Mahakama Pemba yawakaribisha wananchi Febuari 11 Tenis Chake Chake

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa kujitokeza kwa wingi, kwenye siku ya sheria Zanzibar ‘law day’ ili kujifunza na kupata ufumbuzi wa masuala ya kisheria, kwenye hafla inayotarajiwa kufanyika uwanja wa Tenis Chake Chake Febuari 11, mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwenye jengo la mahakama kuu Chake Chake, Hakimu Dhamana wa makahama  Mkoa kaskazini Pemba Abdalla Yahya Shamuuni, alisema siku hiyo pia huwa ni nafasi kwa wananchi nao kupata uwelewa.

Alisema, siku ya sheria hapa Zanzibar imewekwa pamoja na mambo mengine kuhakikisha wananchi wa Zanzibar, ambao wadau wakuu wa mahakama, wanaona kazi na changamoto za utendaji unaowakabili watendaji.

Hakimu huyo dhamana, alisema kwa mwaka huu ingawa kitaifa zitafanyika kisiwani Unguja, lakini na wananchi wa Pemba watapata fursa ya kushiriki, kwa vile hata kisiwani humo zitafanyika.

Alieleza kuwa, hadi sasa mgeni rasmi kwenye kilele kinachotarajiwa kufanyika kisiwani Pemba, ni mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Hemed Suleiman Abdalla, ambapo kabla ya kilele hicho, shughuli kadhaa zitafanyika kisiwani hapa.

Alisema, Febuari 3, wamewatembelea wanafunzi na walioko rumande, kwenye mahabusu ilioko Wete, ili kuwasikiliza changamoto zao na namna mahakama wanavyoiona kiutendaji.

Alifafanua kuwa pamoja na ziara hiyo, ya wiki ya kuelekea siku ya sheria Zanzibar, watendaji wa mahakama pamoja na wadau wao taasisi ya huduma ya sheria kwa umma, Febuari 4, watawafikia wananchi wa kijiji cha Maziwang’ombe wilaya ya Micheweni, kwa ajili ya kuwapa elimu ya kisheria.

“Pamoja na kwamba tumo kwenye shamra shamra za kuelekea siku ya sheria Zanzibar, lakini pia tunadhamiria ya kuwaelekeza wananchi hao pamoja na wale wa Shehia ya Mwambe wilaya ya Mkoani, umuhimu wa kutoa ushahidi,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, Hakimu huyo dhamana wa mahakama ya Mkoa wa kaskazini Pemba, alisema kama inayoeleweka kuwa nchi imekumbwa na janga la udhalilishaji na dawa za kuelvya, hivyo lazima wananchi waelimishwe umuhimu na maana ya ushahidi.

Aidha alifafanua kuwa, Febuari 6 watendaji hao wa mahakama na wadau wao, watakwenda kwa wananchi wa Jimbo la Ole kwa kazi kama ya shehia za Mwambe na Maziwang’ombe.

“Ndugu waandishi wa habari tuelewe kuwa, watendaji wa mahakama katika kuelekea mwaka wao mpya wa kazi, umepanga kuwa Febuari 9 ni kushiriki katika matembezi maalum yatakayoongozwa na Afisa Mdhamini wizara ya Katiba na Sheria Pemba Mattar Zahor Massoud, yatakayoanza mahakama kuu Chake Chake, na kumalizia uwanja wa Gombani.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, hakimu huyo dhamana wa mahakama ya mkoa wa kaskazini Pemba Abdalla Yahya Shamuun, alisema suala la watuhumiwa wa udhalilishaji kupewa dhamana, kwa makosa yasio na dhamana lipo kwenye mamlaka ya mahakama kuu pekee.

Alisema awali, mamlaka ya kutoa dhamana kwa makosa yasio na dhamana yalikuwa mikononi mwa Jaji mkuu pekee, na baada kuonekana kuna tatizo, wapo mawakili wa kujitegemea walifungua ombi mahakama kuu ‘petition’ na mahakama ikiamuru sasa dhamana iwe kwa majaji wote.

“Hili jambo ni zito, ukiangalia mahakama kuu inamlaka makubwa ya kusikiliza kesi za aina zote, ndio maana majaji wa mahakama kuu, wanatoa dhamana baadhi yao kwa nguvu walizopewa kisheria,’’alifafanua.

Baadhi ya wananchi wa mji wa Chake Chake, wameuomba uongozi wa mahakama, kuendelea kufanya kazi zake kwa uangalifu na kufuata sheria, ili wananchi warejeshe imani na chombo hicho.

Kassim Omar Hassan na Fatma Jaku Hashim, walisema kundi kubwa la wananchi wanahofu na utendaji wa baadhi ya mahakimu na majaji, kwa kule kutozingatia sheria wanapotoa hukumu zao kwa washitakiwa.

“Kwa mfano kosa linathibiti mahakamani kuwa fulani amebaka au amelawiti, lakini hukumu ya kukaa chuo cha mafunzo ni ndogo sana, wakati kwenye sheria iko wazi kuwa ni miaka 30 au maisha,’’alisema Kassim.

Ujumbe wa mwaka huu katika kuelekea siku ya sheria Zanzibar ‘dumisha utawala wa sheria na demokrasia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020’   .

Mwisho