mtuhumiwa huyo kuwasili mahakamani hapo, akisubiri taratibu nyingine za kimahakama.

Awali Mwendesha mashtaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Seif Mohamed Khamis, aliiambia mahakama hiyo kuwa, shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikiliza utetezi.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa, baada ya upande wao kufunga ushahidi huo wiki mbili zilizopita, sasa ni zamu ya mtuhumiwa kufanya utetezi wake juu ya shauri hilo.

“Mheshimiwa Hakimu shauri hili ambalo leo ‘jana’ lipo mbele yako ni kwa ajili kumsikiliza mtuhumiwa kutoa utetezi wake leo hii mbele ya mahakama yako tukufu,’’alidai Mwendesha mashtaka huyo.

Ndipo Hakimu wa mahakama hiyo, alipompa nafasi mtuhumiwa huyo kuanza kutoa utetezi wake dhidi ya tuhuma zinazomkabili, na hasa baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

“Mtuhumiwa ni nafasi yako sasa kutoa utetezi wako mbele ya mahakama hii, iwe ni kwa njia ya kiapo bila au bila ya kiapo vyote inakubalika,’’alisema Hakimu huyo.

Ndipo mtuhumiwa huyo alipoieleza mahakama hiyo kwamba ni vyema akaahirisha utetetzi wake kutokana na shahidi wake mmoja kuumwa na kulazwa hospitali.

Alidai kuwa, alitarajia engewasili mahakamani hapo akiwa na shahidi wake huyo, ingawa kutokana na matatizo ya kuumwa haikuwezekana na kuiomba Mahakama impangie tarehe nyingine.

“Ni kweli Mheshimiwa Hakimu nilitarajia siku ya leo ‘jana’ kuwa nianze kujitetea huku nikiwa na shahidi wangu kwapani, lakini amekutwa na maradhi, ndio maana hakufika,’’alidai.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Luciano aliuuliza upande wa mashitaka kama wana jambo lolote, kutokana na maelezo ya mtuhumiwa huyo, ambapo haukuwa na ziada.

Ndipo Hakimu huyo alipomtaka mtuhumiwa huyo kurudi nyumbani, na kufika mahakamani hapo tena Aprili 2 mwaka huu, akiwa na shahidi wake wa utetezi.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, tukio hilo la kuvunja nyumba lililotokea Julai 8, mwaka jana majira ya saa 3:00 asubuhi eneo la Gae la Mtungi Mtambile wilaya ya Mkoani.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo, isivyo halali alivunja na kuingia ndani ya nyumba ya kuishi ya Issa Nassor Issa kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi, jambo ambalo ni kosa kinyume na kifungu cha 258 sheria ya Adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

                                                                                 Mwisho