Mikononi mwa Polisi kwa tuhuma za ubakaji mtoto wa miaka 4.

Imeandikwa na Salmin Juma – Pemba.

Email: salminjsalmin@gmail.com

Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA upande wa Zanzibar ofisi ya Pemba kimewataka wananchi wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wasirudi nyuma kwenda kutoa ushahidi mahakamani ili kesi hizo zipatiwe hukumu na iwe fundisho kwa wengine.

Kauli hiyo imetolewa jana Afisa uwendeshaji (Program Offcer) wa chama hicho huko Pemba Bi Asha Mussa Omar alipokua akizungumza na mwandishi wa habari  hizi juu ya kuongezeka vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto kisiwani humo huku akigusia tukio la udhalilishaji linalodaiwa kufanywa na kijana  Andrew Joseph Frank (20) mkaazi wa Kiungoni kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa kike mwenye miaka minne huko Kiungoni Wilaya ya Wete Pemba.

Bi Asha alisema, hali imekua mbaya nchini kwakua mara nyingi kumekua kukiripotiwa matukio hayo huku akiwataka wazee na wanafamilia ya mtoto huyo wasimame kidete kutetea haki yao na wasirudi nyuma hasa kwenda kutoa Ushahidi.

“matukio haya yanaendelea kwakua watu hawendi kutoa ushahidi hii ndio sababu, kesi inapoanza watu wanakua wengi lakini kadiri inavyoendelea wengine wanajitoa, haitakiwi hivyo, wasimame kutetea haki ya mtoto wao hadi mwisho” alisema Bi Asha.

Kwa upande wake Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa mkoa huo Shehan Mohamed Shehan alithibitisha kumshikilia kijana huyo Andrew Joseph Frank (20)  na alisema tuhuma za ubakaji za tukio hilo limetokea Novemba 11 mwaka huu saa 11:00 jioni.

Alisema, maelezo yanaeleza kuwa, mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo wa miaka 4 na kwenda nae katika mabwawa ya chumvi yaliyopo Kiungoni na kuanza kumfanyia ukatili huo.

“alimchukua mtoto huyu na kwenda kumbaka, kwa kweli alimuathiri sana kwa sababu bado ni mdogo” mwisho wa kunukuu.

Kamanda Shehan alisema, upelelezi wa kesi hiyo umeshakalika na muda wowote kuanzia sasa  mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mmoja miongoni mwa wananchi kutoka huko Kiungoni, ambae hakupenda jina lake lichapishwe mtandaoni alisema, hali inazidi kutisha na amewataka wadau wanaopinga vitendo vya udhalilishaji nchini wazidishe kasi katika kuwaelimisha.

“hivi sasa ni mtihani sana, wadau tunaziona jitihada zenu, lakini na hawa jamaa nao wanazidisha jitihada zao za ubakaji, jitahidini sana watoto wetu wanaumia” alisema mwanamke huyo.

Kubaka ni kosa kisheria kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha Sheria ya adhabu, Sheria namba 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzinar.