Makala: Hivi ndivyo watoto Pemba wanavyoteseka kwa ajira mbaya

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA +255778911533

WATOTO watumikishwa            Kazi ngumu kufanyishwa,                              Hali hii inatisha                                     Yafaa kufikiriwa.

Twafanyishwa kazi nyingi,                   Kwa malipo ya shilingi,                         Huwa twanyimwa msingi,                    Wa elimu kupatiwa

Ukiingia kastamu,                                    inakuumiza damu,                                                     Kuna mambo kem kem,                         Yanayo taka hatua.

Wengine humo melini,                           Biashara mkononi,                                                Hii ndio hali gani,                                   Watoto tunofanyiwa

Ni baadhi tu ya beti kadhaa za mfumo wa mashairi nilizonukuu toka kwa wanafunzi wa skuli ya msingi ya Jadida Wete Pemba, wakati ulee tulipokuwa tukisaka elimu mwaka 2005.

Sahauri lenye maudhui ya kuondoa utumikishwaji wa watoto katika jamii, ambao uliwavutia wanafunzi wengi kwa wakati ule na leo bado nayakumbuka.

Ingawa baadhi ya watoto sio matakwa yao kufanya biashara hizo, lakini wanalazimika kufanya, kutokana hali ngumu ya maisha yao.

Kila siku zinaposonga mbele, tunashuhudia mambo mengi wanayofanyiwa watoto wanaotumikishwa, ambayo huwaathiri katika maisha yao.

Mfano, kufanyiwa vitendo vya udalilishaji, kupigwa, kutukanwa, kubakwa, kulawitiwa na kuibiwa hata kile wanachokipata.

“Kuwatumikisha watoto ni njia moja wapo ya kuwadhalilisha, kwani wanaathirika kielimu, kimwili na kiakili, hivyo humsababishia kudumaa”, anaeleza mwananchi Salma Bakar Ali wa Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete.

Anasema, suala la utumikishwaji wa watoto limekua likiendelea katika jamii, huku likionekana ni kama jambo la kisheria kwao kulifanya.

“Kuna baadhi ya wazazi huwapa watoto wao biashara kama za kutembeza bidhaa zinazotoka baharini mfano chaza chowe na tondo kwenda kuuza mjini Wete, hii husababisha watoto kukosa elimu kwa mtiririko,’’ anasema.

Khadija Henoick Maziku yeye ni Mratibu wa Wanawake na Watoto shehia ya Mjiniole, anasema unapomtumikisha mtoto hukumbwa na udumavu wa kiakili na kukosa ufamu nzuri anapokua darasani.

“Hapa watoto na familia zao, husahau ule msemo wa watu wa kale kua, ‘elimu ni ufunguo wa maisha na wengine wakaongeza kua elimu ni hazina,’’anafafanua.

Kwa uzoefu wake na hasa eneo analoishi kuwepo kwa ajira za watoto zinazozalishwa na wazazi kwa kule kuwapa bidhaa kama za mboga na bilingani kutembeza hata, inamfanya afikirie biashara tu na sio kitu kingine.

Asha Juma Ali wa miaka 62 wa Chasasa Wete anasema, watoto wanaotumikishwa kwa kupewa biashara kuuza wanahatarisha maisha yao na utu wao.

“Zamani ilitokea mtoto kubakwa, alikua anatoka kijijini kuja kuuza chaza mjini, kilichotokea… kulikuwa na mwanaume ambae alimwita na kununua kombe zote na kisha kumuingiza ndani mpaka jioni,’’anasimulia.

Alishangaa wazazi hufurahia sana pesa wanazoletewa na watoto wao baada ya kurudi kuuza biashara, pasi na kujua imenunuliwa kwa njia gani.

Maryam Said Ali mwenye miaka 40 wa Shehia ya Shengejuu anasema watoto wenye kadhia hiyo, huchoka miili yao kutokana na kutembea masafa marefu tena kwa miguu.

