Mgombea uwakilishi Wete kuling’arisha jimbo akipata ridhaa

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA Uwakilishi jimbo la Wete Pemba, Harusi Said Suleiman, amesema kama wananchi wa jimbo hilo, wakiamua kumrejesha tena kwenye nafasi hiyo, ataimarisha huduma za maji safi na salama na kuendeleza miradi, ambayo aliianza miaka mitano iliyopita.

Alisema, kazi kubwa imefanywa na CCM ndani ya Jimbo la Wete, ingawa kwa vile maendeleo hayatoshi, ndio maana amewaomba kumpigia kura tena, ili kumalizia miradi ambayo haijakamilika.

Mgombea huyo uwakilishi aliyasema hayo, kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika Bopwe jimboni humo, ikiwa ni katika harakati za kampeni, kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

Alieleza kuwa, miradi kama ya maji safi na salama, anataka kuyaimarisha zaidi, kwa ujenzi wa matenki ili kuwahakikishia wananchi huduma hiyo kwa saa 24.

“Nyinyi wananchi wa Jimbo la Wete nawaombeni sana minirejeshe tena kwenye nafasi ya uwakilishi wa Jimbo hili, ili nishirikiane na serikali kuu, katika kuwaletea maendeleo zaidi,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa uwakilishi wa jimbo la Wete, alisema anayokazi kubwa ya kuviimarisha vikundi vya ushirika vya wanawake na vijana.

Alisema, kama akipata ridhaa na kuliongoza tena jimbo hilo kwa miaka mitano ijayo, hata kundi la watu wenye ulemavu nalo atalijengea mazingira, ambayo yatarahisisha kazi zao.

Kuhusu aliyoyafanya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, mgombea huyo anaetetea kiti chake, alisema ni pamoja na ujenzi wa vyumba kadhaa vya madarasa.

“Lakini pia nilifanikiwa kuujenga mtaro wa uliyopo kijiji cha Bubujiko, ambako kulikuwa kukitokezea mafuriko kila mvua zinaponyesha, na sasa hali imetuliwa,’’alieleza.

Hata hivyo mgombea huyo, aliwaomba wananchi wa Tanzania kuhakikisha wanawapigia kura za ndio, wagombea wote wa CCM, kuanzia diwani hadi rais wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo, Juma Shaaban Juma, alisema kama akipewa ridhaa ya kulioongoza jimbo hilo, atahakikisha anashirikiana na wizara ya elimu kuimarisha huduma za maktaba.

“Elimu ya sasa inategemea sana uwepo wa maktaba za kisasa, hivyo kama nikipewa ridhaa, nitashirikiana na wizara ya elimu kuona, maktaba yetu inaamirika,’’alieleza.

Aidha mgombea huyo wa ubunge, alisema kutokana na uwepo wa barabara kadhaa za ndani, ambazo kwa siku za mvua hupita kwa tabu, atazishughulikia.

“Kura zenu nimiminieni mimi na musijemkawapa wagombea ambao hawana dira, maana nataka kuzijenga na kupitika vyema barabara zote za chochoroni ndani ya jimbo la Wete,’’alieleza.

Hata hivyo amewaahidi wananchi wa jimbo hilo, kuwa suala la michezo, vikundi vya mazoezi, mafundi wa mitaani na wasanii atawapatia vifaa, ili kuendeleza kazi zao.

Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba Khadija Abdi Nassor, aliwatahadharisha wapiga kura wa Tanzania, kuwa wasijefanya makosa, kwa kuvitilia kura vyama ambavyo havina ukweli.

“Tulikuwa na wabunge na wawakilishi kutoka vyama vya upinzani kwa miaka zaidi ya 15, na hatukuona waliyoyafanya, sasa kura zenu wapeni wagombea wote wa CCM,’’alieleza.

Mapema mjumbe wa Kamati ya siasa ya Mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, alitumia hadhara hiyo, kuwaombea kura wagombea wote wa CCM.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, wamesema miaka mitano ya Mwakilishi wa Jimbo la Wete, anayemaliza muda wake Harusi Said Suleiman, inatosha kama ni ushahidi kuwa anaweza kuongoza.

Asha Mussa Hassan na Mwadini Haji Mmanga, walisema lazima wawashawishi wenzao, kuona wanawapigia kura wagombea hao wa CCM.

Mwisho