Maryam Saleh Juma, mwanamke anaelitamani Jimbo la Ole, aahidi neema tele

Maryam Saleh Juma: Mwanasiasa mwenye uchu wa kulibadili Jimbo la Ole

Ataka akopeshwe kura kupitia chama cha Ukombozi wa Umma alipe maendeleo

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

SASA ni mwendo wa saa 11:05 jioni, nipo moja ya kijiji kilichomo ndani ya Jimbo la Ole wilaya ya Chake chake Pemba.

Jua limeanza kupotea pote, kivuli na kipepo chemba mba kinashuhudiwa chini ya Muwembe ambapo kwa mbali naona kundi la watu.

Nilivuta hatua kama 14, nilipokaribia kwanza niliona mwanamke akiwa juu ya kiriri, nilidhani ni mkutano ya mijadala baina ya wakiristo na waislamu.

Nilipofika hasa baada ya kuchengua chengua watu waliokuwa karibu yangu, nilimuona mtu ninae mfahamu kwa sura kutokana na ujasiriamali wake.

Mwaka 2016, mwanamke huyo aliyekuwa juu ya jukwaa niliwahi kumuandikia habari juu ya ujasiriamali, hivyo ilikuwa rahisi kuvuta kumbu kumbu.

Lakini kwa vile ni mkutano wa hadhara nilivuta kalamu na karatasi, nikaanza kuandika ahadi za mgombea huyo.

“Kama mkinipa ubunge kupitia chama change cha Ukombozi wa Umma, basi nitaweka siku maalum ya kukutana na wanawake na wanaume ili waeleze shida zao,’’nilinukuu sehemu ya ahadi yake.

Kumbe nilimkumbuka jina lake, mgombea huyo wa ubunge wa Jimbo la Ole wilaya ya Chake Chake kuwa ni Maryam Saleh Juma.

Jengine anasema lililomsukuma kuomba ubunge ndani ya Jimbo la Ole, ni kuona wanawake wa vijiji hivyo, hawajapata mbunge ambae ni mtetezi wa shida zao.

Akiwa juu ya jukwaa hilo, huku akishangiliwa na wanawake na wanaume walikuwa kwenye mkutano huo wa kampeni, mgombea huyo wa ubunge amesema wakati umefika kwa wananchi hao kubadilika.

Anasema, huu sio wakati wa kuchagua chama kama ilivyokuwa chaguzi tano zilizopita, bali sasa waangalie mgombe hata kutoka kwenye chama chengine mwenye hamu, shauku ya kuwakomboa.

“Wananchi wa Jimbo la Ole, mwaka huu 2020 Allah amewapenda kuwaletea mimi Maryam Saleh Juma ninae gombea ubunge Jimbo hili, sasa musiangalie chama change niangalieni mimi,’anashauri.

Anasema yeye kama mwanamke, ana hamu, uchungu, pupa la kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ole wanapata neema ikiwemo kutatuliwa shida zao.

HUDUMA YA MAJI

Anasema yapo maeneo ndani ya Jimbo hilo bado kuna shida ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, ambapo anasema kama akichaguliwa hataki kuona mwanamke  anajitwisha ndoo.

“Ni aibu hadi sasa huduma ya maji safi na salama kuwa baadhi ya maeneo yanapatikana kwa usumbufu na baadhi ya vijiji wanatumia visima vya kata, sasa mkinichagua hili litakuwa ndoto,’’anasema.

HUDUMA ZA AFYA

Amewahakikishia wapiga kura wa Jimbo la Ole, kuwa mwanamke ndie anaejua shida za wanawake wenzake, hivyo amewataka wananchi wote wamkopesha kura ili aimarishe huduma za afya.

Mbele ya wananchi hao, mgombea huyo Ubunge wa Jimbo la Ole kwa tiketi ya cha UMMA, amesema atahakikisha wanawake kwanza wanajifungulia hospitali.

Anasema gharama zinazohitajika ikiwemo usafiri wakati wote kwa mama wajawazito, iwe wa kwenda na kurudi kliniki atalibebea hilo ikiwa atapewa ridhaa.

VIKUNDI VYA USHIRIKA

Mgombea huyo anasema kwa vile amezaliwa na kukulia kwenye vikundi vya ushirika hasa vya wanawake, anasema suala la kuwawezesha kiuchumi ndio kipaumbele chake.

Anasema, wanawake kama wakipewa fedha na kupewa mafunzo ya usimamizi wa fedha hizo kupitia vikundi vyao ya ushirika, hakuna mwanamke atakae kuwa mtegemezi.