“Lazima awatafute wateja popote walipo, jambo ambalo linasababisha kutembea masafa ambayo mtu mzima ni vigumu kwenda, lakini yeye hufanya, hii ni athari nyingine,’’anasimulia.

“Wakati mwengine wanaingia skuli mchana, hivyo huacha kwenda madrasa na kwenda kuuza biashara na hufika muda wa kwenda skuli bado hawajarudi kwa masafa yalivyomarefu,’’ anaeleza.

Afisa Ustawi Hifadhi ya Mtoto Nafhat Salim Yahya anasema, njia wanazopita watoto hao sio salama, kwani kuna vichaka, wanaweza kuibiwa, kutoroshwa na hata kufanyiwa ubakaji na ulawiti.

“Kwa kweli watoto wanaopewa biashara hukumbana na udhalilishaji mkubwa sana, lakini bado jamii haijampa umuhimu mtoto, juu ya umuhimu wa elimu pamoja na haki zake nyingine anazostahiki”, anafafanua.

Nafhat aliishauri Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kupinga utumikishwaji wa watoto sambamba na kutekelezwa ipasavyo Sheria iliyopo, ili kukomesha hali hiyo ambayo inawanyima haki zao za msingi.

Salum Ali Khatib mwenye umri wa miaka 25 mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo ambae hufanyia kazi zake mjini Wete, anawaona watoto wanapita na visinia vya madagaa na wengine wamejitwika vikapu vya kombe.

“Wakipita nina kawaida ya kununua baadhi ya siku, ila kwa watu wa dunia ya sasa walivyoharibika, watoto hao wako hatarini kwani wanaweza kufanyiwa ukatili”, anafahamisha.

Siti Suleimani Juma yeye ni Afisa wanawake Wilaya ya Wete anawataka wazazi kutimiza majukumu yao kwa watoto, ili kumkinga na matendo maovu.

“Wasiitupie mzigo Serikali pekee, wazazi wadumishe ndoa zao ili waondoe ajira kwa watoto, maana aghlabu wanaotumikishwa huwa wanaishi na mzazi mmoja, ambapo hukosa huduma stahiki”, anaeleza.

Kwa msisitizo anawataka wazazi hasa akinababa wawahudumie ipasavyo watoto wao na kuwaelekeza, kwani kila mmoja ni mchunga na ataulizwa alichokichunga.

Amina Shehe Hamad mwenye miaka 30 mkaazi wa shehia ya Kangagani anasema, mtu mbaya anapata fursa ya kumuharibu mtoto anaeuza biashara, kwani anakuwa huru na hana ulinzi.

Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 38 mkaazi wa Shehia ya Utaani Wete anasema alishawahi kumshuhudia mtoto aliekua akiuza samaki wa kutembeza mtaani na kisha kulawitiwa.

“Ingawa mshitakiwa aliemfanyia kitendo hicho alipelekwa mahakamani na baada ya kumaliza ushahidi alifungwa, lakini mtoto hakuendelea tena kusoma na hakurudi tena katika hali yake ya kawaida”, anahadithia.

Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed anaelezea, watoto hutumikishwa kwa sababu kadhaa ikiwemo hali ngumu ya maisha kwa familia.

“Wananchi wanapishana kipato na kila kukicha mahitaji yanaongezeka, kutokana na ukuaji wa maendeleo katika nchi, hivyo ili wapate mahitaji ya msingi, mzazi humpa mtoto biashara kwenda kuuza”, anaeleza.

Haroub alitaja kuwa ni uwelewa wa watu wenyewe, kwani utumikishwaji hauji moja kwa moja kwa wazazi, bali huwa ni watu wa karibu ama majirani.

Anawashangaa wananchi ambao hawaangalii haki ya mtoto bali wanajiangalia wao tu na kujiona bora, jambo ambalo humsababishia mtoto kukosa matunzo bora.

