Polisi Wete wapokea matukio 30 ya udhalilishaji kwa miezi mitano

 

Kabla ya kuisoma habari hii, jua unachopaswa kujua

IMENADIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

Kesi 30 za udhalilishaji wa kijinsia zikiwemo za ubakaji na ulawiti, zimeripotiwa katika Dawati la wanawake na watoto la Wilaya ya Wete Mkoa kisiwani Pemba, kuanzia kipindi mwezi wa Januari hadi Mei mwaka huu.

 

Akiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa vitendo hivyo kwa wajumbe wa mtandao wa kupinga udhalilishaji Wilaya ya Wete, Afisa Dawati kutoka Jeshi la Polisi Wete, Nadya Hilal Mfaume, amesema kati ya kesi hizo 30, kesi 20 zipo Polisi huku kesi nne (4) zimefungwa na sita (6) zinaendelea Mahakamani.

 

Amesema, katika kipindi hicho kesi ubakaji zilioongoza kwa kufikia 17 zikifuatiwa na kesi za kutorosha watoto wa kike zilizokuwa (7)  pamoja na shambulio la aibu kujjiri kesi nne (4).

 

Katika hatua nyingine amesema kesi hizo zilizoripotiwa katika kipindi hicho hakuna kesi yoyote iliyopata hatia kupitia mahakamani.

 

Kwa upande wake Rashid Hassan Mshamata, kutoka Jumuiya ya waaidizi wa sheria wilaya ya Wete amesema kati ya kesi hizo, Jumuiya hiyo imefanikiwa kushiriki kuibua kesi 10 ambazo zinahusisha ubakaji, ulawiti utelekezaji, ujauzito pamoja na biashara ya ngono.

 

Katika kuhakikisha mtandao huo unazifuatilia kesi hizo pia umejumuisha wajumbe kutoka Wilaya ya Micheweni ambapo kumeripotiwa jumla ya kesi 12 na  kati ya kesi hizo nne zinahusisha mimba kwa wanafunzi wa skuli.

 

Kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA, Zanzibar -Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said amewataka wajumbe wa mtandao huo, kuendelea kuzifuatilia kesi hizo kwa ukaribu hasa katika kipindi hiki cha uwepo wa virusi vya Corona.

Ameongeza kwa kuwataka kufanyakazi kwa ukaribu na waathirika wa vitendo vya udhalilishaji, ili kuwahamasisha na kuwashawishi kujitokeza kutoa ushahidi Mahakamani pindi wanapohitajika.

Aidha Mratibu huyo, alisema wahariri wa vyombo vya habari wananafasi kubwa ya kutokomeza matendo hayo, kwa kule kuwatuma na kufuatilia kwa karibu matendo hayo mwanzo hadi mwisho.

Ripoti hizo ni utekelezaji wa Mradi wa Jukwaa la wanahabari la kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – TAMWA, Zanzibar kwa ufadhili wa Danish International Development Agency (DANIDA).

Mama mmoja wa shehia ya Bopwe wilaya ya Wete, aliyekuwa na kesi ya mwanawe ya utoroshaji na kisha mtuhumiwa kukosa kutiwa hatiani, baada ya aliyekuwa mumewake kuharib ushahidi, alisema kama wanawake hawakuwa makini, wanaweza kuendelea kudhalilishwa wao na watoto wao.

Mwanasheria dhama wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kisiwani Pemba Ali Rajabu Ali, alinukuliwa akisema kuwa, kama jamii haikuacha rushwa muhali, wasitarajie watuhumiwa kutiwa hatiania na mahakama.

Mtoto aliyewahi kulawitiwa mwaka 2018 wa shehia ya Mchanga mdogo, alisema kama majaji na mahakimu hawakufuata kikamilifu sheria ya Adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa wanaowadhalilisha, jamii isitarajie mabadiliko.

Muu wa Mkoa wa kaskazini Pemba Omar Khamis Othman, alisema suala la kutoa ushahidi mahakamani ni miongoni mwa njia moja wapo kubwa, ya kuyamaliza matendo hayo kwa wanawake na watoto ndani ya jamii.

Mrajisi wa mahakama kuu Zanzibar kisiwani Pemba ambae ni hakimu wa mahakama ya Mkoa Chake Chake Abdull-razak Abdull-kadir Ali, alieleza kuwa suala la kuyaripoti matendo hayo ni moja, lakini pili ni kutoa ushahidi wa kweli mahakamani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Pemba, zinaeleza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu cha Januari hadi Machi mwaka 2019, Pemba kuliripotiwa matukio 54, ambapo kati ya hayo wilaya ya Wete ilikuwa matukio 25.

Matukio mengine 13 yaliripotiwa kutoka wilaya ya Chake Chake, huku wilaya ya Mkoani ikiripoti matukio tisa (9) na Micheweni ikiripoti matukio saba (7), ambapo matukio yote hayo yanahusu udhalilishaji wa watoto waliyochini ya miaka 18.

Kati ya matukio hayo 25 ya wilaya ya Wete, matukio tisa, (9) yalikuwa ya ubakaji, sita (6) utoroshaji, mimba za umri mdogo na shambulio ya aibu zilikuwa tatu tatu, huku ulawiti na shambulio la kuumizwa mwili, yakiwa mawili mawili.

mwisho