Majalada 104 ya kesi za udhalilishaji yapokelewa kwa DPP Pemba 2019

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

JUMLA ya majadala 104 yanayohusu kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto pekee, yamepokelewa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kisiwani Pemba, yakitokea Jeshi la Polisi, kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana.

Kati ya hayo, ni majalada 85 pekee ndio yaliofunguliwa, ambapo ofisi hiyo yenye mamlaka ya kuendesha jinai, iliyafungua baada ya kujiridhisha, na majalada megine 10 kati ya yale 104 yalirejeshwa Polisi, kwa hatua nyingine za kisheria.

Akisiwalisha ripoti ya mwaka ya utendaji wa kazi wa ofisi ya DPP Pemba, wakili wa Serikali na Mwendesha Mashitaka Ramadhan Suleiman Ramadhan, alisema majalada hayo 10, walitoa maelekezo ya kuyafanyia uchunguuzi wa ziada.

Alisema majalada mengine 10, waliamuru yafungwe moja kwa moja, kutokana na kutokuwa na ushahidi hata mdogo unaoweza kumtia hatiani mtuhumiwa husika.

Wakili huyo alieleza kuwa, majalada hayo 85 ambayo kwa mwaka 2019 waliyapandisha mahakamani, ni 15 pekee ndio yaliomalizika na kutolewa uamuzi, na moja pekee ndio lililopatiwa hatia.

“Utaona kuwa, pamoja na watuhumiwa wa udhalilishaji kufikishwa mahakamani, lakini 15 yalifanyiwa kazi na mmoja tu ndie alietiwa hatiani na 14 mahakama iliwaachia huru,’’alifafanua.

Alisema miongoni mwa sababu ambazo anafikiria kuachiwa huru watuhumiwa wa makosa hayo, ni ujazwaji usio mzuri wa fomu za PF3 unaofanya na baadhi ya madaktari.

“Unakuta fomu ya PF3 inamstari mmoja tu, na wakati mwengine mnakaribia kujitolea uamuzi wenyewe, kwamba hii kesi tusiende nayo mahakamani, maana ina taarifa finyu na zisizofahamika,’alieleza.

Katika hatua nyingine, wakili huyo wa serikali alisema, hata baadhi ya madaktari kutotoa matokeo ya uchunguuzi sahihi wanaowafanyia watoto waliodhalilishwa, sambamba na kuwepo kwa maombi kadhaa ya wahanga wa matukio ni moja ya sababu za kutopatiwa hatia.

Kwa upande wake, Hakimu wa mahakama ya Mkoa Chake Chake Luciano Makoye Nyengo, alisema ni vyema wanakamati hiyo wa kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto, wakawafunza wanajamii namna ya kuzuia matokeo hayo.

Alisema, sio vyema kuona jamii imeshindwa malezi ya watoto wao kikamilifu, na kisha wakategemea vyombo vya sheria kama mahakama ndio iwatie adhabu wale wanaowaharibu wao.

“Sisi tunaongozwa na Katiba, sheria, misingi na maandiko mengine, sasa ndio tunayoifuata wakati tunapoendesha kesi, sasa hatuwezi kumpa mtuhumiwa adhabu wakati ushahidi haumuunganishi na kosa lake,’’alieleza.

Nae Afisa Mipango wa wilaya ya Chakechake Kassim Ali Omar, alisema kazi kubwa sasa inayohitajika kwa jamii ni kushirikiana kikamilifu na vyombo vya sheria.

“Jamii ione aibu na haya, sasa kesi za udhalilishaji kuzifanyia sulhu, maana athari yake huwapa nafasi wabakaji na wadhalilishaji wengine kuwa wale wale kwa kila siku,’’alisema.

Akiwasilisha ripoti ya mkutano uliopita Afisa Hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake Chake Rashid Said Nassor, alisema elimu ya watoto kujitambua na kusema ‘sitaki’ inahitaji sana.

Alisema, bado watoto hawajajengwa ilivyo kisaikologia, ili waweze kutoa taarifa mara wanapoona dalili au baada ya kufanyiwa udhalilishaji.

Akichangia mada kwenye mkutano huo, Robert Miguwa Ndalami kutoka kanisa katoliki Chake Chake, alisema adhabu za mahakamani zikiwa kubwa kama sheria ilivyoelekeza, inaweza kuwa fundisho kwa wengine.

Daktari Mohamed Ali Jape, alisema mkazo wa kuwekwa kwa sasa, ni kuhakikisha daktari atakaebainika kuzembea ujazaji wa fomu ya PF3, ni sheria kuchukua mkondo wake.

“Haiwezekani sisi kamati tunatafuta dawa ya kutokemeza matendo haya, kisha atokee daktari akubali kuchukua chochote ili kuyapindisha matokeo ya uchunguuzi, hilo sio sahihi hata kidogo,’’alifafanua.

Hata hivyo wajumbe wa kamati hiyo wamependekeza, kuziandikia mamlaka husika wakiwemo watunga sera, ili kuona Zanzibar inakuwa na sheria zinazoshabihiana na muelekeo wa imani zao.

Kamati hiyo ya wilaya ya Chake Chake ya kupamba na ukatili wa wanawake na watoto, imeanzishwa kwa matakwa ya agizo la rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, alilolitoa wakati akiuzindua mpango wa kitaifa wa miaka mitano 2017/2022 wa kupamba na udhalilishaji.

Mwisho