“Mtoto anaetumikishwa kiajira ni tofauti na mtoto alietulia, muda wake anautumia vibaya, hapati kupumzika na pia anaweza kuwa omba omba kutokana na kuzoea matumizi mapema”, anafafanua.

Anasema, mtoto mwenye kutumikishwa anatembea barabarani na mitaani na hufanya biashara na watu wa rika tofauti, hivyo anasoma tabia za watu tofauti, ambapo huiga taaluma ya kufanya mambo ya ajabu kama wizi na utapeli.

Haroub anasema hata uokotaji wa karafuu zilizoanguka ‘mpeta’ ni sehemu hatarishi ya watoto, maana tayari katika kipindi hichi watoto wawili wameshabakwa eneo la Wete pekee.

“Athari kubwa ya watoto kutumikishwa kwanza ni kubakwa, kulawitiwa, kukashifiwa, kunajisiwa na watu hasa wenye umri mkubwa,’’anasimulia.

Mfano wa visa hivi vya athari vya watoto kutumikishwa na kuokota mpeta wa karafuu, vilitokea mwezi Disemba 27 mwaka 2019 na hili lilikuwa majira ya saa 6:00 usiku baada ya kutoka nyumbani kwao.

Mtoto mwenye umri wa miaka 17 mkaazi wa Ukunjwi Wilaya ya Wete anaeleza, lazima auze kombe ili wapate kujihudumia kutokana na kukosa mtu wa kuwashughulikia huduma zao za kila siku.

“Naenda skuli siku zote na mwaka huu nimeingia kidato cha nne, lakini kila Jumamosi na Jumapili lazima nije mjini kuuza, nafuatana na huyu mtoto wa dada yangu anaesoma darasa la tatu”, anasema.

Huku machozi yakimtiririka kutokana na mama yake ameshaachika, hivyo kwa vile hana mtu wa kumuhudumia, hulazimika kwenda kutafuta kombe na dada zake wengine ambapo yeye anauza.

“Mtu yeyote akiniita ndani kwa kununua kombe hatwendi, kwa sababu watu ni wabaya, simuamini mwanaume wala mwanamke na nilianza kazi hii toka darasa la tatu”, anaelezea.

Mama wa mtoto huyo anaeleza kua, hapendi kuwatuma watoto lakini kutokana na kukosa msaidizi katika maisha yake ya kila siku, ndio hulazimika kumtuma mwanawe huyo.

“Wapo mama kama mimi wao wanawaume, au familia za kuwasaidia ili mkono uende kinywani, mimi niko peke yangu, sasa nisipowatuma watoto kuuza chaza mjini siku hiyo hata taa haiwaki ndani, nifanyeje sasa,’’anahoji.

Pamoja na hilo anasema, bado suala la mwanawe kutafuta elimu analipa kipaumbele cha pekee, akiamini ndio hazina ya sasa na baadae.

Mtoto mwengine mkaazi wa Mtambwe mwenye miaka 13 alithibitisha kupewa biashara hiyo na wazazi wake, ili wapate walau shilingi mbili zitakazowasaidia kutatulia shida zinazowakabili.

“Sijawahi kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, lakini mimi mwenyewe najisikia aibu kutembeza chaza ila nitafanya nini na sisi tuna shida, tunahitaji msaada”, anaeleza.

Anasema umasikini wa kipato kwa wazazi wake anaona ni moja ya sababu ya yeye kutumikwisha juu ya uuzaji wa bidhaa hizo.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TanzaniaTAMWA’ tawi la Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wamekuwa wakipiga vita aina za udhalilishaji kwa wanawake na watoto, ingawa suala la utumikishwaji bado hawajalishughulikia ipasavyo.

“Sasa ipo haja ya kulishughulikia kwani ndio chanzo cha udhalilishaji kutokana na uwezo wao wa kufikiri bado ni mdogo, hivyo huweza kufanyiwa vitendo hivyo”, anasema.

