Mwanamke anusurika kifungo kwa kuingiza mbwa msikitini

 

Mwanamke mwenye akili punguani amenusurika kifungo jela nchini Indonesia kwa kukufuru baada ya kumbeba mbwa na kumuingiza msikitini.

Kanda ya video ya Suthe Margaret akiingia msikitini akiwa amevalia viatu kabla ya kumruhusu mbwa wake ndani ya msikiti huo ilisambaa mwezi Julai.

Ilizua hasira katika taifa hilo lenye Waislamu wengi ambapo mbwa huonekana kuwa kitu kichafu.

Jopo la majaji mjini Bogor , mji uliopo karibu na mji wa Jakarta, lilimpata na hatia ya kukufuru siku ya Jumatano lakini akasema kwamba hawezi kuhukumiwa kwa kitendo chake.

Margaret anaugua ugonjwa wa paranoid schizophrenia, kulingana na uchunguzi wa kiakili mwaka 2013.

Waendesha mashtaka wametaka apatiwe kifungo cha miezi minane jela.

Ni nini kilichotokea katika kanda hiyo ya video?

Mwaamke huyo ambaye anaonekana kuwa na tatizo la kiakili anaingia katika msikiti katika eneo la Bogor akisema kwamba yeye ni Mkatoliki na kuongezea kwamba mumewe atafunga ndoa msikitini baadaye siku hiyo.

Anaushutumu msikiti kwa kumbadilisha dini huku mbwa huyo akimzunguka.

Watu kutoka msikiti huo wanasema kwamba hawatambui harusi hiyo.

Mwanamke huyo baadaye anampiga teke bawabu wakati anapoambiwa kuondoka. Mbwa huyo baadaye alifariki baada ya kugongwa na gari. (bbc)