Mgombea ubunge Chake chake kwa CHADEMA mshahara wake kuimarishia elimu

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chake Chake kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’ Rukia Abuu Mohamed, amesema kama akipewa ridhaa kushika nafasi hiyo, asilimia 20 ya mshahara wake, utatumika kwa ajili ya wanafunzi wenye mitihani ya taifa, kwa kuwaweka pamoja, ili kuongeza kiwango cha ufaulu.

Alisema, bado mikakati yake kweli haijawekwa na jamii, ya kuongeza kiwango cha ufaulu, na kuwaacha wanafunzi hasa wenye mitahani wakiranda randa ovyo, kwa kule kukosa kuwaweka pamoja ili kupata muda wa kujisomea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema anatamani kuwa mbunge na kisha kujikata asilimia 20 ya mshara wake kwa ajili ya wanafunzi waliopo dakhalia.

Alisema, anakusudia kukodi nyumba maaluma zilizokaribu na skuli na kisha wanafunzi wenye mitahani kuwepo hapo, ili wapate muda mkubwa wa kujisomea na hilo linaweza kuongeza kiwango cha ufaulu.

‘Mimi kama nikiwa mbunge wa Jimbo la Chake Chake, nakusudia kukaa pamoja na waalimu ili kuwaweka pamoja wanafunzi wenye mitahini, ambapo pamoja na misaada yangu, lakini hata mshahara wangu asilimi 20, utatumika kukamilisha hilo,’’alieleza.

Aidha mgombea huyo alisema, jengine analolikusudia kuwafanyia wananchi wa Chake Chake ni kuviimarisha vikundi kadhaa vya ushirika vya wanawake, ili sasa viwe kimbilio kwa jamii.

Alifahamisha kuwa, vikundi vya ushirika na vya hisa vya jimbo hilo vipo kadhaa, lakini kwa kule kukosa mitaji, elimu na mikopo havijaonekana kuzaa matunda ndani ya jamii.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa ubunge wa Jimbo la Chake Chaka kwa tiketi ya chama cha ‘CHADEMA’ Rukia Abuu Mohamed, ni kuyaimarisha mitaro ya maji machafu katika mji huo.

“Bado suala la uchafuzi wa mazingira ndani ya jimbo la Chake Chake ambalo ndio uso wa kisiwa cha Pemba, lipo na kama nikipata ridhaa, hilo nitashirikiana na Baraza la mji Chake chake kuona linaimarika,’’alifafanua.

Kwa upande wa vijana, aliwataka kumpigia kura na akishika nafasi hiyo, atawatafutia eneo maalum kwa ajili ya kufanya biashara, ili waachane na vibanda vidogo vidogo ambavyo vinaharibu mandhari ya maji.

Aidha amewaomba wananchi na wafuasi wa vyama vya ACT-Wazalendo, CCM, ADC, CHAUMMA, SAU, AFFP, NCCR- Mageuzi na wale wa CHADEMA kumpigia kura, ili aende bungeni kwa kuwatumikia.

Haji Makame Omar wa kijiji cha Chachani jimbo la Chake Chake, alisema kwa kuwa, jimbo hilo bado linachangamoto kubwa, huwenda akipewa mwanamke zikapungua.

“Mimi najua kuwa yupo mgombea ubunge wa jimbo hili kutoka CHADEMA, lakini kwa ahadi zake hasa za kuimarisha elimu na vijana, hata mimi nimeshawishika kumpigia kura,’’alieleza.

Yussuf Haji Iddi na Halima Omar Bakari, walisema jimbo la Chake Chake, linahitaji kiongozi anaeumwa na maendeleo kama alivyoonesha mfano, mgombea huyo wa CHADEMA.

“Kwa sisi tunaemfahamu Rukia, wala hana haja ya kufanya kampeni, lakini ni vyema akafanya, ili na wengine wamfahamu, ingawa ni mchapakazi hodari,’’alieleza Halima.

Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Chake Chake Lumkan Yussuf Abdi, anasema mgombea wao ubunge wa Jimbo la Chake Chake, chama kilimuamini kutokana na uchapakazi na uhodari wake usioyumba.

Alisema, mgombea huyo ameshahuduma nafasi kadhaa ndani ya CHEDMA, ndio maana hata alipoomba kuteuliwa na chama kugombea nafasi hiyo, alimuangusha mgombea mwanzake ambae ni mwanamme.

“Sisi CHADEMA tunawamini zaidi vijana na wanawake katika uongozi, ndio maana wapo akina Halima Mdee, Esta Matiku na Bulaya wamewaminiwa kama alivyo Rukia kwa jimbo la Chake Chake,’’alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema, hawaviogopi vyama vya CCM, ACT-Wazalendo na CUF na akisema kama uchaguzi utakuwa huru na haki, mgombea wao ataibuka mshindi.

Uchaguzi mkuu wa sita wa vyama vingi nchini, unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kwa kumchagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Mwisho