Mahakama kuu yampadhamana Babu ‘aliyembaka mjukuu wake’ Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSO, PEMBA

BAADA ya mahkama kuu ya Zanzibar Januari 7 mwaka huu kumpa dhamana aliyekuwa ‘boss’ wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar ‘ZSTC’ wilaya ya Mkoani, anaetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita, hatimae mahakama hiyo tena, imempa dhamana mzee Ridhiwani Juma Khamis wa Wawi Chake Chake, anayekabiliwa na tuhma za kumbaka mjukuu wake.

Mahakama kuu chini ya Jaji Mkusa Isack Sepetu, baada ya kupokea ombi la dhamana la mshitakiwa huyo, ililipitia na kisha baada ya kujiridhisha sababu zilizomo, juzi Januri 31, mwaka huu imemtoa rumande na kumuweka maisha ya uraini mzee huyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mrajisi wa mahkama kuu Pemba na hakimu wa mahkama ya mkoa ‘A’ Chake Chake Abdull-razaki Abdull-kadir Ali, alisema mahkma kuu ilishawishika kumpa dhamana mshitakiwa huyo, kwa sababu mbili kuu.

Alisema moja ni kutokana na kuwa na umri mkubwa wa miaka 60, ambapo kumuweka kwenye mazingira hayo kunaweza kukazaliwa jambo jengine pamoja na sababu ya pili ya dhana kutokuwa na kosa hadi mahakama imtie hatiani.

“Hii sababu ya umri iko wazi, lakini nyingine bado yule ni mtuhumiwa na hadi sasa mahakama iko kwenye dhana, hivyo sababu hizo, ndio ambazo zilipelekea kupatiwa dhamana mshitakiwa huyo,’’alisema.

Aidha Mrajisi huyo alisema, pamoja na ombi lake la dhamana kutolewa uamuzi huo, lakini alipewa masharti kadhaa mtuhumiwa huyo, ambayo yote aliyatimiza na kupelekea kupewa dhamana.

Miongoni mwa masharti aliyowekewa na kuyatimiza, ni pamoja na kukubali kuandikisha shilingi milioni 3, kutosafiri nje ya kisiwa cha Pemba pasi na kibali cha mahakama husika.

Masharti mengine aliowekewa mshitakiwa huyo na kuyatimiza, ni kuwa na wadhamini watatu, ambao wote wataandikisha shilingi milioni 2 kila mmoja pia wawe na vitambulisho vinavyotambulika na barua za sheha wa shehia wanapoishi.

“Ni kweli mshitakiwa yule wa Wawi anaedaiwa kumbaka mjukuu wake, leo ‘jana Januari 31 mwaka huu, amepewa dhamana na mahakama kuu, na tumeshaisoma kwenye mahakama ya Mkoa ‘A’ Chakec Chake na sasa yuko uraiani,’’alieleza.

Hata hivyo alisema, jamii isiitafsiri vibaya mahakama kuwa, wanaopewa dhamana ni watu wenye hadhi fulani, bali ni haki ya kila mmoja kuomba dhamana na mahkama ikijiridhisha anaweza kupewa.

Hii ni kesi ya pili, kwa mujibu wa sheria ambazo hazina dhamana, na kisha kwa mujibu wa sheria Mahkama kuu ya Zanzibar kutoa dhamana, ambapo ya mwanzo ni ile ya Januari 7, mwaka huu ya mtuhumiwa Seif Suleiman Kassim, ambapo kesi hii itarudi tena mahakamani Febuari 24 mwaka huu, huku ya mzee Ridhiwan ikirudi tena Febuari 5 mwaka huu.

Awali mtuhumiwa huyo akiwa ndani ya mahakama ya mkoa ‘A’ Chake Chake chini ya Hakimu Abdull-razak Abdull-kadir Ali na Mwendesha Mashtaka kutoka afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mohamed Ali Juma alidai kuwa, mshitakiwa huyo akijua kua ni kosa, alimbaka mjukuu wake.

Tukio hilo lilitokea katika tarehe isiofahamika mwezi Machi mwaka jana, majira ya saa 7:00 mchana Wawi wilaya ya Chakechake Pemba.

Ilidaiwa kuwa, siku hiyo alimuingilia mjukuu wake, jambo ambalo ni kosa kisheria, kinyume na kifungu cha 143 (1), (4) cha sheria ya Adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Kifungu hicho cha (4) kinaeleza kuwa, “iwapo itadaiwa kwenye taarifa au shtaka na ikithibitika kuwa, mtu mwanamke ana umri chini ya miaka 18, mkosaji mwanamme atapewa adhabu ya kifungo cha maisha ”

Ambapo kifungu cha (6) cha sheria hiyo hiyo, kinaeleza kuwa ‘iwapo mtu mwanamme anajaribu kutenda kosa lolote kati ya yaliotajwa, atakuwa ni mkosa, na atapewa adhabu ya kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka 10’

Taarifa za kihalifu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonesha kuwa, kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2017, kulikuwa na jumla ya watu 159 waliofanyiwa matendo ya kuingiliwa na maharimu wao, ambapo wanaume ni 141 walioripotiwa na wanawake walikuwa 18.

Mikoa ya kipolisi iliongoza ni Temeke 86, Singida 47, Dododma 7, Simiyu 5, Shinyanga 4,  Kagera 3, Tabora na Mara wawili wawili, wakati mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, na Mtwara kulikuwa na watu mmoja mmoja huku mikoa mitano ya Zanzibar hakukua na matukio ya aina hiyo kwa mwaka huo.

Mwisho