Mkanyagano mwengine watokea, wanafunzi 15 wafariki dunia

 

Idadi ya Wanafunzi waliopoteza maisha baada ya kukanyagana katika shule ya msingi Kakamega nchini Kenya imefikia 15.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Kakamega, bwana David Kabena amesema kuwa wanafunzi wengine 39 walijeruhiwa na 20 wamepata matibabu tayari.

Inadaiwa kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

Zaidi ya wanafunzi 100 wanatibiwa na wengine wako kwenye hali mbaya.

Mkanyagano huo ulitokea baada ya kengele ya kumaliza masomo kupigwa na wanafunzi walikuwa wakitoka kuelekea nyumbani.

Ripoti zinasema kuwa wanafunzi hao walikuwa wakitoka katika madarasa yao mwendo wa saa kumi na moja jioni wakati mkasa huo ulipotokea.

Imedaiwa kwamba baadhi yao walianguka kutoka ghorofa ya tatu ya jengo hilo walipokuwa wakitoka darasani.

Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa wanafunzi wawili wamepelekwa katika chumba cha dharura katika hospitali iliyopo kaunti ya Kakamega.

Wazazi wamekusanyika hospitalini wakiwa na hofu kuwa inawezekana kuna wanafunzi wengi zaidi wamejeruhiwa.

Wengi waliumia wakati wakijaribu kutoka kwenye jengo la shule. (bbc)