“Bado wanawake waliowengi wakiwemo wa Jimbo la Ole ninalo gombea hawajapewa taaluma ya kutosha jinsi ya usimamizi wa fedha na kuendeleza vikundi vyao,’’anasema.

VIJANA AKIWA KAMA MBUNGE

Anasema, baada ya chama chake kumpitisha kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Ole, na akipewa ridhaa na wananchi, anataka kuona wanaendeleza kazi zao mbali mbali.

“Inawezekana vijana waliowengi ndani ya Jimbo la Ole wanaelekeza nguvu katika ukataji wa matofali, kwa kule kukosa kazi nyingine, lakini nikipata ubunge watafurahi,’’anasisitiza.

Anasema, kama wapo wanaohitaji mitaji ya kufanya biashara, kuingia katika kilimo cha mboga mboga au kufungua kituo kidogo cha ufundi, wakimpa kura hilo linawezekana.

WAZEE WA JIMBO LA OLE

Mgombea huyo ubunge pekee mwanamke wa Jimbo la Ole Maryam Saleh Juma, anasema hatazamii kuwasahau wazee, akiamini kuwa ndio wanaoweka mambo sawa kuelekea ushindi wake.

Amewaahidi kuwapatia mikopo na kuwaingiza kwenye miradi midogo midogo, ambayo itaendana na hadhi na afya zao, ili nao wasiwe omba omba kama ilivyo kwa baadhi ya maeneo.

Anasema, kutokana na kuwepo mfuko maalum wa mbunge, ndio ambao utamuwezesha kuhakikisha anatimiza ahadi zake hizo bila ya ubaguzi.

KILIMO

Maryam Saleh Juma, anasema kama akichaguliwa kushika nafasi hiyo, atakigeuza kilimo kwa wananchi wa Jimbo hilo kuwa kimbilio kama ilivyo baadhi ya maeneo ya Tanzania bara.

Anasema kwanza atahakikisha anawashawishi mabwana na mabibi shamba kuwepo ndani ya Jimbo lake kwa muda mwingi sambamba na kununua trekta moja kila baada ya miaka miwili.

“Wapiga kura wengi ambao Oktoba 28 watanipa jimbo kwa kura nyingi ni wakulima tena wa jembe la mkono, lakini niwahakikishie kununulia trekta japo moja ili liwasaidie,’’amewaahidi.

NANI MARYAM KISIASA NA CHANGAMOTO ZAKE

Anasema alianza kwenye miaka ya 96, kuingia kwenye siasa baada ya siku moja kupita wanawake wenzake wa CCM wakiwa na mavazi yao na kupendeza sana.

Alishawishika na kuingia ndani ya CCM kama mwanachama wa kawaida, ingawa baadae alihamia chama cha wananchi CUF kuanzia mwaka 2000.

“Siasa bado ni chaguo langu sana hadi sasa pamoja na kwamba ni mjasiriamali pia, lakini huku nilidumu kwa muda mrefu na nilikuwa mstari wa mbele,’’anasimulia.

Akiwa mwanachama wa kawaida wa CUF anasema alishapata sulubu mara tatu ya kulala kituo cha Polisi kwa kuzuliwa mambo ambayo hakuyafanya.

“Mara moja nilichukuliwa kituo cha Polisi nikiwa na kanga ya shingo, maana sikujua nani anayehodisha, nilipotoka nikachukuliwa ingawa baadae niliachiwa,’’anabainisha.

Kwenye heka heka za mwaka 2001, anasema alikuwa mbele, na anakumbuka hata kashi kashi la siasa lililotokea Mkoani Pemba, kwa mara ya kwanza aliweza kuyazima mabomu kwa gunia.

“Bomu lilianguka mbele yangu kama hapo, wakati huo nimevaa mavazi ya mwanamme, lakini nilikuwa na gunia na nikalivamia bomu na kulizima,’’anasema.

Anasema baadae, aliachana na chama hicho cha CUF ambapo aliirejesha kadi na kujiunga na NCCR-Mageuzi na kudumu nacho kwa muda wa miaka kumi.

Akiwa na NCCR- Mageuzi alichaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano mkuu taifa, baada ya kusota na nafasi za ukatibu na uwenyekiti ngazi ya wilaya.

“Kisha nilikihama chama, maana Mwenyekiti Mbatia anataka vyake na sisi na akina Kafulila tunataka chama kiendeshwe kwa mtindo, mwengine vurugu, zogo nikajiengua,’’anasimulia.

