Mgombea urais Zanzibar abwaga manyanga ataja chama atakachokiunga mkono

 

IMEANDIKWA NA MWANDISHI MAALUM-PEMBA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHA UMMA) ambaye pia ni Mgombea wa Urais wa chama hicho Ali Omar Juma, amewataka wanachama wa chama hicho kumpigia kura ya ndio Maalim Seif Sharif Hamad ambae ni mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT- Wazalendo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwezi huu.

Akizungumza alipopewa nafasi ya kusalimia katika mkutano wa Mgombea Urais wa ACT -Wazalendo uliofanyika kijiji cha Ditia Jimbo la Wawi wilaya ya Chake Chake Pemba,  Juma amesema vyama hivyo vina ushirikiano wa kidugu katika historia ya kisiasa za Zanzibar  na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza huku akishangiriwa na wanancha wa ACT -Wanzalendo waliohudhuria mkutano huo, Mgombea huyo ambae kwa sasa ahatogombea tena urais kwa tiketi ya CHAUMMA, alisema chama hicho kimesikitishwa kuenguliwa kwa wagombea wa ACT, hivyo watahakikisha wanaungana kukiondoa Chama cha Mapinduzi CCM madarakani tarehe 28 mwaka huu.

“Leo nawatamkia kuwa chama changu cha UMMA, sasa kimeamua kuungana rasmi na ACT-Wazalendo na sasa kura za urais ambazo mlidhamiria kunitilia kura mimi, sasa kura zote ziende kwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT, Maalim Seif,”alisema.

Alisema Maalim Seif anafaa na sifa kubwa ya kuwa kiongozi hapa Zanzibar na ndio maana Chama cha UMMA kimeamua kumuungano kwa mwaka huu.

Akizungumza na wachanchi na wafuasi wa chama hicho, Mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT Maalim Seif Sharif Hamad, alisema akichaguliwa kuwa rais ataboresha utumishi wa Umma na Utumishi wa vikosi vya SMZ.

Amesema mara ya kuchaguliwa na kuingia madarakani atapandisha mshahara kwa kima cha chini kuwa shilingi laki tano (500,000), na baada ya kipindi chake cha miaka mitano kumalizika, atahakikisha mtumishi wa ngazi ya chini anapokea shilingi laki saba na elfu hamsini ( 750,000).

Aidha amesema ataimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Umma, ili waweze kuwajibika katika kiwango kizuri wanapokuwa wanatoa huduma kwa wananchi.

Amesema kumekuwepo na malalamiko ya ubaguzi katika ajira hivyo akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha ajira zote zinazotolewa zinafuata utaratibu wa kisheria.

Kwa upande mwengine amesema kumekuwepo na malalamiko ya makato kwa wafanyakazi wa umma hasa vikosi vya SMZ kukatwa fedha kwa ajili ya michango ikiwemo kwenye michezo hivyo akichaguliwa ataondosha makato yote yasiyo ya lazima kwa watumishi wa umma.

               mwisho