Mwenye miaka 83 aendelea kufundisha skuli

 

Umri wa kustaafu kisheria kwa wafanyakazi wa Umma, pamoja na waalimu nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ni miaka 65, lakini Bibi Bernadette lukoki , ana umri wa miaka 83, licha ya uzee wake, anaendelea na kazi ya kushika chaki

Kila siku , bibi huyu amekuwa akiiomba serikali kumkumbuka ili apumzike hivi sasa,kwa kuwa afya yake imeanza kudhoofu.Mwandishi wetu wa kinshasa Mbelechi Msoshi alimfuata darasani ili ajionee jinsi anavyofundisha.

Mzee huyu anafundisha darasa la kwanza, wanafunzi wake humuita Bibi, kwani wengi wake ni kama wajukuu.

”Kulingana na miaka mingi niliyofundisha ninajua namna ya kufanya ili wakae kimya na waelewe ninachowafundisha kwasababu ninapenda watoto wawe na ujuzi”.

Mwalimu huyu mwenye miaka 83 amekuwa kwenye kazi ya ualimu kwa miaka 66 .Lakini kwa sasa si kazi rahisi kwake.

Bibi Bernadette anaendelea kufundisha huku akisubiri malipo yake ya mwisho kutoka serikalini.

” Kwa kusema kweli,siwezi tena kuendelea kufundisha watoto kwa kuwa wazazi hawalipi tena ada ya shule ya msingi, hivyo kufanya idadi ya watoto kuongezeka, na kazi zimekuwa nyingi zaidi, inanibidi kumfuatilia kila mmoja” alieleza.

”Siwezi kubaki nyumbani, nilianza kazi hii tangu 1953 , na pesa ndogo nimepata hapa zimenisaidia.”

Ajuza wa miaka 80 anavyotumia lugha ya mtaani kuvutia wateja

BBC Ilijaribu kumuuliza Mkurugenzi wa shule ili kufahamu kwa nini mama huyu bado hajapumzika, Kongwaka Litela Yvone ni mkurugenzi wa shule ya msingi EP Mushi.

”Nimeshaitumia serikali jina la mama huyu kila mara kuomba astaafu lakini sipati jibu, mama huyu ameanza kutumika kabla ya mimi kuzaliwa, na ameendelea kutumika na mimi, ni ma mbo ya kusikitisha sana, kweli anafundisha vizuri, kulingana na umri wake anapaswa kupumuzishwa. Nimeomba viongozi wetu waangalie namna ya kumstaafisha mama huyu”.

Bi bernadette , amesema, hadi sasa hajapata matunda ya kazi yake, anaendelea kuishi katika hali ya umasikini kama kila mwalimu, mshahara wake ulifikia zaidi ya dola mia mwezi jana wakati rais rais alihaidi kurebisha maisha ya walimu.

Baada ya miezi nne baada ya kuapishwa kwake ; Raisi Felix Tshisekedi aliahidi kushughulikia wafanya kazi wa serikali ambao wamefikisha umri wa kustaafu. (bbc)