Moto ulivyoteketeza bidhaa za shilingi milioni 50 Mtambile Pemba

 

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

SIKU moja baada ya maduka matatu na ghala moja kuteketea kwa moto sokoni Chakechake, bidhaa nyingne za wafanyabiashara wawili wa Mtambile Mkoani zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50, nazo zimeteketea kwa moto.

Moto huo ulioripotiwa kutokea baina ya majira ya saa 6:00 na saa 6:30 mchana wa August 2, uliunguza bidhaa kadhaa za mfanyabiashara Massoud Salum Abdalla ‘ndevu’ ambapo moto huo ndimo ulimoanzia.

Mfanyabiashara huyo alisema anawasiwasi mkubwa kwamba, moto huo uliotetekeza bidhaa zake, umesabishwa na hitilafu ya umeme ndani ya duka lake.

Baadae moto huo ulihamia dukani mwa jirani yake Kassim Juma Kassim, ambapo licha ya msaada mkubwa wa wananchi kutoa bidhaa nje, lakini amekula hasara ya zaidi ya shilingi milioni 5.

Alisema kama wengetokezea wameshafunga duka wengeteketeza kila kitu na kisha kuhamia duka jengine kubwa ‘super market ’ ilioko jirani na duka lake.

Nyumba hiyo yenye maduka mawili, ofisi ya ACT, pia moto huo umesababisha hasara ya zaidi ya shilingi million 5 kwa Abdalla Bahari ambae anaishi nyuma kwenye nyumba hiyo.

Alisema vifaa vyake alivyovikosa kabisa ni magodoro, vitanda, nguo na vyombo vya kawaida vya matumizi ya ndani.

Katika tukio hilo hakuna mtu aliejeruhiwa, ambapo familia ya Abdalla kwa sasa iko matembezeni, jambo lililoleta usalama wakati wa tukio hilo.

Mwandishi wa habari mwandamizi Mohamed Khalfan  mkaazi wa Mtambile, alisema licha ya Kikosi cha zima moto na uokozi kufika baada ya tukio hilo, lakini walichofanikiwa ni kuudbiti moto usiendelee nyumba za majirani.

Alisema kwa nyumba hiyo iliokuwa na maduka mawili na iliokuwa ikiishia familia moja, hakuna kilichobakia na jengo lote limeteketea kwa moto.

Mwandishi huyo alisema, jengo ambalo linamilikiwa na Abdalla Nassor, anasema wastani wa shilingi milioni 100 zimempotea kwa nyumba yake kuteketea kwa moto.

Mashuhuda wengine wa tukio hilo akiwemo mmiliki wa duka ulimoanzia moto huo, Massoud Salim Abdalla ‘ndevu’ alisema aliona moshi kwenye moja ya viungio vya umeme dukani mwake.

“Baada ya kuona hivyo nilijua sasa duka linataka kuwaka nikaita watu na kuanza kutoa bidhaa nje, pamoja na msaada wa wananchi, lakini nimepata hasara ya zaidi ya shilingi 40,’’alifafanua.

Picha ya kushoto jengo likiingia moto, KULIA baada ya jengo hilo kuungua moto

Nae mmiliki wa duka ambae aliwahi kutoa baadhi ya bidhaa Kassim Juma Kassim, alisema moshi mkali uliokuwa ukitokea kwenye duka na Ndevu ndio uliompa ishara kuanza kutupa vitu nje.

“Watu wengine walikuja kunisaidia mimi kutoa bidhaa nje na wengine walikuwa kwa ndevu, hivyo mimi afadhali hasara yangu ni wastani wa shilingi milioni 5’, alifafanua.

Walisema hawakuzembea baada ya kuona moshi unazidi kwa kasi walichukua hatua ya kuwapigia kikosi cha zima moto na uokozi wilaya ya Mkoani na baada ya dakika 20 walifika.

Nae Mohamed Rajab Hamza, alisema kama sio juhudi za wananchi kuzima moto huo na wengeamua kuvisibiri vikosi vya zima moto na uokozi hasara yengekuwa kubwa zaidi.

“Zimamoto walichelewa kidogo na walipofika wanadai maji yamewaishia sasa, walipofika tayari maduka na jengo lote limeshateketea kwa moto,’’alieleza.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba Hassan Nassir Ali alithitisha kutokea kwa tukio hilo, na kuwataka wafanyabiashara ambao wamepata hasara kuwa na moyo wa ustahamilivu.

Alisema yote hiyo ni mipango ya Muumba, hivyo kwanza washukuru kwamba roho zao zimesalimika na hakuna alieathirika na tukio hilo.