Mtuhumiwa: “Nilibambikiziwa bangi kituo cha Polisi Chake Chake”

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTUHUMIWA Omar Othman Ismail wa Chambani wilaya ya Mkoani, ameiambia Mahakama ya Mkoa ‘B’ Chake Chake kuwa, misokoto 85 ya majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi, sio ya kwake ila alibambakiziwa na askari ndani ya kituo cha Polisi Chake Chake, baada ya kukataa kutoa  rushwa.

Alidai hayo mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Luciano Makoye Nyengo, wakati akitoa utetezi wake, juu ya kukamatwa na misokoto hiyo, tokea mwezi Mei mwaka jana, yenye uzito wa gramu 377.7

Alidai kuwa, kabla ya kukamatwa na Polisi wa kitengo cha kupamba na dawa za kulevya eneo la Chambani majira ya saa 7:30, walimtaka awapeleke sehemu au nyumba inayouzwa dawa za kulevya aina ya bangi.

Mtuhumiwa huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa, baada ya kuvutana kwa muda huku akiwakatalia, ndipo ghafla walipomfunga mikono yote miwili kwa pingu na kisha kumpakia kwenye piki piki.

Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa, wakati wanakwenda kituo cha Polisi Chake Chake, walimtaka awape kiasi fulani cha fedha ili wamuachie, ingawa aling’ang’ana hadi kufiki kituoni.

“Tokea tunaondoka sasa Chambani, huku mimi nikiwa na pingu, askari hao ambao walijitambulisha kwangu, walinitaka nitoe fedha, vyenginevyo kitakachonikuta nitajuta, lakini na mimi sikutoa hata shilingi moja,’’alidai mahakamani hapo.

Hivyo alidai kuwa, hahusiki na kesi hiyo ya bangi, kutokana na siku ya kukamatwa kwake, hakuna mzigo wa aina yoyote aliokamatwa nao na hakuna shahidi wowote.

Mtuhumiwa huyo, aliendelea kuishawishi mahakama kuwa, hahusiki na misokoto hiyo, na anachofahamu yeye ni kukabidhiwa ndani ya kituo cha Polisi Chake Chake, baada ya kukataa kutoa fedha ‘rushwa’.

“Mimi hadi naingia ndani ya kituo cha Polisi, nimefungwa pingu na hadi nahojiwa kwa mara ya kwanza, sina mzigo, lakini baada ya kukataa kutoa fedha, ndio nikandikishiwa misokoto 85 ya bangi,’’alidai.

Baada ya kumaliza kutoa utetezi wake mtuhumiwa huyo, Hakimu wa mahakama hiyo Lucaino Makoye Nyengo, aliiuliza upande wa mashitaka, ikiwa una maswali yoyete kwa mtuhumiwa huyo.

Ndipo Mwendesha Mashtaka huyo kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Seif Mohamed Khamis alipomuuliza mtuhumiwa huyo, sababu za yeye kukamatwa na Polisi.

Aidha wakili huyo wa seriakli, alimuuliza mtuhumiwa huyo iweje kama bangi hiyo sio ya kwake, ashindwe kuwauliza Polisi wakati walipofika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao dhidi yake.

“Wewe unajitetea kuwa, mzigo wa bangi uliokamatwa nao sio wa kwako, lakini mbona hao Polisi wa kupambana na dawa za kulevya, walipokuja hapa mahakamani hukuwauliza suali hili la msingi,’’alihoji.

Hata hivyo baada ya Hakimu wa mahakama ya Mkoa ‘B’ Chake Chake Luciano Makoye kuliahirisha shauri hilo, alimtaka mtuhumiwa huyo kurudi rumande, na kuwasilisha mashahidi wake wawili wiki mbili zijazo ndani ya mwaka huu, kesi yake itakaponguruma tena.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Mei 15 mwaka jana majira ya saa 7:30 mchana, alipatikana misokoto 85 ya majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 377.7.

Mtuhumiwa Omar Othman Ismail, alipatikana na misokoto hiyo mchana eneo la Chambani wilaya ya Mkoani Pemba, na Polisi wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, wilaya ya Chake Chake, baada ya kumtilia shaka.

Ambapo hilo ni kosa kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria Udhibiti wa dawa za kulevya  sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 11 (a) cha sheria nambari 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.

Mwisho