Athari moja kati ya nyingi za watoto kutumikishwa kukosa haki zao za msingi na kusababisha makuzi yao kiafya kuwa mabaya.

Tatu Abdalla Mselem ambae ni mratibu kutoka jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), anasema wapo watoto hufanya ajira ya kingono na kupeleka pesa nyumbani, ilhali mama anajua lakini wengine huwaachia huru.

“Athari ipo maana itakuwa hasomi, atafanya kazi za nguvu ambazo kwa umri wake haumruhusu, atafanya kazi za hatari, kwani hajaweza kupambanua kuwa hizi kazi ni za hatari au ni salama kwake,” anaeleza.

Naibu Mrajis mahakama kuu Pemba Abdul-razzak Abdul-kadir Ali anasema hakuna kesi ya utumikishwaji wa watoto iliyoripotiwa mahakamani, pamoja na kwamba hilo ni kosa la jinai.

“Ni uwelewa mdogo kwa jamii na mtoto mwenyewe, kwani anajikuta anapata maslahi hivyo, haoni sababu ya kushtaki na ananyamaza ili aendelee kupata zaidi”, anasema.

“Ingawa hali ya kimaisha inachangia, ambapo wazazi hawamkatazi mtoto wao, kwani wanafaidika wote, lakini ni kosa kisheria, inatakiwa hata majirani wanapoona hali hii waripoti”, anafahamisha.

Hata Mkataba wa kimataifa juu ya kulinda haki za mtoto umesainiwa Novemba 30 mwaka 1989 na kutiwa saini ni nchi 197 ikiwemo Tanzania, umeeleza wazi haki za watoto, kijamii, kisiasa na kiuchumi pia unapinga aina zote za udhalilishaji na utumikishwaji wa watoto.

Ambapo mkataba wa Afrika juu ya haki na ustawi wa mtoto ambao umepitishwa na Umoja ya Afrika (AU) Julai 1 mwaka 1990 na kuanza kazi 1999 ambapo Tanzania ni mwanachama wa mkataba huo.

Na baada ya Tanzania kuridhia mikataba hiyo ndio maana ikaanza taratibu za kutunga Sheria maalumu ambayo itahusu haki za watoto.

Sheria ya ajira namba 11 ya mwaka 2005 katika vifungu vya 6 (1) (2) (3) (4) na 7 (1) (2) (3) cha Sheria ya mtoto namba 6 ya mwaka 2011 inapinga utumikishwaji wa watoto.

Kifungu cha 6 (1) kinaeleza kua mtoto hatakiwi kutumikishwa ajira yeyeote mbaya zaidi, ambapo (2) kikikataza ajira kwa mtoto kwa kazi yeyote isipokuwa shughuli nyepesi za ndani.

Kifungu cha 6 (3) kinaeleza, shughuli nyepesi lakini mzazi au mlezi ahakikishe mtoto huyo anapata muda wa kushughulikia masomo yake na muda wa kutosha wa kupumzika.

Ambapo kifungu kidogo cha (4) kinaeleza  kuwa mtu yeyote ambae atamtumikisha mtoto kinyume na vifungu hivyo, kimetoa adhabu ya kupigwa faini isiyopungua shilingi 500,000 akishindwa atalazimika kutumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

Kifungu cha 7 (1) (2) kimeorodheshwa kazi ambazo mtoto kushirikishwa au kupewa utumwa, biashara za kuuza watoto, kulazimishwa kufanya kazi, kutumikishwa katika jeshi, ukahaba au picha za ngono, kusafirisha madawa ya kulevya na kazi nyengine yeyote ambayo inaathiri afya, usalama na maadili ya mtoto.

Kifungu cha 7(3) kimetoa adhabu kwamba, atakaekwenda kinyume atapaswa  kulipa faini isiyopungua milioni tatu au  chuo cha mafunzo kwa muda usiopungua mwaka mmoja au adhau zote mbili.

MWISHO.