Mgombea uwakilishi Chambani ataka tena ridhaa aitekeleze ilani ya CCM 2020/2025

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA uwakilishi Jimbo la Chambani wilaya ya Mkoani Pemba, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Bahati Khamis Kombo, amewaomba wananchi wa jimbo hilo, kumrejesha tena madarakani, ili aitekeleze Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kama alivyofanya kwa ile ya mwaka 2015/2020 kwa kipindi kilichopita.

Alisema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, alifanikiwa kuwapelekea huduma kadhaa wananchi wa vijiji vya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na huduma ya umeme, maji safi na salama.

Mgombea huyo wa uwakilishi wa jimbo la Chambani, ameyasema hayo, uwanj wa mpira wa kijiji cha Dodo Pujini kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni, wa chama hicho.

Alieleza kuwa, kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 jimbo la Chambani, aliling’arisha kwa kujenga skuli za msingi na maandalizi, uwekaji wa kifusi kwenye barabara za Wambaa- Kwazani na kuwarahisishia wananchi usafiri.

Alifahamisha kuwa, aliwachimbia kisima wananchi na wanafunzi wa skuli ya Ukutini na kulaza mipira ya kusambaazia huduma ya maji safi na salama, sambamba na huduma ya nishati ya umeme.

“Nilipoingia madarakani, nilikabidhiwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 na kuipeperusha vyema, kwa kuwafanyia mambo mazuri wananchi, tena bila ya ubaguzi, maana hiyo ndio dira na sera ya chama hichi,’’alifafanua.

Mgombea huyo alifahamisha kuwa, kutokana uhaba wa fedha za mfuko wa jimbo, alilazimika kutumia fedha zake, ili kuhakikisha anawatumikia kwa dhati wananchi wa Jimbo hilo.

“Bara bara ya kijiji cha Kumvini- Kibaridi niliijenga kwa kiwango cha lami, sambamba na kusimamia ujenzi wa barabara kuu ya Ole –Kengeja, pamoja na vituo vya mama na mtoto,’’alieleza.

Hivyo, amewataka wananchi wa Jimbo hilo, kumpa ridhaa kwa kumpigia kura ili ashike tena nafasi hiyo, na kuahidi kuliimarisha jimbo hilo.

Alieleza kuwa, yapo baadhi ya miradi ambayo hayajakamilika vyema, hivyo akipewa ridhaa, ataendelea kushirikiana na wananchi na madiwani ili kuikamilisha.

Kwa upande wake mgombea wa ubunge wa Jimbo hilo Mohamed Abrhaman Mwinyi, amesema kama akipewa ridhaa atahakikisha baadhi ya bara bara za ndani anazijenga.

“Mkinichagua kuwa mbunge wa Jimbo la Chambani, nitahakikisha bara bara zote za ndani, nitazijenga kwa kiwango cha kifusi, maana hata kwenye ilani, imetaja uimarishaji wa miundombinu,’’alifafanua.

Mapema Katibu wa CCM wa mkoa wa kusini Pemba Mohamed Ali Khalfan, amesema ikiwa wananchi wa jimbo hilo wanataka maendeleo, wasisite kuwapigia kura mgombea ubunge, uwakilishi na udiwani wa Jimbo la Chambani.

Alisema, kwa maendeleo ya kitaifa yatakelezwa bila ya ubaguzi na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, sambamba na mgombea urais wa Zanzibar Dk. Ali Hussein Ali Mwinyi, na jukumu la wabanchi ni kuwapigia kura.

Mjumbe wa kamati ya CCM ya mko wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, amewahakikisha wananchi wa mkoa huo, kuwa watakwenda kwenye uchaguzi kwa amani.

Alisema, hataki kuona mwananchi anazuiwa na mtu kundi watu ili wasitekeleze haki yao ya kuchagua, kwa kuimarisha ulinzi katika kipindi chote.

Mwisho