MARYAM NA CHAMA CHAKE CHA ‘UMMA’ CHA SASA

Kwa mwaka huu 2020, anatimiza miaka 20 akiwa ndani ya himaya ya Hashim Rungwe kiongozi mkuu wa chama hicho ambapo kwa sasa pia ni Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anakiri kuwa, chama hicho kama wanatafutwa waanziilishi kwa Tanzania basi yeye anaingia kwenye kitabu cha kumbu kumbu, kutokana na kushiriki mara dufu vikao.

Kwa sasa Maryam pamoja na kwamba ni mgombea ubunge wa Jimbo la Ole, pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kusini Pemba.

Ingawa anasema kutokana na ukata wa fedha ndani ya chama chao, ndio kati ya majimbo 18 ya uchaguzi yaliopo kisiwani Pemba, wamefanikiwa kwa mara kwanza kusimamisha wagombea watano.

Anasema Jimbo la Wawi kwa nafasi ya Uwakilishi yupo Mwanamke, na wengine wakisimama majimbo ya Ziwani na Ole.

Hata nafasi ya Ubunge wapo wagombea wawili tu kutoka majimbo ya Ole anapogombea yeye na jimbo la Wawi, ingawa anasema ana matumaini ya kushinda.

MAISHA YA MARYAM KABLA YA SASA

Maryam Saleh Juma ambae mwaka huu anatimiza miaka 48, alizaliwa kijiji cha Vitongoji wilaya ya Chake Chake, ingawa kwa harakati za wazazi wake alipata elimu ya skuli na kur-an kijiji cha Pandani wilaya ya Wete.

Anasema baada ya baba yake kufariki, mama yake alishindwa kumuendeleza kielimu na yeye baada ya kurudi kijiji cha Vitongoji akiwa mtu mzima, alianza kujitafutia fedha za halali kwa ubanjaji wa kokoto.

Ingawa kabla ya kurudi Vitongoji, akiwa Pandani alianza na ujasiriamali wa ususi wa makuti na kisha kuyauza na kupata fedha za kuiendeshea familiya yao.

Mwaka 1990 akiwa tayari ameshaingia kwenye ndoa, ujasiriamali ulianza kumuingia kichwani mwake, na hadi sasa ni mwalimu wa utengenezaji wa sabuni na bidhaa nyingine.

MUME WA MGOMBEA

Hamad Khamis Mwalimu anasema huu ni mfumo wa vyama vingi hivyo kila mmoja anayo haki ya kugombea na kwenda chama anachotaka.

“Mimi namsadia maana kwanza nimeruhusu kuingia kwenye chama atakacho, lakini pia nafuatilia sera zake zikinivutia, nitawashawishi na wenzangu,’’anasema.

“Unajua kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, hii ngoma kila mmoja anakatika nyonga kwa mshindo alioupenda, nami niko kwenye ACT,’’anafafanua.

WANAOMFAHAMU MGOMBEA

Haji Ali Omar wa Ole,  anasema wakati umefika sasa kupata mwakilishi na mbunge mwanamke ndani ya Jimbo la Ole akiamini kuwa ndio wanaoumwa na jimbo.

Asha Mmanga Hamad nae ambae ni mpiga kura, anasema safari hii atawashawishi wenzake kumpigia kura mgombea huyo, wakiamini mabadiliko makubwa.

Kama alivyo Asha, ni sawa na Mwajuma Mbarka akisema sasa wakati umewadia kwa wananchi kuacha kuchagua chama bali waangalie aina ya mtu.

“Maryam kwenye vikundi vya ushirika kafanya vizuri mno, sasa akipewa Jimbo hili la Ole kwa nafasi ya Ubunge mambo yatazidi kuchepua,’’anasema.

Mwanzoni mwa mwaka huu Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Ofisi ya Zanzibar  kwa upande wa Pemba ilizipitia shehia 36 kisiwani humo ili kuwahamasisha wanawake kuingia majimboni.

Akiongoza msafara huo wa kijiji hadi kijiji, Mratibu wa TAMWA Fat-hiya Mussa Said, anasema hakuna Katiba, maazimio wala mikataba inayomzuia mwanamke kugombea.

“Tena ikitokezea kwenye nafasi za udiwani, uwakilishi na hata ubunge katika Jimbo kuna mwanamke kajitokeza, basi apewe kura za ndio na wapiga kura,’’anasema.

Afisa Miradi wa TAMWA Pemba, Asha Mussa Omar, alisisitiza haja kwa wanawake kuendelea kufuata maadili ya kizanzibari hasa wanaogombea ili isiwachafue wengine wenye nia.

Uchaguzi mkuu wa sita wa vyama vingi nchini, unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu ambapo watanzania watawachagua madiwani, wawakilishi, Ubunge, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yule wa Zanzibar.

 Mwisho