Mama aliemtupa mwanawe mchanga apata ugonjwa wa kuokota makopo Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAMA aliemtupa mtoto wake kichakani muda mfupi baada ya kujifungua miezi minne iliopita, shehia ya Dodo wilaya ya Mkoani Pemba, ameripotiwa kupatwa na ugonjwa unaomsababishia kuokota makopo, kijisaidia ovyo, kulala popote na kupiga watu kwa baadhi ya wakati, hali inayopelekea, wanafamilia kulazimika kumfungia ndani wakati mwingine.

Taarifa zilizopatikana kutoka kijijini hapo zinaeleza kuwa, mama huyo Khadija Hamad Ali miaka 30, amekuwa akipita pita kwenye majaa na kuokota makopo, mifuko, nguo chafu na kuburura vipande vya miti ovyo ovyo.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, pamoja na mama huyo kuwa na tabia hiyo, lakini pia amekuwa akijisaidia haja kubwa na ndogo popote inapomtokezea, bila ya kujali eneo hilo kuwa panamkusanyiko wa watu au kando ya barabara kuu.

Baadhi ya wananchi wa Dodo waliokataa majina yao yasichapishwe kwenye pembatoday, walisema, mama huyo ameanza mabadiliko hayo ya tabia, tokea mwezi Julai mwaka huu, wiki tatu tu baada ya kumtupa mwanawe mchanga wa siku moja.

Walisema, wakati mwingine mama huyo akili humjia vyema na kufanya shughuli zake kama kawaida, ikiwemo usafi wa ndani ya nyumba, kupika, kufua na hata kuwaosha watoto wake.

Walieleza kuwa, lakini hayo huyafanya kwa muda mfupi tu na haizidi siku nne ndani ya mwezi, hurejea kwenye hali yake ya mabadikilo ya kiakili na kuanza kufanya mambo ya maajabu na ya kusikitisha.

“Anaweza akakupita hapa amebeba matambara, machanja ya miti, makopo, chupa chafu, nguo hakuvaa vizuri na hapo ukimtania kidogo tu anaweza kukushambulia kwa kukupiga,’’alisema mwananchi mmoja.

Kaka wa mwanamke huyo Ali Hamad Ali, alithibitisha dada yao kupatwa na ugonjwa unaofanana na wa akili, hasa kutokana na matukio ambayo sio ya kawaida, anayoyafanya.

Alisema, suala la kujisaidia ndani ya nyumba yao haja zote, kumwanga maji, kuvunja vyombo kama masufuria na kuwapiga watoto ni jambo la kwaida kwake.

Alibainisha kuwa, baada kuona tofauti za kitabia kwa mama huyo, walimfikisha hospitali na kupatiwa dawa, ambazo hazikumsaidia sana na sasa hawajui wapi waende nae.

“Unajua, nao umaskini unatuzonga, hata tukiambiwa tuende nae Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, au Unguja kwa ajili ya matibabu yake, hatuna uwezo sasa tupo tunamuangalia tu,’’alifafanua.

Katik hatua nyingine, kaka huyo, alisema amekuwa na kawaida kila anapomaliza kujifungua dada yake, hupatwa na mabadiliko ya kiakili, lakini huwa haizidi wiki mbili, ingawa kwa sasa hali hiyo ameshatimiza miezi minne sasa.

“Ni kawaida kila anapomaliza kujifungua huyu dada, huwa kiafya hasa ya akili haipo vizuri, lakini kwa mwaka huu, baada ya kujifungua amechukua muda na huwenda huu ugonjwa wa akili umeshamkumba,’’alifafanua.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Shadya Shaaban Seif, ameishauri familia ya mama huyo, kumfikisha kijana wao, kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili iliopo Wete Pemba.

Alisema ni vyema wakaangalia uwezekano wa kumfikisha kwa wataalamu ili, kufanyiwa uchunguuzi wa kina na kujiepusha na matumizi ya dawa za miti shamba pekee.

Mtaalamu wa magonjwa ya binaadamu wa hospital ya Chakechake Pemba dk: Rahila, alisema kama ni ugonjwa wa afya ya akili, unahitaji matibabu endelevu na sio tiba ya siku moja, hivyo ni vyema familia hiyo, ikaenda tena hospitali kwa uchunguuzi zaidi.

‘Unajua mazingira ya mjamzito, na kisha harakati za kujifungua huchanganya mambo ambayo kama familia haikuwa makini wanaweza kukukosa, lazima wawe karibu na wataalamu wa afya ili wapate tiba,’’alishauri.

Familia ya mama aliemtekelekeza mwanawe mchanga wa siku moja kichakani, na kisha kuokolewa na Mbwa shehia ya Dodo wilaya ya Mkoani Pemba, imesema huwenda mama huyo ameshakumbwa na ugonjwa wa akili, kutokana na mambo ya siri kufanya hadharani.

Mwezi Julai mwaka huu, mama huyo aliripotiwa kituo cha Polisi Chakechake, kwamba alimtupa mtoto wake aliejifungua nje ya ndoa, muda mfupi na kisha mtoto huyo kubebwa na Mbwa hadi kwenye makaazi ya watu, na kwa sasa mtoto huyo analelewa na serikali kisiwani Unguja.

Watoto 142 waliripotiwa kutupwa na wazazi wao baada ya kujifungua, kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2017, ripoti ya kihalifu ya Jeshi la Polisi Tanzania imeeleza.

Kati ya idadi hiyo, Mkoa wa kaskazini Unguja, kuliripotiwa watoto wawili, Kusini Unguja mmoja, wakati mikoa ya Mjini magharibi, kusini Pemba na Kusini Unguja hakukuripotiwa matukio hayo.

Mwisho