Mgombea ubunge ADA-TADEA Mtambile kuanza na elimu ya juu akipata ridhaa

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Mtambile kwa tiketi ya chama cha ADA-TADEA Amina Muhammed Ali, amesema kama akipewa ridhaa, anakusudia kutoa ushirikiano na waalimu wa skuli za sekondari za jimbo hilo, ili kuhakikisha zinaingia kwenye 10 bora kitaifa.

Alisema anajiskia aibu kuona skuli za Zanzibar kila mwaka zinashika nafasi ya mwisho na kutoingia kwenye skuli 10 bora zikiwemo za Jimbo la Mtambile, hivyo kama akipewa ridhaa anakusudia kuondoa tatizo hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mgombea huyo, alisema hajaona sababu kuwa wanafunzi wa skuli za Tanzania bara skuli zao zinashika nafasi ya kwanza hadi ya kumi ingawa kwa Zanzibar hilo limekuwa ndoto.

“Mimi kama nikichaguliwa ntatumia hadi mshahara wangu kuwachukua vijana wenye ufaulu wa sayansi na ambao hawajaajiriwa na kuwapelea skuli za Kengeja, Mtambile, Kangani na Kisiwani panza ili kusaidia,’’alieleza.

Aidha mgombe huyo ubunge wa Jimbo la Mtambile kwa tiketi ya ADA-TADEA, alisema jengine analokusudia ni kuviinua vikundi vya wanawake na vijana kwa kuwapatia wataalamu.

“Kwa mfano wanawake wenzangu wa Kisiwa panza wao wamejiwekeza kwenye mwani, basi nitawaletea wataalamu kwanza wafundishwe kupanda ule wenye bei,’’alieleza.

Kuhusu watoto na familia zinaozoishi kwenye mazingira magumu, Mgombe huyo wa ubunge alisema atazipatia mitaji ya kujikomboa iwe ni kwenye kilimo, mifugo na biashara nyinginezo.

“Lakini hata wale mayatima na watu wenye ulemavu nao kama wananchi wa Jimbo la Mtambile watanikubali, nitawasaidia kwa hali na mali ili waishi kama makundi mengine,’’alifafanua.

Kuhusu ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeshea kampeni, alisema kwake hilo hilo halimshituwi maana uamuzi wake wa kuingia jimboni hautegemei fedha za chama.

“Unajua hakuna fomula kuwa kampeni lazima iwe ni mikutano ya hadhara, bali hata kukutana na wapigakura ana kwa ana, kupita kwenye mikusanyiko pia huko ni kufanya kampeni,’’alifafanua.

Aidha mgombea huyo, amewataka wanawake na wanaume wanapiga kura jimbo la Mtambile wamtilie kura za ndio, ili aimarisha huduma za kijamii ambazo hadi sasa hazijasimama imara.

Kombo Mjaka Mohamed na Othman Ali Suleima wa Mtmbile walisema mgombea huyo kama akipewa ridhaa anaweza kuwa muokozi mkubwa wa jimbo lao.

“Bado ndani ya jimbo letu kuna changamoto kama za watu wenye ulemavu, wanawake kwenye vikundi vyao, lakini kama mgombe huyo ubunge tena mwanamke ameahidi hayo apewe ridhaa,’’alisema Kombo.

Mwantatu Himdi Nassor na Shufaa Makame Ngwali wa Kisiwa panza, walisema kilio chao kwa sasa ni ukosefu wa mashine za kusarifia mwani.

“Huyu anaewania ubunge Jimbo la Mtambile ametuahidi kama akipata atatusaidia hilo, sasa kwa mwaka huu mimi kura yangu na muume wangu tutampa,’’alieleza.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA, kilizipitia zaidi ya shehia 35 za Pemba, ili kuwahamasisha wanawake kugombea nafasi mbali mbali.

Uchaguzi mkuu wa sita wa vyama vingi nchini, unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu ambapo vyama kadhaa kwa sasa vinaendelea kuchuuna kwenye viwanja mbali mbali kuomba kura.

Mwisho