Mgombea urais Zanzibar ADA-TADEA kutenga bajeti ya michezo akipata ridhaa

 

IMEANDIKWA NA MWANTANGA AME- ZANZIBAR

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, amesema anakusudia kuinua sekta ya michezo, kwa kuweka bajeti maalum ya kuendeshea ligi kuu ya Zanzibar, badala ya kusubiri wafadhili.

Alisema hayo ikiwa ni sehemu ya kampeni zake, zinazoendelea kufanyika kisiwani Unguja na Pemba kwa kujiandaa na Uchaguzi Mkuu utaofanyika Mwezi Oktoba, mwaka huu.

Mgombea huyo, alisema sekta ya michezo, inahitaji kuangaliwa zaidi, na atakapoingia madarakani atachukua uamuzi wa kuwa na bajeti ya ligi kuu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuifanya ligi ya Zanzibar kutokuwa na vikwazo, kwani hivi sasa michezo inakufa kutokana na kutegemea wafadhili.

Alisema atakapoweka utaratibu huo, wafadhili watakaosaidia watapewa nafasi, lakini hataiondoa bajeti ya serikali katika michezo.

Alisema katika michezo kunahitaji misingi mizuri kuazia ngazi ya skuli za msingi hadi sekondari, ikiwa ni hatua itakayowezesha kupata wachezaji wazuri wa baadae, kwa vile michezo ni sehemu ya ajira ndani na nje ya nchi.

“Nakusudia kuanzisha akademi za michezo ambazo zitaongozwa na wazalendo kama Ali Bushiri au Seif Bausi,  watazisinamia vizuri kuzalisha vipaji na kurejesha michezo ya zamani kama mpira wa Vinyoya (badminton), iliyotupa sifa nyingi, lakini hivi sasa imekufa” alisema Khatib.

Aliongeza kuwa pia atasimamia ligi ya wanawake ambayo hivi sasa inaenda kwa kusua kusua licha ya Zanzibar kuwana vipaji vingi na vizuri vya wanaoweza kucheza mpira huo.

Alisema inasikitisha kuona timu za wanawake zimekuwa zinakosa kupewa msukumo katika ligi yao, jambo ambalo limekuwa likichochea kuuwa vipaji vyao. (CHANZO: ZANZIBAR LEO)