Mahakama yaagiza kukamatwa mali ya mwanamke tajiri zaidi Afrika

 

Mahakama ya Angola imeagiza kukamatwa kwa mali na akaunti za benki za mwana bilionea wa rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos.

Kukamatwa kwa mali hiyo kunatokana na mipango ya serikali iliopo kukabiliana na ufisadi katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Utawala wa rais Joao Lourenco unataka kuchukua takriban dola bilioni moja ambazo umekuwa ukimdai bi Isabel Dos Santos na washirika wake.

Amepinga madai hayo na kusema kwamba hajafanya makosa yoyote wakati babake alipokuwa mamlakani.

Akidaiwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika, Bi Dos Santos anakadiriwa na jarida la Forbes kuwa na mali yenye thamani ya dola bilioni 2.2.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 46 anaishi ughaibuni, akisema kwamba aliondoka Angola kwa kuwa maisha yake yalitishiwa.

Angola ni taifa la pili katika uzalishaji wa mafuta barani la Afrika.Haki miliki ya pichaAFP
Image captionAngola ni taifa la pili katika uzalishaji wa mafuta barani Afrika.

Anaendesha biashara kubwa akiwa na kampuni nchini Angola na Portugal ambapo anamiliki hisa katika kampuni ya Nos SGPS.

Mahakama iliagiza mali ya bi Dos Santos kupigwa tanji ikiwemo kaunti zake za benki mbali na hisa zake katika kampuni nchini Angola, ikiwemo ile ya Unitel na Benki ya Fomento de Angola BFA kilisema chombo cha habari cha taifa.

Katika taarifa alisema kwamba anashutumu kile alichokitaja kuwa shambulio linaloshinikizwa kisiasa.

”Nimegundua kwamba kesi ilifanyika kwa siri nchini Angola na uamuzi wa kupiga tanji mali yangu kutangazwa, hakukuwepo mawakili kutoka upande wangu, mbali na wakurugenzi wa kampuni zangu. Tuliambiwa kuhusu uamuzi huo baada ya kuamuliwa nyuma yetu. Nimetumia muda wa saa 24 nikijaribu kuwahakikishia wafanyakazi wangu na familia zote zilizoathiriwa na agizo hilo kwamba hatutakubali. Nitatumia kila njia Angola na sheria za kimataifa kupigana dhidi ya agizo hili na kuhakikisha kuwa ukweli unajulikana”.

Bi Dos Santos alijipatia umaarufu mkubwa 2016 wakati babake alimteua kwa njia ya utata kuwa mkuu wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali Sonangol.

Alifutwa kazi katika wadhifa huo na Lourenco, mrithi aliyeteuliwa na babake.

Nduguye Jose Filomeno Dos Santos anakabiliwa na kesi ya ufisadi nchini Angola, ambapo upande wa mashtaka unasema kwamba yeye na wenzake walisaidia kutoa nje ya taifa hilo fedha za Angola za dola milioni 500.

(bbc)