Mwendesha mashtaka, Hakimu wakwamisha kutoendelea kesi ya ‘Ronaldo’ Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

KUTOKUWEPO kwa hakimu na mwendesha mashitaka wa mahakama ya wilaya ya Chakechake, imesababisha kutotolewa kwa uamuzi ‘ruling’ juu ya tuhuma za kupatikana na nyongo moja yenye uzito wa gramu 0.0140, inayomkabilia Khamis Ali Othman ‘Ronaldo’ miaka 29.

Hivyo, baada ya mtuhumiwa huyo kuwasili mahakamani hapo, ilibidi kesi yake kwa muda ihamie mahakama ya mwanzo, chini ya hakimu Hashim Kassim akisaidiwa na mwendesha mashitaka kutoka Jeshi la Polisi sajenti Juma Habibu. na kisha kulighairisha shauri hilo.

Mara baada ya mtuhumiwa huyo kuwasili mahakamani, hakimu alimuuliza mwendesha juu ya hatua ya kesi hiyo, na kudai kua ni ya kutolewa uamuzi, ingawa mwendesha mashitaka husika hayupo mahakamani.

“Muheshimiwa, shauri hili ambalo mtuhumiwa yuko mbele yako, lipo kwa ajili ya kutolewa uamuzi ‘ruling’ lakini mwendesha mashitaka amedharurika,’’alidai mahakamani hapo.

Hivyo Sejent Juma, ameiomba mahakama hiyo  kulighairisha shauri hilo, na kuangalia uwezekano wa kulipangia tarehe nyingine, na siku hiyo litakuwa na mwendesha mashitaka husika.

Hakimu wa mahakama hiyo ya mwanzo, Hashim Kassim alimuuliza mtuhumiwa ikiwa ameyasiki vyema maelezo hayo na kujibu ndio.

“Kama umeyasikia, kwamba mwendesha mashitaka wa shauri hili hayupo, pia vile vile hata hakimu husika leo hakufika, hivyo hatuwezi kufanya uamuzi, lakini wewe njoo tena Feabuari 3, mwaka huu,’’alisema hakimu.

Kupatikana na dawa za kulevya ni kosa kinyume kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria no 9 ya mwaka 2009, kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria no 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.

                        Mwisho